Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa
Serikali za mitaa nchi nzima yanayoonyesha kuimarika kwa upinzani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Khalist Luanda alisema jana kwamba wakati CCM ikifanikiwa
kupata ushindi wa jumla mitaa na vijiji 9,406, kwa pamoja vyama vingine
vya upinzani, vimegawana nafasi 3,211. Kwa ushindi huo upinzani umeongeza viti 1,981
ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita mwaka 2009
ambao kwa ujumla, ulipata nafasi 1,230 za wenyeviti wa mitaa na vijiji. Kwa upande wake, CCM imepoteza nafasi 2,636 za
uenyekiti wa vijiji na mitaa ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2009
ilipopata jumla ya viti 12,042.
Hata hivyo, uchaguzi mwa mwaka huu, umefanyika
huku kukiwa na nyongeza ya mikoa, wilaya, mitaa na vijiji katika baadhi
ya maeneo nchini. Luanda alisema CCM kimepata vijiji 7,290
kikifuatiwa na Chadema yenye vijiji 1,248. CUF imeshika nafasi ya tatu
kwa kuwa na vijiji 946, ikifuatiwa na UDP yenye vinne na TLP na NLD
vyenye viwili kila kimoja. Katika nafasi za wenyeviti wa mtaa, CCM kimechukua
jumla ya mitaa 2,116. Vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni
Chadema (753), CUF (235), ACT (9), NCCR - Mageuzi (8) wakati vyama vya
TLP, UMD, UDP na NRA vimepata mtaa mmoja kila kimoja.
Matokeo hayo yamejumuisha maeneo mengi ambayo CCM ilipita bila ya kupingwa. Katika matokeo hayo, CCM imeendelea kufanya vizuri
katika mikoa ambayo imekuwa ikitajwa kuwa ni ngome yake lakini kuna
maeneo ambayo yalionekana kuyumba kwa kuzolewa na upinzani. Mfano wa ngome ambazo CCM kimetikiswa zaidi ni
Mkoa wa Dodoma katika wilaya za Kondoa na Chemba ambako vyama vya CUF na
Chadema vimefanya vizuri tofauti na uchaguzi uliopita. Kuhusu nafasi ya mwenyekiti ambaye alisimikwa na
wananchi kibabe katika Mkoa wa Arusha, Luanda alisema Tamisemi
haitamtambua, bali atakuwa ni mwenyekiti wa kimila tu.
No comments:
Post a Comment