Wananchi na wamiliki wa viwanda katika eneo la
Salasala Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wamelilalamikia Shirika la
Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), kwa kushindwa kuwapa
huduma ya maji kwa takribani miezi mitatu sasa.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, wananchi hao
walisema awali Dawasco lilikuwa likiwapatia huduma hiyo kwa wiki mara
mbili, lakini kwa sasa limekatisha huduma hiyo bila taarifa yoyote kwa
wananchi kwa miezi mitatu.
Meneja Masoko wa kiwanda cha sabuni cha Family, Watambura
Chishagimbi, alisema kukosekana kwa huduma hiyo katika kipindi hicho
kimewaongezea gharama za uzalishaji kutokana na kununua kiasi kikubwa
cha maji kwa gharama kubwa, huku dumu moja la ujazo wa lita 20
wakilazimika kununua kwa Sh. 500.
Badhi ya maeneo yaliyoathirika na tatizo hilo ni makazi ya watu,
kiwanda cha kuzalisha biskuti, kuku, shule ya msingi Green Acres,
G&B Soap Industries Ltd, pamoja na wafanyabiashara wadogo
wanaozunguka eneo hilo kwa ujumla.
“Kwa muda wa miezi mitatu sasa tunaweza kupata maji siku moja kwa
wiki au tusipate kabisa, hivyo tunalazimika kununua maji kwa wachuuzi wa
magari ambapo lita 1,000 tunanunua kwa Sh. 15,000, hali hiyo inatuweka
katika wakati mgumu wa uzalishaji bidhaa,” alisema Chishagimbi.
Naye mkazi wa eneo hilo, Bakari Kitomari, alisema kukosekana kwa
huduma hiyo kumewaongezea makali ya maisha na kuiomba Dawasco kunususru
hali hiyo na kuishauri iwarudishe katika utaratibu wa awali kwa wiki
mara tatu.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa Dawasco, Evalasting Lyaro,
alisema eneo lililokumbwa na adha hiyo ni linalozunguka eneo la kampuni
ya IPTL, ambapo wananchi wamekosa huduma hiyo kutokana na bomba kubwa
la Ruvu kukaliwa na vifaa vigumu vilivyosababisha kushindwa kusukuma
maji.
“Hata hivyo, wananchi hao wategemee kupata huduma hiyo leo (jana),
baada ya wataalamu kufunga kijiko eneo la bomba lililosababisha tatizo
hivyo hakutakuwa mgawo kama awali,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment