Aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Ubungo kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas Massaburi, amefungua kesi ya
kupinga ushindi wa Saed Kubenea, kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema).
Dk. Massaburi amefungua kesi hiyo ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Mbali ya Kubenea, wengine waliounganishwa katika kesi hiyo ni
Masimamizi wa Uchaguzi katika jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali.
Katika kesi hiyo, Dk. Massaburi anadai kwamba mshtakiwa wa kwanza
(Kubenea), alitoa rushwa ya kununua jenereta katika hospitali ya
Mavurunza iliyopo kata ya Kimara, kutoa rushwa ya ujenzi wa barabara ya
Matete, kutoa zawadi kwa kununulia ‘Pool Table’, kwa ajili ya
kuwashawishi wananchi wampigie kura.
Madai dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo ni hakumpatia
nafasi ya kuhesabu kura upya kama alivyoomba, hakumjulisha tarehe, muda
na wapi matokeo ya jimbo hilo yalikuwa yanajumulishwa, yeye na mawakala
wake hawakuona wakati vifaa vya uchaguzi vinafunguliwa.
Pia anadai kwamba baadhi ya vituo havikufanya uchaguzi, na pia
baadhi ya wapigakura walipiga kura wakati hawajafikisha umri wa kupiga
kura.
Katika madai hayo, Dk. Massaburi anaiomba Mahakama Kuu itengue ushindi wa Kubenea uliotangazwa na Msimamzi wa Jimbo hilo.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Kubenea
alithibitisha kupokea madai hayo kutoka kwa Dk. Massaburi na kwamba
ameombwa kuwasilisha utetezi wake katika mahakama hiyo ndani ya siku 21.
Aidha, Kubenea alisema katika kesi hiyo, atawakilishwa na jopo la
mawakili watano akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, Mabere
Marando, Peter Kibatala, Method Kimongoro na Frederick Kihwelo na
kwamba wamepanga kuwasilisha utetezi wao ndani ya wiki hii.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment