Social Icons

Pages

Thursday, May 28, 2015

TANZANIA ITAKAVYOFAIDI SOKO LA VITO VYA THAMANI

Tanzania imebahatika kuwa na aina nyingi ya madini ya vito vya thamani kama vile dhahabu, almasi na Tanzanite.
Wingi wa rasilimali hizo za thamani duniani umekuwa ukiwafanya baadhi ya watu kuamini kuwa nchi ni tajiri lakini unapoingia kwenye uhalisia, utajiri huo haulisukumi taifa kumea vizuri kiuchumi.
Je, tatizo ni nini? Kuna mipango gani ya kukabiliana na hali hiyo? Haya ni maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa na wengi na makala hii inakusudia kuyajibu.
Arusha na moja ya mikoa nchini ambao kuna uchimbaji wa aina nyingi za madini. Moja ya madini yanayoupa sifa kubwa mkoa huu ni madini ya Tanzanite ambayo hayapatikani eneo jingine popote duniani.
Biashara kubwa ya madini hayo ipo katika Jiji la Arusha na kuna mitaa, ambayo ni kawaida kukuta vijana, wakiwa wamekaa kando ya barabara wakichonga madini na kuuza. Mitaa hiyo ipo katikati ya Jiji la Arusha kama vile Barabara ya Pangani, jengo la Chama cha Wafanyakazi Arusha (Ottu) na Mtaa wa St Thomas.
Katika mitaa hii, utakuta vijana wengi wakiwa na viti na meza ndogo wakichonga madini na wengine wakiuza. Mbali na Tanzanite, pia kuna aina nyingine madini kama vile saphire, spinel, tourmaline, sperssatite na aquamarine. Miongoni mwa madini hayo yapo yanayochimbwa mikoa ya jirani.
Kuuzwa holela kwa madini kunatajwa ndiyo kunasababisha madini mengi kutoroshwa na kuvuka mipaka kuingia nchi mbalimbali ambazo huziuza kwenye soko la dunia. Aina hii ya biashara hulikosesha taifa mapato na isitoshe hata wachimbaji na wafanyabiashara hiyo hapa nchini hupata faida kidogo tofauti na ingekuwa wangepeleka wenyewe kwenye soko la dunia.
Kwa mfano ripoti ya mwaka 2013 inaonyesha kuwa uuzaji wa madini ya Tanzanite uliingizia Tanzania Dola 38 tu za Marekani huku nchi zinazopata madini hayo kwa njia ya panya, zikijipatia mapato makubwa. Kulingana na ripoti hiyo, katika mwaka huo, Tanzanite iliingizia Kenya Dola 100 milioni na India Dola 300 milioni.

Tanzania yazinduka
Kwa kutambua namna inavyopoteza mapato na nchi kutofaidika kikamilifu na madini yake, Serikali imeamua kuweka mkakati ambao utaziba mianya ya utoroshaji wa madini nchini. Ili kuifanya biashara ya madini ya vito, kutambulika kisheria na kuinufaisha Serikali katika kukusanya kodi mipango imeanza kujengwa kituo cha kukata, kusanifu na kuuza madini Arusha.
Kituo hiki, kinakuwa cha kimataifa, ambacho kitakusanya wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite wa ndani na nje ya nchi kukaa pamoja kufanya biashara halali.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene anasema kituo hiki, kitajengwa na Serikali kwa kushirikiana na Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). “Katika kituo hiki, kutakuwa na maduka ya kununua na kuuza madini, ofisi za mamlaka ya kodi (TRA), ofisi za madini na eneo la kukata na kusanifu madini,” anasema.
Lengo la Serikali kuja na mpango huo, ni kuhakikisha madini yanayopatikana nchini, yanalinufaisha Taifa pia kunakuwapo masoko ya uhakika. “Hatutaki biashara ya utoroshaji wa madini pia kuuzwa nje yakiwa ghafi,” anasema.
Wakati Serikali ikiweka mikakati hiyo, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) nao unaweka udhibiti kwenye viwanja vya ndege kuhakikisha hakuna madini yanayotoroshwa nje ya nchi kimagendo.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta anasema: “Kwa kipindi cha kuanzia Januari mpaka Desemba mwaka jana, wakala umeweza kukamata watoroshaji wa madini ya aina mbalimbali katika matukio 27 tofauti.”
Kamishna wa madini nchini, Paul Masanja anasema mipango ya Serikali na wadau kwa sasa ni kuhakikisha Tanzania hasa Arusha inakuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito barani Afrika.
“Madini ya vito tuliyonayo nchini, hayapatikani katika mataifa mengi Afrika hivyo tunataka kulifanya Jiji la Arusha kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito barani Afrika,” anasema.
Anasema kituo cha kisasa cha kukata na kuuza madini, kikikamilika wafanyabiashara wakubwa duniani wa madini ya vito watakuja nchini kununua madini.
Hata hivyo, anatoa wito kwa wachimbaji na wanunuzi wa madini ya Tanzanite nchini, kuacha tabia ya utoroshaji wa madini hayo nje na kuuza madini hayo yakiwa ghafi.

Wadau wanasemaje?
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wa madini Mkoa wa Manyara, Sadiki Mnenei, Wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One, Faisal Juma Shabhai na Hussein Gonga na Ofisa wa Kampuni ya Kuuza Madini ya Crown Lapidary Limited, Lucas Mdemu wanasema kituo hicho kikijengwa ni faraja na mkombozi kwa wachimbaji na wafanyabiashara hiyo.
Mnenei anasema kwa miaka mingi wachimbaji wadogo wa madini ya vito wamekuwa hawana masoko ya ndani ya uhakika ili wauze madini yao. “Wachimbaji wamekuwa wakipeleka madini yao nchi Ulaya, Marekani, India na Kenya na baadhi yao wamekuwa wakitapeliwa na wanunuzi sasa kituo cha kimataifa kikiwa Arusha ni ukombozi kwao na hawatakuwa na sababu ya kupeleka madini nje ya nchi kwani wanunuzi watakuja Arusha,” anasema.
Shabhai anasema kituo kitawafanya wafanyabiashara ya madini nchini kumiliki biashara hiyo kimataifa. Mdemu anasema, biashara ya Tanzanite itakuwa bora kama, wanunuzi wa madini hayo watanunua sehemu ambazo zinatambulika kisheria. Serikali kuja na mpango wa kujenga kituo hiki ni ukombozi wa wafanyabiashara, wataokoa mapato yanayopotea na nchi itafaidika na rasilimali zake.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: