Waziri wa kilimo, Chakula na Ushirika Steven Wasira.
Kutokana na matatizo mengi katika kilimo cha pamba
ikiwamo kutotabirika kwa bei, baadhi ya wakulima wa zao hilo Wilaya ya
Bariadi mkoani Simiyu wameonyesha mwelekeo wa kutaka kuhamia kilimo cha
mazao ya alizeti na choroko.
Uamuzi huo unafikiwa na wakulima hao kutokana na bei iliyopangwa
kwa ajili ya kununulia zao hilo kuwa ndogo ukilinganisha na gharama
wanayotumia kufanyia maandalizi hadi kuvuna. Wakizungumza na NIPASHE juzi, baadhi ya wakulima wa vijiji vya
Gambosi na Nyamswa wilayani humo, walisema hakuna matumaini ya bei nzuri
ya pamba kutokana na kukatishwa tamaa.
“Tatizo ni bei ya pamba sisi wakulima tunapewa bei ndogo sana ndiyo
maana tunaona tuhamie mazao mengine ya kibiashara kutokana na kutumia
gharama kubwa lakini tunapouza tunapewa bei ndogo, hivyo kupoteza muda
na kupata hasara na suala hili ndilo litakaloua zao hili,” alisema
Masule Sigola, mkazi wa kijiji cha Gambosi.
Naye Katibu Mkuu Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (Tacoga),
George Mapanduji, alisema ushindani wa ununuzi kwa wakulima na mawakala
kutaka kuwa na kilo nyingi za pamba, umechangia kutozingatiwa kwa
madaraja ya pamba, hivyo kushusha ubora wa zao hilo la kimataifa na kuwa
ya chini.
Alisema zamani mkulima alikuwa akichambua pamba yake na
kuitenganisha safi na mafifi, kila moja inakuwa na bei yake, lakini kwa
sasa hali hiyo haipo tena isipokuwa inatangazwa bei moja tu hivyo
kushusha ubora wa pamba katika soko la kimataifa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment