Social Icons

Pages

Friday, April 17, 2015

MBINU ZA UANDISHI BORA

Ifahamike kuwa kila  kampuni  ya uchapishaji wa magazeti au vitabu na kampuni za televisheni na redio huwa na mtindo wao wa kuandika au kutangaza habari ambao ni tofauti kidogo na vyombo vingine katika matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Hata hivyo ziko mbinu ambazo ni za jumla kwa kila mwandishi ambazo hana budi kuzifuata kama kwa mfano matumizi ya tahajia ya maneno, miundo ya sentensi na mpangilio wa maneno. Tofauti zinazojitokeza ambazo hutumiwa na wachapishaji ama wa magazeti au wa vitabu zinazojulikana kama ‘House style’ ni ndogo na haziwezi kuathiri sana uandishi kwa jumla.

Mbinu Bora za Uandishi
Utangulizi
Kwa kuwa waandishi wengi wamesoma katika vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari, imeonekana  kuwa kuna haja ya kuwa na mwongozo wa uandishi bora na aina za mitindo inayotumika na kukubalika.
Mwongozo huu umejikita katika matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo msingi katika uandishi wa habari.
Ifahamike kuwa kila  kampuni  ya uchapishaji wa magazeti au vitabu na kampuni za televisheni na redio huwa na mtindo wao wa kuandika au kutangaza habari ambao ni tofauti kidogo na vyombo vingine katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Hata hivyo ziko mbinu ambazo ni za jumla kwa kila mwandishi ambazo hana budi kuzifuata kama kwa mfano matumizi ya tahajia ya maneno, miundo ya sentensi na mpangilio wa maneno. Tofauti zinazojitokeza ambazo hutumiwa na wachapishaji ama wa magazeti au wa vitabu zinazojulikana kama ‘House style’ ni ndogo na haziwezi kuathiri sana uandishi kwa jumla.
Maelezo yafuatayo yametokana na utafiti pamoja na ushauriano baina ya wataalamu wa lugha.

Maelezo
Msingi wa maelezo yaliyoandikwa umezingatia miongozo iliyowahi kutolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) siku za nyuma kama ilivyoandikwa katika machapisho yao kama kitabu cha “Jifunze Kiswahili Uwafunze Wengine,’ pamoja na ‘Mwongozo wa Uandishi’.
Kwa kuanzia ningependa kufafanua baadhi ya maneno yanayokanganya kiasi fulani wasomaji wengi kutokana na kushindwa kuyapambanua. Sababu kubwa ya mkanganyiko huu ni athari ya lugha za asili katika Kiswahili sanifu pia ni misingi mibovu wa sarufi ya Kiswahili inayosababishwa na walimu wa shule za msingi wasiokuwa na ujuzi wa kutosha katika taaluma katika fani ya Fonolojia, Fonetiki, Mofolojia, Semantiki na Sintaksia. Pia wako wale wanaoathiriwa na lugha za kigeni kama Kiarabu na Kiingereza. Lugha hizi za kigeni kimetufanya tuione lugha ya Kiswahili kama chotara wa lugha nyingine wakati lugha hii ina misingi ya lugha ya Kibantu. Nitaanza kufafanua baadhi ya maneno nna vifungu vya maneno kwa utaratibu wa kutumia alfabeti. Kwa mfano:

A
Ajali/ajari:  Ajali ni tukio lenye madhara yanayotokea ghafla. Ajari  ni malipo  kwa kazi ya ziada na jina linalofahamika ni ovataimu ambalo limetoholewa kutoka katika neno la Kiingereza la ‘overtime’.

Aidha/au /ama:
Neno aidha asili yake ni  Kiarabu na tangu likopwe, matumizi yake hayajabadilika. Kuna wakati tunalitumia kama waaidha. Watumiaji wengi wanafuata mtindo wa Kiingereza wa ‘either ... or’. Tunasoma kwa mfano: “Wataalamu  wa Kichina watabaki aidha bara au visiwani. Matumizi sahihi ni “Wataalamu wa Kichina watabaki ama bara au visiwani.
Maana ya aidha ni tena, basi, zaidi ya hayo, vilevile. Kwa mfano:
Kabla ya kwenda sokoni nitapitia aidha benki kuchukua   fedha. 
Ahirisha/hairisha: Neno sahihi ni ahirisha. Kuahirisha maana yake ni kuchelewesha jambo kwa makusudi ili lifanyike baadaye.
Adhima/azma: Neno adhima si neno sahihi la Kiswahili ila liko neno adhimisha ambalo maana yake ni kufanya sherehe ya kukumbuka kwa tukio fulani kama vile siku ya kuzaliwa, siku ya kufunga ndoa, siku ya kupata uhuru, n.k.
Neno lingine linalofafana na hilo ni adhimu ( kiv) –enye sifa, iliyotukuka, tukufu, jalili.
Azma ni jambo linalokusudiwa kufanywa, makusudio au lengo. Wakati mwingine huandikwa kama azima.
Alimradi/ilimradi: Haya ni maneno yenye maana moja. Maana yake ni ili, iwapo, kwa masharti kwamba,  mradi.
Aidha: Maana ya aidha ni vilevile, pamoja na hayo, pia, isitoshe n.k. Kuna wakati tunachanganya aidha na au katika sentensi moja. Hii inatokana na athari ya Kiingereza ya kutumia ‘either … or’... Kwa usahihi inatakiwa iwe ‘ama / au’ tunapotaka kulinganisha mambo.

B
Budi: Neno hili likisimama peke yake lina maana ya hiari. Tukisema ,”Wakulima ni budi walime” tuna maana  kuwa wakulima ni hiari walime.Tunatakiwa kusema “Wakulima ni lazima walime au wakulima hawana budi kulima. Kwa usahihi tunasema “Wakulima hawana budi kulima” (yako maneno yanayofanana kimuundo kama sina budi, hatuna budi, hawana budi , huna budi)
Baadaye/baadae: Neno sahihi ni baadaye

D
Digiti/Digitali: Digiti ni nomino na limetoholewa kutoka kwa neno ‘digit’ lenye maana ya tarakimu.  Neno hili ni nomino na ni sahihi. Digitali ni kisifa (adjective). Kwa kawaida tunatohoa nomino na wala siyo kisifa. Hivyo neno sahihi ni ‘digiti”.                         
Durusu/rudufu: Haya ni maneno yanayochanganywa na yana maana tofauti. Kudurusu ni kupitia tena maandishi  yaliyoandikwa kwa madhumuni ya  kusahihishwa au kuboreshwa  na kutoa toleo jipya. 
Rudufu ni kufanya nakala, kufanya kitu madhubuti k.v kurudufu nyuzi kuwa imara.
Darubuni: Ni chombo  cha kuonea mbali; kionea mbali yaani ‘Telescope/binoculars’.
Dahili/sajili: Maana ya kudahili ni kutaka kujua habari za watu kwa kuulizauliza au kudadisi. Kusajili ni kuweka orodha ya kmbukumbu za vitu au watu kwa kuviandika katika daftari maalumu.

F
Fedha/pesa/hela: Haya ni maneno yenye maana moja lakini yana asili tofauti. Maneno mengine yanayofanana na hayo ni sarafu, fulusi, faranga ambayo hutumika katika malipo. Maneno yote yanakubalika. Hata hivyo tuna mazoea ya kutumia neno fedha upande wa bara na pesa upande wa visiwani.
Fikiri /dhani: Maneno haya yanafanana kwa kiwango fulani lakini wengi wetu huyachanganya  na kuyatumia kama visawe. Yana tofautiana kidogo. Fikiri ni kutumia ubongo kutatua jambo, kutafakari, kuwaza. Kudhani ni kufikiri bila kuwa na uhakika.

G
Ghairi: Kuacha kutenda kilichokusudiwa.
Ghushi/gushi: Neno sahihi ni ghushi

H
Hadubini: Ni chombo  cha kuona vitu visivyoonekana kwa macho (Microscope).      
Hoteli/mahoteli: Neno sahihi ni  hoteli.
Hovyo/ovyo: Neno sahihi ni ovyo. Digiti ni nomino na limetoholewa kutoka kwa neno ‘digit’ lenye maana ya tarakimu.  Neno hili ni nomino na ni sahihi. Digitali ni kisifa (adjective). Kwa kawaida tunatohoa nomino na wala siyo kisifa. Hivyo neno sahihi ni ‘digiti”.                          
Hadhari/Tahadhari: Hadhari ni nomino na tahadhari ni kitenzi. Hadhari ni uangalifu. Hadhari kabla ya athari/hatari. Tahadhari ni kitenzi. Kuepuka jambo ili usipatikane na hatari au ubaya.
Hatima/ hatma: Neno sahihi ni hatima
Harusi/arusi: Maneno yote mawili yanatumika ila kwa mazoea ya wengi neno harusi ndilo linalotumika zaidi.

I
Idadi/nambari: Idadi ni jumla ya vitu au mambo yanayohesabika. Nambari limetokana na neno namba (number) yana maana ya tarakimu kama 1, 2, 3, 4, 5. Idadi ni namba au hesabu ya kujumuisha.Tunasema idadi kubwa ya Watanaznia ni wakulima.

J
Jingine/Lingine: Yote ni  sahihi ila hutegemea muktadha husika.
Jinsi na jinsia: Jinsi ni namna kitu kilivyo au kiumbe kama vile binadamu, wanyama au ndege. Tunayo jinsi ya kike na jinsi ya kiume. Kwa lugha ya kigeni ni ‘sex’.ku. Jinsia  ni hali ya kuwa mume au mke. Masuala yanayohusiana  na mwanamume na mwanamke. Kwa lugha ya kigeni ni ‘gender’.

K
Kuwapo /Kuwepo: Neno linalosadifu ni kuwapo ijapokuwa kwa mazoea watu wengi wanatumia kuwepo.
Kiwanda/Karakana: Kiwanda  ni mahali penye sehemu za kuundia vitu mbalimbali  kama milango, vioo, madirisha, magurudumu, n.k. Sehemu hizi hufahamika kama karakana. Hivyo kiwanda huwa ni mkusanyiko wa karakana mbalimbali.
Kampuni/Makampuni: Neno sahihi ni  kampuni na   wala siyo makampuni.
Kurudufu: Maana yake ni kunakili  au kutoa nakala nyingine.
Kimbiza /Wahisha: Kukimbiza ni kufuata kitu au mtu kwa mbio nyuma  au kufukuza. Kuwahisha ni kutenda jambo  mapema kabla halijaharibika. Waandishi wanatumia ‘kukimbiza badala ya kuwahisha.                               
Kuongea/kuzunguma: Tofauti kati ya maneno haya ni ndogo sana. Kuongea ni kushiriki katika mazungumzo. Kuzungumza ni kusema maneno katika mkutano au kwenye mjadala au baraza na kutoa maoni.
Kupeleka:  ni kuchukua kitu au mtu na kukifikisha/kumfikisha mahala fulani. Tukiongeza kiambishi cha –ea tunapata kupelekea kwa maana ya kufikisha kitu kwa niaba ya…Mtoto alimpelekea mzazi wake mbegu shambani. Hivi sasa matumizi ya pelekea yanaleta kichefuchefu kwa Waswahili.
Kuyeyuka/kuyayuka: Neno sahihi ni yeyuka kwa maana ya kugeuka kwa kitu kigumu kuwa kioevu.
Kunyauka/kukauka: Kunyauka ni kufifia kwa sababu ya ukame au joto. Kukauka ni kutoka maji na kuwa kavu
Kengeuka: Kwenda kombo, angamia. Kengeua ni kumfanya mtu afuate njia mbaya au tabia mbaya, kupotosha.
Kutokana/Kufuatia: Maneno haya mawili yanatumika kama vile yana maana moja. Kwa kweli yana maana tofauti kabisa. Kwa mfano tunasema,” Kutokana na njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 20,000 ya mahindi. Ni makosa kusema, “ Kufuatia njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 20,000 ya mahindi.
Kugharamia/kugharimia:
Neno sahihi ni kugharimia badala ya kugaramia. Gharama ni nomino.
Kwa ujumla/kwa jumla:
Maneno yote yanatumika kutegemeana na maudhui.Tunasema  kwa jumla maisha ni magumu. Hata hivyo neno linatumika kama: Kwa ujumla wake mvua imekithiri. Ni makosa kutumia, ‘Kwa ujumla tumefanikiwa…bali kwa jumla tumefanikiwa.’

CHANZO: MWANANCHI

No comments: