Social Icons

Pages

Monday, December 07, 2015

MUHAS YATOA WAHITIMU FANI YA AFYA YA MAZINGIRA NA KAZI

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Prof. Ephata Kaaya. Kwa mara ya kwanza nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi  Muhimbili (Muhas), kimetoa wahitimu wa shahada ya uzamili katika fani ya afya ya mazingira na kazi.
Hayo yalisemwa juzi jijini Dar es Salaam kwenye sherehe ya mahafali ya tisa na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Ephata Kaaya, wakati wa kutunuku shahada za uzamivu, shahada za uzamili, shahada za kwanza, stashahada za juu na stashahada mbalimbali kwa wahitimu 878 waliomaliza masomo yao mwaka huu.
Alisema shahada hiyo inawaandaa wahitimu kuwa na ujuzi na maarifa ya kutosha kukabiliana na changamoto nyingi katika kuhifadhi afya za viumbe hai, hususan katika mazingira ya kuishi na kufanyia kazi yanayoweza kusababishwa na kemikali, hewa, maji,  vyakula na udongo.
“Wahitimu hawa watakuwa na uwezo wa kutambua, kutathmini, kudhibiti hatari za afya katika mazingira ya kuishi na kufanyia kazi,” alisema. Alisema maeneo ambayo yatanufaika kwa kuwatumia wataalam hao ni pamoja na vyuo vya elimu ya juu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, serikali za mitaa, mamlaka ya afya na usalama kazini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, shughuli za migodi mikubwa, na viwanda vikubwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Deogratius Ntukamazina, aliiomba serikali iendelee kukifadhili chuo hicho na kupanua miundombinu yake hususani kumalizia ujenzi wa Kampasi Kuu ya Mlongazila ili kufanikisha majukumu ya chuo kwa ufanisi.
“Kampasi hii itakapomalizika chuo kitaweza kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 3,500 waliopo sasa hadi zaidi ya 15,000 na hivyo kuongeza rasilimali watu kwenye sekta ya afya katika ngazi zote,” aliongeza kusema.

CHANZO: NIPASHE

No comments: