Social Icons

Pages

Thursday, May 28, 2015

KESI ZA MADAI KATIKA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI


Mahakama ya Hakimu Mkazi imeanzishwa chini ya kifungu cha nne cha Sheria ya Mahakama Sura ya 11 kama ilivyorejewa mwaka 2002.
Mahakama hii husikiliza mashauri ya madai yaliyomo ndani ya mkoa au eneo ambalo itakuwa imepangiwa kisheria ambalo ni zaidi ya eneo la mkoa au wilaya moja tofauti na Mahakama ya Wilaya inayoishia kwenye wilaya husika.
Mamlaka ya kifedha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ni sawa na yale ya mahakama ya wilaya na kwa madai ya mali zisizohamishika yanaishia Sh150 milioni na kwa mali inayohamishika ni Sh100 milioni.
Katika mamlaka ya usimamizi na marejeo, hakimu mkazi mfawidhi ana mamlaka ya kuita jalada na kutathmini mwenendo wa kesi za Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya au ya Mwanzo, na kutolea uamuzi na kupeleka ripoti Mahakama Kuu.
Rufaa zote zinazotoka Mahakama ya Mwanzo zinapaswa kupelekwa Mahakama ya Wilaya na si Mahakama ya Hakimu Mkazi. Rufaa kutoka Mahakama ya Wilaya haziendi Mahakama ya Hakimu Mkazi, bali inapaswa kupelekwa katika Mahakama Kuu.
Hii ni kwa sababu Mamlaka ya Mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi yanawiana japokuwa mahakama ya Hakimu Mkazi inaizidi kwa baadhi ya mambo.
Jambo lingine Muhimu ni kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 45 cha Sheria ya Mahakama Sura ya 11 kama ilivyorejewa mwaka 2002, Waziri wa Sheria, kwa kushauriana na Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu anaweza kumuongezea mamlaka hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ili aweze kusikiliza kesi ambazo zinapaswa kusilikilizwa na Mahakama Kuu.
Kwa kuzingatia mamlaka hayo yalioongezwa kisheria, Hakimu Mkazi atakuwa na uwezo wa kusikiliza kesi maalumu alizopewa mamlaka kuzisikiliza au kesi zozote ambazo atawajibika kuzisikiliza kwa kuzingatia mamlaka hayo. Taratibu zote za nyaraka na uendeshaji wa kesi zitakuwa ni zilezile za Mahakama ya Hakimu Mkazi lakini mamlaka ndiyo yatakayokuwa ya Mahakama Kuu katika kutoa uamuzi wa kesi mbalimbali.
Wakili anaruhusiwa kusimamia kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi.
Bado linabaki kuwa ni jukumu la mdai kuwasilisha madai yake ya kesi mahakamani kupitia hati ya madai na kuhakikisha ameandaa ushahidi wa kutosha kupitia mashahidi na vielelezo sahihi ili kuthibitisha ukweli na uzito wa madai yake.
Katika mchakato wa mwenendo wa kesi mahakama hutoa nafasi ya wahusika wa kesi kujadiliana na kupatana. Ni muhimu kumaliza kesi katika hatua hii ya mapatano kwa njia ya amani na maridhiano ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza wa muda na gharama katika kuendesha kesi.
Mdai kumbuka ubishi hausaidii. Busara ikitumika hakuna lisilowezekana. Usikatae fedha. Siku zote fedha hushuka thamani.
Pesa utakayolipwa leo si sawa na utakayolipwa miaka miwili ijayo. Mdaiwa pia unapaswa kutumia busara, patana na mdai, lipa madeni unayodaiwa kuepuka usumbufu wa gharama nyingi sana utakazodaiwa kesi itakapokwisha.
Endapo mahakama itawapa fursa ya kupatana na mkashindwa kufanya hivyo, taratibu za kawaida za kesi kusikilizwa zitaendelea na baadaye mahakama kutoa hukumu. Endapo hutaridhika na uamuzi huo, unayo haki ya kukata rufaa Mahakama Kuu ndani ya siku 30 hadi 60 kuanzia tarehe uliyopata nakala ya hukumu.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: