Social Icons

Pages

Thursday, April 02, 2015

KURA YA MAONI KATIBA YAWASHA MOTO BUNGENI

Wabunge wa Kambi ya Upinzani wakijadiliana baada ya Bunge kuahirishwa ghafla na Spika mjini Dodoma jana kufuatia mabishano makali juu ya hatma ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.Vurugu zimeibuka bungeni na kusababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kulazimika kuahirisha Bunge kwa muda baada ya wabunge wa upinzani kuibana serikali kuitaka itoe majibu kama kazi ya uandikishaji wapiga kura itakamilika na kuruhusu kufanyika kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa Aprili 30, mwaka huu. Vurugu hizo ziliibuka baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuomba mwongozo wa Spika akitaka Bunge lisitishe shughuli zake na kujadili jambo la dharura kuhusiana na kazi ya uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura ambalo halijakamilika hadi sasa.
Katika mwongozo wake, Mnyika alisema mpaka sasa kazi ya uandikishaji haijakamilika hata kwa Mkoa wa Njombe na Watanzania nchi nzima wapo katika hali ya utata kuhusu lini wataandikishwa kabla ya kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa. “Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Bunge uliopita uliagiza serikali ishughulikie suala la uandikishaji wapiga kura na majibu yatolewe katika mkutano huu wa Bunge la 19, lakini sasa leo mkutano unakwenda kufungwa bila majibu kutolewa, hivyo tusitishe shughuli za Bunge ili tujadili suala hili ambalo ni la dharura,” alisema.
Mnyika alisema katika mkutano wa 19 wa Bunge, ameomba miongozo minne kuhusu suala la uandikishaji wapiga kura, lakini serikali kupitia Waziri Mkuu inakwepa kutoa majibu, hivyo hakuna haja ya kuendelea na kikao hadi majibu yapatikane. Vurugu ambazo ziliambatana na kupiga kelele mfululizo ziliongezeka, baada ya Spika Makinda kujibu mwongozo huo kwamba mwongozo wa Mnyika unafanana na ule aliotangulia kuuomba Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo.
Majibu hayo ya Spika Makinda yaliwatibua wabunge wa upinzani ambao kwa pamoja walisimama mfululizo na kila mmoja kuzungumza kivyake na Spika kumweleza Katibu wa Bunge aendelee kusoma Muswada wa Sheria ya Habari wa mwaka 2014. Hata hivyo, Katibu wa Bunge alishindwa kuendelea kusoma kutokana na kelele zilizokuwa zikipigwa na wabunge wa upinzani ambao walikuwa wakisema kuwa wamechoka kuburuzwa. Kutokana vurugu hizo, Spika alijibu mwongozo wa Mnyika kwamba kwa kuwa jana ilikuwa siku ya kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu atalitolea majibu suala hilo.
Majibu hayo hayakukubaliwa na wabunge wa upinzani na ndipo Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali; Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema; Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee; Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, walisema na kuomba taarifa, lakini Spika Makinda aliwakatalia.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Machali, alisikika akisema wabunge wa upinzani wamechoka kuburuzwa na kumshutumu Spika Makinda kwamba analiharibu Bunge kutokana na kuitetea serikali isitoe majibu katika jambo muhimu kama hilo. Kufuatia vurugu kuendelea na Bunge kukosa hali ya utulivu, Spika Makinda alichukua uamuzi wa kusitisha shughuli za Bunge hadi jana jioni hali iliyozua maswali mengi kwa wabunge wa CCM.
Awali, Jafo katika mwongozo wake ambao Spika alisema unafanana na wa Mnyika, aliomba kura ya maoni isigozwe mbele badala yake Bunge lipishe katiba ya mpito. Jafo alisema Taifa lipo katika kipindi muhimu cha uandikishaji wananchi katika daftari la wapiga kura na taarifa zilizopo ni kwamba wananchi wamejitokeza wengi kutaka kuandikishwa katika daftari hilo na kumekuwa na changamoto ya upungufu wa vitendea kazi, hali itakayosababisha lisikamilike kwa wakati.
Alisema kutokana na hali hiyo itakuwa vigumu kukamilika kwa uandikishaji kabla ya Aprili 30, mwaka huu ili kuwezesha wananchi kupiga kura ya maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa. “Kura ya maoni itatanguliwa na utoaji wa elimu, hivyo napendekeza katika kikao cha Mkutano wa 20 wa Bunge lijalo kwa sababu sisi tuna dhamana ya Watanzania na uandikishaji unaoendelea, hivyo tutumie mkutano wa 20 serikali ilete muswada wa dharura kupitisha Katiba ya mpito,” alisema.
Kwa mujibu wa Jafo, Katiba ya mpito itakuwa na mambo manne ya muhimu ambayo ni kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, matokeo ya Rais kupingwa mahakamani na mgombea binafsi kuruhusiwa. Alisema kwa kuwa Taifa linapitia katika hali tata kama mambo hayo yatapitishwa, Katiba ya mpito itafanya kazi kwa miezi sita au 12 baadaye wananchi watapiga kura ya maoni baada ya kupata elimu ya kutosha kuliko kuingilia katika kura ya   maoni   kwa   ajili   ya  Katiba   mpya.  Baada ya Jafo kuzungumza hayo, wabunge walimpinga  huku wakiendelea kupiga kelele, hali iliyomlazimu kuwaambia wabunge waliokuwa wakipiga kelele waendelee.
 
GODBLESS LEMA
Akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Arusha, Lema, alisema wanapinga kitendo cha Spika kuilinda serikali isitoe majibu mambo ya msingi hali ambayo inatia shaka. Lema alisema katika uchunguzi wao wamebaini kuwa serikali inataka kutumia mbinu kusogeza uchaguzi mkuu na ndiyo maana haitaki kutoa majibu kuhusu uandikishaji wapiga kura itakamilika lini.

SAID ARFI
Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi, alisema vurugu zinazotokea bungeni ni kwa sababu ya wabunge wanavutwa mno na hisia za kisiasa. Arfi alisema kura ya maoni ipo kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni ambayo kimsingi haimpi mamlaka Rais ya kutangaza tarehe ya kuanza kwa kura ya maoni bali jukumu hilo linatakiwa kufanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) baada ya kuandika swali na kulichapisha kwenye Gazeti la Serikali. “Tumeacha kusimamia sheria, tunavutwa na hisia za kisiasa kwa hali hii tunaharibu Bunge,” alisema.

ISMAIL RAGE
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, alisema hoja aliyoitoa Jafo haina tofauti, hivyo hakukuwa na sababu Mnyika naye kutoa kuomba mwongozo kama huo.

JAMES MBATIA
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, alisema mwaka jana walikutana na Rais Jakaya Kikwete na kukubaliana kura ya maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa ifanyike mwakani, lakini inashangaza hali ilivyo sasa. Alisema kwa jinsi uandikishaji unavyokwenda, kura ya maoni haiwezi kufanyika, lakini serikali haitaki kukubali na kutoa matumaini ambayo hayawezi kutekelezwa, jambo ambalo alisema ni hatari.

JAMES LEMBELI
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, alisema serikali inataka kuwafanya Watanzania kama watoto wadogo kwani ni jambo lililo wazi kwamba kura ya maoni haiwezi kufanyika kutokana na muda uliobaki. Alisema serikali na Nec wanachanganya wananchi katika suala la kura ya maoni kutokana na kutoa kauli zinazotofautiana.

KHAMIS KIGWANGALLA
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Kigwangalla, alisema suala la kura ya maoni ni changamoto kubwa kwani lisipofanyika kipindi hiki itabidi hadi mwakani. Hata hivyo, alisema kama haitafanyika sasa kuna uwezekano wa mambo ya msingi kama Tume huru ya Uchaguzi na mgombea binafsi kutukuwapo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Alisema kimsingi kwa muda uliobaki kura ya maoni haiwezi kufanyika.

SAID NKUMBA
Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba, alisema kwa kuwa Nec ndiyo iliyopewa kazi ya kuandikisha wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura na haijasema kama itashindwa kufikia muda wa kura ya maoni, hivyo suala hilo iachiwe tume hiyo. “Mwenyekiti wa Nec alishasema kama kazi ya kuandikisha wapiga kura itashindwa kukamilika, itatoa taarifa kwamba kura ya maoni haitafanyika, hivyo kwa kuwa hadi sasa haijasema lolote hivyo iachiwe,” alisema.

ABDUL MAROMBWA
Mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Marombwa, alisema bado kuna matumaini kura ya maoni itafanyika kwa kuwa Nec haijatoa taarifa kama imekwama kuandikisha wananchi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: