Social Icons

Pages

Tuesday, June 02, 2015

SHULE ZA MSINGI ZA BWENI NA ATHARI ZA KIMALEZI

Wanafunzi wakishiriki usafi wa mazingira shuleni. Baadhi ya wazazi wanasema shule za bweni si mwafaka kwa wanafunzi wadogo kiumri.
Hivi karibuni, serikali ya Rwanda imepiga marufuku shule za bweni kwa wanafunzi wa elimu ya msingi. Wizara ya Elimu ya nchi hiyo, imetoa muda wa miaka mitatu kwa shule za msingi za bweni kufunga huduma hiyo. Lengo la Serikali ya Rwanda ni kutaka kuona watoto wakipata muda zaidi wa kukaa na wazazi wao, kuwafinyanga kimalezi mpaka wafikie umri wa kujitambua zaidi.
Hivyo kwa serikali ya Rwanda muda mwafaka wa wanafunzi kwenda  shule za bweni ni  pale wanapofika sekondari.
Upepo wa shule za bweni kwa wanafunzi wenye umri mdogo umeikumba pia Tanzania. Hivi sasa kuna idadi kubwa ya shule zinazopokea wanafunzi chini ya miaka 10 wanaosoma elimu ya msingi. Je, ni mwafaka kwa Serikali ya Tanzania kufuata nyayo za Rwanda kuzuia shule hizo?

Utengano na wazazi
Hapa nchini, wanafunzi wanatumia miezi si chini ya tisa wakiwa shuleni, muda ambao   Meneja wa utafiti na uchambuzi wa sera wa shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventure anasema hauwapi watoto nafasi ya malezi kutoka kwa wazazi
“Miezi tisa ni mingi kwa  mtoto kuwa mbali na malezi ya wazazi, kwa hivyo nakubaliana na mabadiliko ya Rwanda; ingetokea  hapa nchini ingesaidia  japokuwa ninaamini haiwezekani kutokana na changamoto ya umbali wa shule nyingi  zilivyojengwa  ambazo  zinalazimisha kuwa na bweni japo si vizuri kimalezi,’’ anasema na kuongeza:
“Kiuzoefu, watoto wengi  wanaosoma shule za bweni huathirika kimalezi; wanabadilika tabia bila mzazi kujua lakini kama mwanafunzi anakwenda shule na kurudi, ni rahisi kwa mzazi  kutambua mabadiliko na mwenendo wake.”
Anasema hata Korea Kusini ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea, lakini hayatumii mfumo wa shule za bweni ila kwa wanafunzi maalumu, kama anavyofafanua:
“Korea Kusini wanatumia shule za bweni kulea vipaji na si kwa masomo ya sekondari au shule ya msingi, vipaji ndiyo vinalelewa, kukuzwa ili kulinda visipotee.’’
Katibu Mkuu wa Umoja wa wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini (Tamongsco), Benjamin Nkonya, anasema uamuzi wa kufungia shule za bweni  kwa daraja la elimu ya msingi ni sahihi.
“Kuanzia kidato cha kwanza mpaka vyuoni inawezekana kukaa bweni na kwa Tanzania tunaweza kufanya hivyo, lakini lazima kuwapo na huduma nzuri za usafiri wa mabasi ya wanafunzi kwa wanafunzi wa shule za kwenda na kurudi nyumbani,’’anasema.
Hata hivyo, Nkonya ambaye pia ni mmiliki wa Shule ya Sekondari  ya King Solomon, anasema uzoefu unaionyesha uendeshaji wa shule za bweni una nafuu kuliko shule za kutwa
Evelyin Mchau amewahi kusoma katika shule ya bweni, anaunga mkono kufutwa kwa shule za bweni hasa kwa watoto wa elimu ya awali na msingi.
“Kuanzia chekechea na shule ya msingi wanatakiwa kusoma shule za kawaida ili kuwa karibu na wazazi,  lakini sekondari kwa mfano, mimi shule ya bweni imenisaidia  kimalezi. Nilikabidhiwa kwa mwalimu wa malezi ambaye alinifuatilia mwenendo wangu,” anasema.

Shule za bweni na maadili
Mzazi wa jijini Dar es Salam, Maria Mashasi anasema ameamua  kusomesha watoto wake wawili katika shule za kutwa baada ya kugundua kuwa shule za bweni hazina faida kimaadili.
“Mtoto wangu mkubwa anasoma darasa la pili, mwingine  chekechea, wote wanasoma ABC Capital School iliyopo Kinyerezi. Sikuona umuhimu kwani nimeshuhudia watoto wa rafiki yangu waliosoma bweni lakini wameathiriwa na utandawazi. Alitumia gharama kubwa kuwasomesha lakini waliambulia mimba na  uvutaji dawa za kulevya,” anasema na kuongeza:
“Kinachosababisha wazazi kupeleka watoto bweni ni hali ya kubanwa na majukumu bila kuona umuhimu wa malezi yao kwa watoto, kazi haiwezi kuwa bora zaidi ya malezi kwa mtoto,Tanzania tunatakiwa kufuata Rwanda.”

Hoja kinzani
Mwalimu wa shule ya bweni ya Barbro Johansson, iliyopo Mbezi jijini Dar es Salaam, Doroster Mandes,  anasema  uamuzi wa Rwanda ni sahihi lakini inategemea na mazingira ya shule zake. Kwake tathmini ya Rwanda inaweza kutofautiana na Tanzania.
“Kuna mwanafunzi anaharibika hata akiwa shule za kawaida, unakuta mzazi anatingwa na hajui mwenendo wake shuleni. Hilo pia ni tatizo kwa hivyo kufungia bweni siyo suluhisho kwani kuna shule zinazotumia misingi mizuri ya malezi,” anaeleza mwalimu Doroster.

Haja ya shule za bweni
Kwa baadhi ya watu, shule za bweni kwa watoto zina manufaa kadhaa kama vile kuwaepusha watoto na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule.
“Wazazi wengi wanalazimika kuwapeleka bweni hata chekechea, shule za msingi kutokana na mateso yaliyopo, yaani mwanafunzi anaathirika kisaikolojia kabla ya kufika shuleni. Anaamshwa asubuhi na mzazi, anafika kituoni konda hamtaki, akifika amechelewa anakutana na bakora za mwalimu, kwa mazingira hayo matokeo yake lazima afeli mtihani,” anasema Nkonya.
Aidha, wapo wazazi wanaoamini kuwa shuleni ni mahala mwafaka kwa watoto kuzingatia masomo kuliko nyumbani. Hivyo kuepukana na ushawishi wanapendelea kuwapeleka watoto shule za bweni wakiwamo wale wenye umri mdogo wa hata chini ya miaka saba.

Kauli ya Serikali ya Tanzania
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela anasema Tanzania haiwezi kufuata mtazamo au uamuzi wa Rwanda kufuta shule zinazotoa huduma ya malazi kwa wanafunzi.
“Rwanda ina sababu zake na sisi tumeshaangalia hilo tukakubaliana nalo. Kila nchi ina changamoto zake kwa hivyo nadhani hata sisi tuko sawa kwa upande wetu.”

CHANZO: MWANANCHI

No comments: