Social Icons

Pages

Friday, December 19, 2014

SOSEJI YA SAMAKI KUPAISHA UCHUMI KAGERA

Soseji ni kitafunwa ambacho wengi wamezoea kuona kinatengenezwa kutokana na nyama. Hata hivyo, kutokana na ubunifu mbalimbali wapo baadhi ya wajasiriamali wameanza kutengeneza soseji za samaki.
Mary Karega ni mjasiriamali aliyeanza kutengeneza soseji za samaki akiwa wa kwanza hapa nchini, baada ya kupata ufahamu wa namna ya kutengeneza soseji hizo kutoka nchini Uganda. Karega anasema kuwa alianza kutengeneza soseji mwaka 2012, baada ya kwenda kuhudhuria mkutano wa wadau wa samaki nchini Zambia.
Anasema mkutano huo, ulioandaliwa na mradi wa Smart Fish unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya kupitia Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO) unaofanya kazi ya kuhamasisha wavuvi na wananchi kuhusu masuala ya uvuvi, ulijumuisha wajasiriamali, kampuni na wafugaji wa samaki. “Nikiwa katika mkutano huo nilikutana na mtu anayetengeneza soseji za samaki, baada ya mkutano huo nilikwenda nchini Uganda alikokuwa ametokea ili kujifunza zaidi,” anasema.
Baada ya kujifunza anasema kuwa, alirejea hapa nchini na kutafuta wataalam waliosomea masuala ya chakula, na kukubaliana kuanzisha mradi huo kwa kutafuta mashine na kuanza mradi wa majaribio Juni 2012. “Baada ya kuanzisha mradi huo, wizara iliutambua na mwaka huo niliitwa kushiriki maonesho ya nane nane mkoani Dodoma, watu wengi waliofika katika banda langu walizionja na kuzipenda,” anasema.
Anasema kutokana na bidhaa hiyo ya soseji ya samaki alipata ushindi wa kwanza kwa wajasiriamali wadogo wachakataji wa bidhaa za samaki. Mwitikio ulikuwa mzuri na ndiyo maana aliona ni mradi wa kutilia mkazo. “Niliona ni bidhaa ambayo Tanzania inahitajika, kwa hiyo nikaanza mchakato wa kutafuta vibali kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) na Shirika la Viwango nchini (TBS).
TFDA  tayari wamempatia kibali mwaka huu na TBS mchakato wake unaendelea mwaka huu wametembelea kiwanda na kuona namna wanavyozalisha soseji. “Mchakato wa kupata kibali cha TBS unaendelea vizuri na uko katika hatua za mwisho za kutengeneza viwango vya soseji ya samaki ambavyo mwanzo havikuwapo,” anasema.
Sasa wameanza uzalishaji rasmi baada ya kuthibitishwa na TFDA na kuwa hali ya uzalishaji itaongezeka kadri soko litakavyoongezeka, kulingana na watu watakavyozidi kuifahamu bidhaa hiyo. “Masoko ya soseji yanategemea mikoa yote ya Tanzania, bado tunategemea soko la ndani, lakini tunasubiri cheti cha ubora kutoka TBS, ili bidhaa hiyo iweze kukubalika kwa walaji nje ya nchi,” anasema.
Anasema kuwa nchi kama Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wamekwishafanya nazo mazungumzo na kuwa wako tayari kununua bidhaa hiyo. Anasema mbali na soseji, anatengeneza chakula cha mifugo hasa kuku kutokana na mifupa na ngozi za samaki na pia anatengeneza mafuta ya samaki kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Ili kuhakikisha serikali inapunguziwa mzigo katika tatizo la ajira, kiwanda hicho kwa sasa kinatoa ajira kwa watu 30 lakini ajira hizo zinatarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya watu 100 kulingana na uzalishaji utakavyopanda.
Karega anasema kuwa, pamoja na jitihada hizo anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya bidhaa hiyo kutofahamika vizuri maana ni mpya katika soko. “Kutambulisha bidhaa mpya kunahitaji pia uwekezaji ili watu waweze kuifahamu, lakini pia sijapata mawakala kutoka katika mikoa mingine, ili bidhaa hii iweze kuenea katika maeneo mengi kwa muda mfupi,” anasema. Anasema ili kuboresha shughuli zake ana mpango wa kupata mashine za kisasa zaidi ili kuongeza uzalishaji. “Nalenga pia kuanzisha mradi wa kufuga kuku, kulima mbogamboga, kufuga samaki ili kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa samaki, ingawa kwa sasa halijaanza kuniathiri,” anasema.
Anasema kuwa hata kama kwa sasa tatizo la upungufu wa samaki halijaanza kumuathiri ana hofu ya kupata athari hizo baadaye, baada ya uzalishaji wa soseji kuongezeka. “Ndiyo maana nahitaji kuwekeza katika kufuga samaki, nchi kavu na ndani ya ziwa endapo sera za nchi zitakuwa zinaruhusu,” anasema Karega. Anasema sasa katika uzalishaji wake wa soseji anatumia samaki aina ya sangara, lakini siku za usoni analenga kutumia samaki wa aina tofauti ili kukuza na kulinda soko. “Kuna mtu inawezekana hapendi soseji zilizotengenezwa kutokana na sangara, huyo itabidi atumie za kambale au aina nyingine, ndiyo maana nina mpango wa kutumia samaki tofauti,” anasema. Anasema kuwa pia matumizi ya aina tofauti za samaki katika utengenezaji wa soseji mbali na kumfanya mtu kuchagua anahitaji soseji ya samaki gani, pia yanawezesha kukabiliana na changamoto ya upungufu wa samaki katika ziwa.
Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu, yalifanyika maadhimisho ya siku ya uvuvi duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika viwanja vya Gymkhana manispaa ya Bukoba. Miongoni mwa masuala yaliyozungumzwa ni namna gani wadau wa uvuvi wanaweza kuongeza thamani katika samaki na mazao mengine ya uvuvi na namna ya kukabiliana na vitendo vya uharamia ziwani. Aidha katika maadhimisho hayo, wavuvi walilalamikia uwekezaji wao wanaoufanya hasa katika maeneo ya visiwani kutopewa kipaumbele kama ilivyo katika sekta nyingine.
Alex Bakenjela akisoma risala kwa niaba ya umoja wa wavuvi mkoani humo alisema kuwa, uvuvi ni sekta muhimu inayotoa ajira kwa vijana na kuziwezesha halmashauri kupata mapato, lakini wamekuwa wakisahaulika katika kuboreshewa mazingira ya kufanyia shughuli zao. “Wavuvi tumewekeza sana visiwani, lakini uwekezaji wetu hautambuliki ndiyo maana pamoja na kuwapo kwa uwekezaji huo hatuwezi kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha,” anasema Bakenjela. Anasema kutokana na kuwapo kwa usalama mdogo unaochangia kuvamiwa na majambazi mara kwa mara, na kuporwa mali zao, Septemba 19 mwaka huu wavuvi walifanya harambee kwa ajili ya kununulia boti ya kufanyia doria.
“Katika harambee hiyo, tulipata Shilingi milioni 42 kati ya Shilingi milioni 57 zilizolengwa, tulinunua mashine na kuikabidhi polisi ili isaidie kufanya doria na kutufanya kuondokana na kuvamiwa na majambazi,” anasema.
Pamoja na jitihada za wavuvi pia serikali nayo inafanya kila jitihada ili kukomesha vitendo vya uharamia ziwani ambavyo mbali na wavuvi kuporwa mali zao pia baadhi yao wanauawa wakati wa uvamizi.
Katibu mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Yohana Budeba anasema kuwa, serikali inajitahidi kuweka mazingira ambayo yatadhibiti vitendo vya uvuvi haramu na uharamia majini, ambavyo kuharibu mazalia ya samaki na wavuvi kupoteza mali zao. “Suala la doria ni la gharama kubwa, sasa tumenunua maboti manne kwa ajili ya kufanyia doria, yamewekwa Mwanza, Mbamba Bay, Kigoma na Ikola, tutaendelea kununua vitendea kazi kulingana na bajeti itakavyoruhusu,” anasema Budeba.
Anasema katika mwaka wa fedha 2014/2015 zilitumika shilingi milioni 320 kwa ajili ya kununulia maboti hayo na mashine ya kufua umeme (generator) kwa ajili ya kuboresha mazingira katika baadhi  ya mialo. Kuhusu uongezaji wa samaki katika ziwa Victoria anasema kuwa serikali ya Tanzania, inaendelea kufanya mazungumzo na nchi jirani za Uganda na Kenya, ili waweze kukubaliana kufunga ziwa hilo kwa muda ili samaki waongezeke. “Ziwa linaajiri watu wengi, kwa hiyo siyo rahisi likafungwa ghafla, linaweza kusababisha athari nyingine ikiwamo kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, inabidi tuweke kwanza mazingira ya kuridhisha na tukubaliane nchi hizo ili wote tufunge kwa kipindi tutakachokubaliana,” anasema.
Saning’o Ole Telele ni naibu waziri wa wizara hiyo ambaye  anaona ili kuweza kupata manufaa, ni bora wavuvi, wafugaji wa samaki na hata wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi, kujiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili waweze kunufaika na huduma zitolewazo na mifuko hiyo.
Telele anasema kuwa kwa kuanzia serikali ilifanya mkutano mmoja baina ya wadau wa sekta ya uvuvi na mfuko wa hifadhi ya jamii nchini (NSSF), ili kuwapa wavuvi uono na uelewa kuhusu fursa hiyo muhimu katika maisha yao.
Aidha anasema kuwa wizara hiyo inaendelea na jitihada zake za kutoa mafunzo kwa wananchi hasa jamii ya wavuvi kuhusu ufugaji wa viumbe wa kwenye maji ili kuwezesha wananchi wengi kuwekeza katika sekta hiyo na kuachana na vitendo vya uvuvi haramu. Anasema sekta ya uvuvi ni muhimu kwa taifa maana inatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni nne ambao hushiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo na kuongeza protini kwa walaji.
“Hivi sasa wastani wa ulaji wa samaki kwa Watanzania unakadiriwa kuwa kilo 8 kwa mtu kwa mwaka, ikilinganishwa na kilo 16.8 kwa mtu kwa mwaka zinazopendekezwa na shirika la kilimo na chakula la umoja wa mataifa (FAO)” anasema, ili Tanzania iweze kunufaika zaidi na uvuvi, inabidi kuzingatia suala la kuongeza thamani katika samaki na mazao mengine ya uvuvi ili kuwa na uvuvi wenye tija badala ya uvuvi wa kuganga njaa.
“Wizara inatambua mchango wa kampuni ya Triple B Fish Sausage ya mama Karega wa Bukoba, kwa ubunifu wake amekuwa mzalishaji wa kwanza nchini wa soseji zinazotokana na malighafi ya mabaki ya samaki,” anasema Telele.
Anasema taarifa alizonazo ni kwamba TBS inaandaa viwango vya bidhaa hiyo mpya itokanayo na samaki na kuwa suala hilo wanalifuatilia kwa karibu kwani kuwapo kwa viwango hivyo mahsusi kwa ajili ya zao hilo, kutapanua wigo wa soko. Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, katika mwaka 2013 jumla ya tani 375,160 za mazao ya uvuvi yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.4 zilivunwa  nchini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: