Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen
Wasira, amesema ipo haja kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa makini
kuteua mgombea wa urais mwenye maadili, mzalendo na atakayeendeleza
mazuri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete.
Kadhalika, amesema kabla ya kuteua mgombea wa urais kupeperusha
bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, ni vema
akafanyiwa tathmini kabla ya kuteuliwa. Alitaja vitu ambavyo anatakiwa atathminiwe kuwa ni uwezo wa kuongoza, uadilifu na anayeweka mbele maslahi ya Watanzania.
Alisema hivi sasa uzalendo umeshuka kidogo, hivyo rais ajaye anatakiwa aje na ajenda itakazoweka uzalendo mbele.
Wasira alisema Rais Kikwete anastahili kupongezwa kwa mambo makubwa
ya maendeleo ambayo ameyafanya katika kipindi chake cha miaka 10 pamoja
na kuwapo kwa baadhi ya changamoto chache zilizobaki.
Akizungumza na NIPASHE katika mahojiano, Wasira alisema kati ya
mambo ambayo Rais Kikwete atakumbukwa ni miradi mingi ya barabara ambayo
ameitekeleza, elimu na sekta ya kilimo. “Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, Rais Kikwete katika
kipindi chake amefanya mambo mengi mazuri, hastahili kubezwa hata
kidogo, najua wabaya hawawezi kukosekana, lakini anahitaji kupongezwa
kwa haya aliyoyafanya,” alisema Wasira na kuongeza:
“Kila kiongozi anapoingia madarakani huwa na vipaumbele vyake,
hakuna mtu atakayekuja kubadilisha Tanzania kuwa Sayuni, isipokuwa mtu
anafanya maendeleo kulingana na uwezo wake, ni vema atakayechaguliwa
aje na ajenda zake, lakini pia aendeleze mazuri na kuvipa kipaumbele
vitu ambavyo Rais Kikwete ameviacha, na kuwapeleka Watanzania mbele sio
kuwarudisha nyuma.”
Wasira alisema bado zipo changamoto chache ambazo zitahitaji Rais
ajaye azifanyie kazi ikiwamo suala la ajira kwa vijana pamoja na
umaskini.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment