Jumla ya Sh. 675,436,159 zimetumika kwa ajili ya
kuzilipa kaya 17,162 zilizopo wilayani Sengerema katika mkoa wa Mwanza
kwa ajili ya kuzikwamua kuondokana na wimbi la umaskini.
Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wilayani humu,
Rehema Simeon, akizungumza wakati wa kuzikabidhi kaya maskini za vijiji
tisa wilayani humu, alisema lengo la mfuko huo ni kuwaondolea umaskini
wananchi hao.
“Tuna vijiji 106 kati ya 153 ambavyo wananchi wake wapo katika
malengo ya kuondolewa umaskini na Tasaf, leo tunamalizia kaya za vijiji
tisa kwa awamu ya tatu baada ya kuanza Julai, mwaka huu na kukamilika
Desemba, mwaka huu,” alisema Simeon.
Alivitaja vijiji ambavyo baadhi ya kaya zilikabidhiwa pesa kwa
ajili ya kujikwamua na umaskini ni Mnadani, Mtakuja, Kizugwangoma,
Kanyamwanza, Butonga road, Sima, Isungang’holo, Ishinshangholo na
Ilyamchele.
Alisema walengwa waliondolewa umaskini kwa kupatiwa fedha za mtaji
wamekuwa wakipatiwa kati ya Sh. 20,000 hadi 78,000 kwa kila kaya
hususani zikiwalenga akinamama ambao ni wasimamizi wakuu wa familia.
Hata hivyo, alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni pale
wanapokuta kaya imehama ama kufariki dunia na wenyeviti kudai kutaka
kuachiwa fedha hizo kwa makusudi ya kuzipatia familia ya kaya husika.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Sengerema, Vincent
Bushaija, aliwataka walengwa wa kaya zilizopata fedha hizo, kujiwekea
malengo ya kuzitumia na kupata mabadiliko ya kimaisha.
“Tunataka tuone watoto wanaenda shule wakiwa na sare na madaftari,
akinamama waende kliniki kupeleka watoto wao na familia katika kaya
kupata milo mitatu kwa siku badala ya miwili,” alisema Bushaija.
Bushaija alisema kutolewa kwa fedha hizo ni mpango wa serikali
kuboresha afya, watoto wapelekwe kliniki pamoja na shule wakiwa nadhifu
kwa kuvaa sare za shule.
Stephania Msabaha, ambaye ni mlengwa wa mfuko huo, alisema mpango
huo wa Tasaf kuwaondolea umaskini ni mzuri, hivyo kiasi alichopata
kitamsaidia kuendesha shughuli za ufugaji wa kuku wa kienyeji na kutunza
wajukuu zake watatu.
Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri na Tasaf, Theopasta Nyabange,
alisema amekuwa wakifuatilia na kukagua iwapo kama mlengwa amelipwa
kinachostahili ama la.
Nyabange alitoa wito kwa kuwataka wasimamizi walipe kwa utaratibu uliopo ili kuepukana kuingia katika matatizo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment