Siku moja baada kuibuliwa
pendekezo na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza mishahara
watumishi wake, Mkurugenzi wa Masoko wa TPDC, Joyce Kisamo amesema fedha hizo hazijaombwa kwa ajili ya wafanyakazi wote na ametetea viwango hivyo kuwa vipo
chini ya hali halisi ndani ya sekta ya gesi na mafuta nchini.
Akifafanua pendekezo hilo katika
warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na shirika hilo jana na kuhusisha watumishi
wa Serikali na vyombo vya habari, Kisamo alisema mishahara hiyo imeombwa kwa
ajili ya watumishi maalumu watakaosimamia mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam.
Alisema watumishi hao watakuwa
wakifanya kazi katika mazingira magumu ya kushinda porini kwa zaidi ya siku 28
na kwamba uamuzi wa TPDC kuomba kiwango hicho cha fedha uliangalia ushindani wa
malipo katika soko. Alisema kuna wakati walitangaza kazi
kwa mameneja wa mradi huo, wengi walijiunga na TPDC kutoka Songas, lakini
baadaye baadhi walirudi walikotoka kutokana na walichotakiwa kulipwa kuwa chini
ya matarajio. “Watu wanashindwa kuelewa, fedha
hizi hatujaomba kwa ajili ya wafanyakazi wote ila ni kwa wale watakaohusika
kuendesha na kurekebisha mitambo ya usafirishaji gesi ambayo tumeigharimia kwa
fedha nyingi. “Mtumishi huyu anafungiwa kwenye
mitambo ili umeme usikatike au usumbufu wowote usitokee, hivi Sh12 milioni kwa
mwezi na familia yake inamsubiria inatosha…mimi bado kwangu ni kidogo,” alisema
Kisamo.familia yake inamsubiria inatosha…mimi bado kwangu ni kidogo,” alisema
Kisamo.
Jana gazeti dada la The Citizen
lilibainisha kuwa TPDC kupitia mpango wa mradi wa kusafirsha gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam imeomba kuwaongezea mishahara watumishi wake ambapo mtumishi
wa kima cha chini atatakiwa kulipwa Sh5.4 milioni na Ofisa Mkuu Mtendaji
kulipwa Sh36 milioni kwa mwezi. Pia, Watumishi hao katika pendekezo hilo
lililopelekwa Septemba kwa Baraza la Kutetea Walaji la Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura-CCC), watapatiwa marupurupu manono mbali na mishahara
hiyo. Watumishi wa kati wa shirika hilo,
nyaraka hiyo inapendekeza walipwe kati ya Sh12.6 milioni hadi Sh28 milioni
kiasi cha kuwafanya wafanane na maofisa Watendaji wa juu wa kampuni wanaolipwa
vizuri nchini.
Hata hivyo, Baraza la Kutetea Walaji
la Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura-CC) limeliita pendekezo hilo
la mishahara kuwa ni la “kusadikika” na “lisilo na uhalisia”. Huku akionyesha kusikitishwa na
kupingwa pendekezo hilo, Kisamo alisema kiwango hicho kitakachotolewa kwa
watumishi hao maalumu ni kidogo sana na wala hakifafanishwi na kile
wanacholipwa baadhi ya watalaamu wengine katika kampuni nyingine zilizopo ndani
sekta hiyo nchini.
Aliongeza; “sisi tumeangalia
industry (tasnia) ya ndani pekee na hiki kiwango tulichoomba kimeshushwa na
hakifanani hata kidogo na inayolipwa na Songas. Nimeongea na Ewura na kuwaleza
kuwa ‘tungediscuss’ (tungejadili) kabla ya kupelekwa nje kwenye mitandao.” Alisema kutokana na mashaka hayo
wananchi wanaweza wakalikataa ombi hilo na kusababisha kuwakosa watalaamu ambao
wangesimamia mitambo hiyo ya usafirishaji ambayo bila kusimamia na kuhudumiwa
mara kwa mara itaharibika mapema.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment