Social Icons

Pages

Tuesday, December 08, 2015

MAGUFULI AFUTA NYAYO ZA SITTA NA MWAKYEMBE

Kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli, katika kukabiliana na ukwepaji kodi na ufisadi wa fedha za umma imechukua sura mpya baada ya kuwasimamisha vigogo kadhaa wa Mamlaka ya Bandari (TPA) wakiwamo wateule wa waliokuwa Mawaziri wa Uchukuzi kwa nyakati tofauti, Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta.
Mkurugenzi Mkuu wa Bandari aliyeteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi katika ngwe ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Nne iliyomaliza muda wake, Sitta, ni miongoni mwa watu waliosimamishwa kazi kwa amri ya Rais Dk. Magufuli.
Kadhalika, Rais Magufuli alitangaza kuivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari iliyokuwa imeteuliwa na Sitta huku ikiongozwa na Professa Joseph Msambichaka aliyekuwa ameteuliwa kushika nafasi hiyo kwa nyakati tofauti na Dk. Mwakyembe aliyewahi pia kuiongoza Wizara ya Uchukuzi kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Afrika Mashariki na pia Sitta.    
Akitangaza uamuzi wa Rais Maguguli jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema vile vile kuwa ameamuru kukamatwa na kuchunguzwa kwa baadhi ya vigogo wa mamlaka hiyo na taasisi nyingine za umma waliohusika kufanikisha ukwepaji kodi wa makontena 2,431 ulioikosesha Serikali mabilioni ya fedha.
Majaliwa alisema Rais Dk. Magufuli amefikia uamuzi wa kutengua nafasi ya Massawe kutokana na utendaji mbovu wa TPA kwa muda mrefu na pia kwa kitendo chake cha kutochukua hatua kwenye vyanzo sahihi vya upotevu wa mapato.
“Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli amevunja Bodi yote ya Bandari na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari,” alieleza.
Alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya ziara za kushtukiza Novemba 27, 2015 na Desemba 4, mwaka huu.
Wiki iliyopita, Majaliwa alifanya ziara ya ghafla bandarini na kubaini kuwapo kwa makontena 349 yaliyopitishwa bila kulipiwa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam na kuikosesha Serikali takriban Sh. bilioni 80, na hivyo kwa mlinganisho huo, makontena 2,431 yakadiriwa kuikosesha Serikali mapato ya Sh. milioni 557 (takriban Sh. bilioni 560). 
Majaliwa aliongeza kuwa (yeye) amewasimamisha kazi viongozi watano wa taasisi mbalimbali za Serikali waliohusika katika kuidhinisha utoaji wa makontena 2,387 bila kulipiwa kodi na pia watumishi nane waliokuwa wakishughulikia makontena kwenye Bandari Kavu (ICD’s) mbalimbali jijini Dar es Salaam. 
Kwa mujibu wa Majaliwa, wahusika hao (wote) waliosimamishwa kazi kwa kuhusishwa na ukwepaji kodi wa makontena 2,387 wanapaswa kukamatwa mara moja, kuhojiwa na mwishowe waisaidie Bandari kujua kontena zisizolipiwa kodi zilipaswa kutozwa kiasi gani.
Alisema ripoti za ukaguzi wa ndani TPA kwa kipindi kinachoishia Julai 30, mwaka huu, zimebainisha ukwepaji kodi mkubwa ulioisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na kontena hizo (2,387) kuondoshwa bandarini bila kulipiwa kodi.
“Viongozi hawa hawakuwamo kwenye ripoti ya ukaguzi lakini ni wahusika wakuu. Hawa ndiyo waliotoa ruhusa ili makontena yaende kwenye ICDs,” alisema Majaliwa wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Majaliwa aliwataja viongozi hao kuwa ni Meneja Mapato ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu kitengo cha Fedha,  Shaban Mngazija;  aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu (ICD) – ambaye sasa amehamishiwa Makao Makuu kwa Naibu Mkurugenzi, Rajab Mdoe; Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Ibin Masoud; na Meneja Bandari Msaidizi ( Fedha), Apolonia Mosha.
Kadhalika,  Waziri Mkuu aliwataja wasimamizi nane waliosimamishwa kazi kuwa ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Steven Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante na James Kimwomwa ambaye alihamishiwa Mwanza lakini kuanzia sasa anasimamishwa kazi akiwa kwenye mkoa huo.
“Bila wao kuidhinisha hakuna Kontena linaweza kutoka au kwenda kokote. Watumishi wote hao wawe chini ya ulinzi na waisaidie polisi kupata taarifa ya hayo makontena (2,387) ni ya nani na yana thamani gani,” alisema Majaliwa. 
Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza waandishi wa habari kwamba Desemba 3, mwaka huu aliamua kurudi tena bandarini kufuatilia na kuangalia hatua ya udhibiti wa upitishaji wa bidhaa mbalimbali kinyume cha utaratibu. 
“Ziara yangu ilinipa nafasi ya kupitia hatua zote za upitishaji mizigo ambazo pia, kwa mujibu wa taarifa ya Ukaguzi wa Ndani ya tarehe 30 Julai 2015, Mamlaka ya Bandari iligundulika kuwapo kwa mianya mingi ya ukwepaji kodi ikiwamo makontena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi – Septemba 2014 kinyume cha utaratibu,” alisema Majaliwa.
“Vitendo hivi vinaonyesha kuwa bandari yetu hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa kodi na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Serikali haitavumilia kuona watu wachache au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiibia Serikali kwa namna yoyote ile kwa manufaa ya wachache kikifanikiwa kwani bandari ni eneo muhimu ambalo likisimamiwa vizuri, linaweza kukusanya fedha nyingi na kuchangia pato la taifa,” alisema.
 
NYAYO ZA MWAKYEMBE, SITTA
Bodi iliyovunjwa na Rais Magufuli jana iliingia madarakani kufuatia uteuzi uliofanywa Juni 2, mwaka huu na Sitta, ikiongozwa na Mwenyekiti Profesa Joseph Msambichaka huku wajumbe wakiwa ni pamoja na aliyekuwa Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Tulia Ackson (sasa Naibu Spika wa Bunge); Mhandisi wa Ujenzi, Musa Ally Nyamsingwa; Mtaalamu wa Manunuzi na Mjumbe wa Bodi ya Posta, Donata Mugassa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu.
Wengine ni Mhandisi wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Gema Modu; Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Francis Michael; Mkurugenzi wa Mipango NSSF, Crescentius Magori na aliyekuwa Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Flavian Kinunda.
Kabla ya uteuzi huo, Sitta aliivunja Bodi ya Wakurugenzi iliyokuwa imeteuliwa na Mwakyembe Novemba 6, 2012, ikiongozwa pia na Profesa Msambachaka huku wajumbe wake wakiwa Dk. Jabir Kuwe Bakari, John Ulanga, Caroline Temu, Jaffer Machano, Dk. Hildebrand Shayo, Said Salum Sauko, Mhandisi Julius Mamiro na Asha Nasoro.
Bodi hiyo ilidumu kwa miaka mitatu kabla ya kukumbana na ‘rungu’ la Sitta, aliyeingia baada ya Mwakyembe kuteuliwa kuwa Waziri wa Afrika Mashariki.
Awali, alipotua Wizara ya Uchukuzi, Mwakyembe aliwahamisha vituo vya kazi watumishi 27 wa idara mbalimbali bandarini kwa tuhuma za wizi, rushwa na utendaji mbovu na kumteua Madeni Kipande kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TPA, kushika nafasi ya Ephraim Mgawe, ambaye pia aliondolewa kwa tuhuma mbalimbali na sasa anakabiliwa na kesi mahakamani.
Hata hivyo, Kipande (aliyeteuliwa na Mwakyembe), naye hakudumu kwa muda mrefu kwani ujio wa Sitta katika Wizara ya Uchukuzi ulihusisha mabadiliko kadhaa yaliyomuweka kando na nafasi yake kutwaliwa na Awadh Massawe

KATIBU MKUU UCHUKUZI ATEMWA
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Shabani Mwinjaka. Majaliwa alisema uamuzi wa rais wa kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu Mwinjaka umeanza jana na atapangiwa kazi nyingine.
Alisema uamuzi huo ulitokana na ziara yake (Majaliwa) ya Desemba 3, mwaka huu katika Shirika la Reli Tanzania (TRL) ambayo iligundua matumizi mabaya ya fedha Sh. bilioni 13 nje ya utaratibu na kwamba uchunguzi unakamilishwa.
Alisema Katibu Mkuu amesimamishwa kazi kwa sababu ya kutosimamia kwa makini mashirika mawili ya Bandari na Reli ambayo yako chini ya wizara yake.
“Tarehe 3 Desemba, mwaka huu, nilifanya ziara ya kushtukiza pale TRL… nikakuta wametumia visivyo Sh. bilioni 13.5 walizopewa na Serikali. Pia nilikuta wamekopa Sh. bilioni 3 kutoka Benki ya TIB lakini nazo wamezitumia nje ya utaratibu. Fedha hizi zilikuwa ni za kusaidia kuboresha miradi ya shirika lakini wao wamezitumia visivyo uchunguzi bado unaendelea,” alisema Waziri Mkuu.
 
MATUKIO BANDARI DAR
Desemba 3, mwaka huu, Waziri Mkuu alimpa saa tatu Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo. 
Pia, alimpa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye utumiaji wa kujaza karatasi kwa mkono na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment) hadi Desemba 11, 2015.
Ziara ya Majaliwa ya kwanza ilifukuzisha kazi watumishi 12 ambao walifikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi na rais alitengua uteuzi wa Kamishana wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, kwa kushindwa kuchukua hatua kwenye ukwepaji kodi katika kontena 329.
Hata hivyo, Rais alitoa muda wa siku saba kwa kampuni 43 zilizohusika na ukwepaji kodi kulipa haraka kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa na kampuni tatu zimelipa zaidi ya Sh. bilioni 5.
Pia, ziara ya pili ilisimamisha kazi watumishi 34 na kufanya jumla ya waliofukuzwa kazi kuwa 47.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: