
Kasi ya Serikali ya, Rais John Magufuli, katika 
kukabiliana na vitendo vya ukwepaji kodi na pia kubana matumizi yasiyo 
ya lazima ya fedha za umma imeibua mapya kufuatia baadhi ya watu kuanza 
kuhoji ni kwa nini mambo yanayofanyika sasa yalishindwa kufanyika katika
 miaka mitano ya mwisho ya serikali ya awamu ya nne.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe ukihusisha pia mahojiano na baadhi 
ya wachambuzi wa masuala ya siasa, umebaini kuwa, mwenendo wa serikali 
ya Rais Magufuli ambayo hadi sasa bado haijawa na Baraza lake la 
Mawaziri umekuwa ukiwapa matumaini makubwa Watanzania wengi kutokana na 
hatua mbalimbali zinazochukuliwa kwa nia ya kumaliza kero mbalimbali 
katika siku 32 tu za kuwapo madarakani na kuzidi maradufu kasi ya 
serikali kamili ya Rais Kikwete iliyokuwa na jumla ya mawaziri 55 na 
kudumu madarakani kwa miaka mitano, sawa na siku 1,825 (mwaka mmoja ni 
siku 365).
“Hii kasi ya Serikali ya Rais Magufuli inaibua mambo mengi sana. 
Kwanza inawapa matumaini makubwa Watanzania kwa kuamini kuwa miaka 
mitano ijayo, kama kasi hii itadumishwa, maana yake taifa litapiga hatua
 kubwa za maendeleo,” mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa aliiambia 
Nipashe.
“Hata hivyo, kasi hii inaibua maswali mazito kuhusiana na kile 
kilichofanywa na serikali kamili ya awamu ya nne katika kipindi chake 
cha mwisho ikiwa na mawaziri 30 na naibu mawaziri 25… kwa nini 
ilishindwa kushughulikia baadhi ya mambo yaliyokuwa wazi kabisa na 
ambayo Magufuli na wenzake watatu wamefanikiwa kuyafanya katika kipindi 
kifupi cha mwezi mmoja?. Kwakweli kuna mengi ya kujiuliza,” mchambuzi 
huyo alihoji wakati akizungumza na Nipashe.
Mchambuzi mwingine aliiambia Nipashe kuwa, utendaji wa serikali ya 
Magufuli inayoundwa na viongozi wakuu watatu tu, yaani Rais mwenyewe 
(Magufuli), makamu wake Samia Suluhu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, 
tena katika siku 32 tu za kuwa madarakani, unaibua maswali mengi mazito 
kuhusiana na ufanisi wa serikali ya iliyokuwa na mawaziri 55, huku 
ikitumikia wananchi kwa miaka mitano.
“Yapo mengi yanayoibua maswali haya,  kwa mfano, Magufuli na 
wenzake wawili wamefanikiwa kufichua mianya ya ukwepaji kodi mkubwa 
katika Bandari ya Dar es Salaam. Kulikuwa na matumizi makubwa holela ya 
fedha za umma kupitia sherehe zisizo na idadi, semina, makongamano, 
 posho za vikao visivyo na tija, utitiri wa safari na mambo mengi 
yaliyoshughulikiwa na Magufuli na wenzake ndani ya mwezi mmoja tu wakati
 mawaziri wa Rais Kikwete walishindwa kuyashughulikia kwa miaka yote 
mitano ya mwisho. Yapo mengi ya kujiuliza, kwamba je, ni kweli wote 
walikuwa wakifanya kazi kwa maslahi ya umma au ya kwao binafsi?”.
“Na je, ni kweli baadhi yao walizidiwa nguvu ya fedha za baadhi ya 
wafanyabiashara wasio waaminifu au na wao wenyewe walikuwa ni sehemu ya 
mtandao wa hujuma dhidi ya mali za umma?.  Kwakweli maswali ni mengi na 
mazito dhidi ya wasimamizi wa ofisi mbalimbali za umma katika serikali 
iliyomaliza muda wake,” mchambuzi mwingine aliongeza.
Aidha, katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwapo kwa mambo 10 
makubwa ambayo Serikali ya Magufuli isiyokuwa na Baraza la Mawaziri 
imefanikiwa kuyatekeleza kwa mafanikio makubwa licha ya kuonekana kuwa 
yalishindikana katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita na 
kuigharimu serikali mabilioni ya fedha.
Baada ya ushindi wake wa asilimia 58.46 ya kura zote halali 
zilizopigwa katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2015, Magufuli aliapishwa 
Novemba 5, mwaka huu na kuanza kazi siku hiyohiyo kwa kumteua George 
Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
ALIYOFANYA MAGUFULI KWA SIKU 32
1.SAFARI ZA NJE
Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alifutilia mbali 
safari holela za nje alizodai zimekuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya 
fedha kila uchao. Hili alilitolea uamuzi Novemba 6. Akaagiza kuwa safari
 zote muhimu ughaibuni ni lazima zipate ruhusa yake au ya Katibu Mkuu 
Kiongozi Ikulu, lengo ikiwa ni kuokoa fedha zinazoweza kutumiwa kwa 
shughuli nyingine za maendeleo kwa taifa. Akitolea mfano, alisema katika
 mwaka wa fedha wa 2013/2014 na 2014/2015, taifa lilitumia zaidi ya Sh. 
bilioni 356 kugharimia safari za nje; jambo ambalo yeye hayuko tayari 
kulishuhudia. 
Hadi sasa, Magufuli ameshaonyesha mfano kwa kuamuru watu wanne tu 
kusafiri wakitokea ofisi ya ubalozi wa Tanzania Uingereza kwenda 
kumuwakilisha katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola 
kwenye visiwa vya Malta, badala ya watu zaidi ya 50 waliozoea kusafiri 
katika safari kama hii ya Rais. 
Katika serikali iliyokuwa na jumla ya mawaziri na naibu mawaziri 
55, jambo hili halikuwezekana hata kidogo, licha ya kelele nyingi 
zilizokuwa zikipigwa na wananchi mbalimbali akiwamo Mwenyekiti wa 
NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliyedai hali ni mbaya na kwamba, Rais 
Kikwete peke yake alishatumia muda mwingi wa kuwapo madarakani akiwa nje
 ya nchi na kuligharimu taifa wastani wa zaidi ya Sh. trilioni 4.5 
katika miaka 10 ya kuwapo kwake madarakani.
2.  UKWEPAJI KODI BANDARINI, TRA
Hili ni eneo mojawapo kati ya mengi yaliyofanywa kwa umahiri mkubwa
 na ‘jeshi la watu watatu’ la serikali ya Rais Magufuli. Kwa kurejea 
ahadi yake ya kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) inaongeza 
mapato na pia kukomesha vitendo vya ufisadi, tayari Magufuli na serikali
 yake wameibua gumzo kubwa baada ya kufichua ukwepaji kodi uliobaini 
kuwapo kwa makontenda 2,431 yaliyopitishwa katika Bandari ya Dar es 
Salaam bila kulipiwa kodi. Awali, yalinaswa makontena 349 yasiyolipiwa 
kodi na kulikosesha taifa takriban Sh. bilioni 80, hivyo wastani wa 
mapato yaliyokuwa yamepotea kwa makontena 2,431 ni zaidi ya Sh. Bilioni 
557.  
Hadi sasa, tayari watu 47 wamekamatwa na Polisi kuhusiana na tuhuma
 za kuhusika na ukwepaji kodi huo huku baadhi yao wakiwa tayari 
wamefikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka ya uhujumu uchumi, 
miongoni mwao wakiwa Ni maafisa wa vyeo vya juu TRA. Hatua kama hizi 
zilizochukuliwa na serikali ya Magufuli ndani ya siku 32 hazikuwahi 
kuonekana katika kipindi chote cha siku 1,825 (miaka mitano) ya serikali
 iliyomaliza muda wake ikiwa na jumla ya mawaziri 55.
3. VIPIMO CT-SCAN, MRI MUHIMBILI
Licha ya serikali iliyokuwa na mawaziri 55 ya Rais Kikwete kufanya 
kazi kubwa ya kununua mashine za vipimo vya CT-Scan na MRI, bado 
havikuwa vikitimiza malengo ya kutumikia wananchi kwa asilimia mia moja 
kwani muda mwingi zilikuwa mbovu. Hata hivyo, muda mfupi tu baada ya 
kuingia madarakani, Rais Magufuli alivamia Muhimbili na kutangaza 
maamuzi mazito ikiwa ni pamoja na kumuondoa Kaimu Mkurugenzi na kisha 
kuamuru mashine hizo zitengenezwe. Hadi kufikia jana, vipimo vyote 
viwili vilikuwa vikifanya kazi Muhimbili na kuwaondolea kero wananchi, 
jambo lililokuwa likionekana kuwa haliwezekani kufanyika katika serikali
 ya awamu iliyopita kwani licha ya ahadi kadhaa kuwahi kutolewa, bado 
hakukuwa na mabadiliko makubwa.
4.POSHO KAMATI ZA BUNGE
Kwa uda mrefu kumekuwa na malalamiko juu ya matumizi mabaya ya 
fedha za umma kwa kuwalipa posho wabunge hata katika vikao vya kazi zao 
za kila siku, vikiwamo vya kamati kuhusiana na mashirika mbalimbali ya 
umma. Katika siku zake 32, tayari Rais Magufuli kupitia Msajili wa 
Hazina, Lawrance Mafuru, ameshatangaza kufutwa kwa posho za vikao vya 
kamati za Bunge na hivyo kuokoa fedha ambazo sasa zinaweza kuelekezwa 
katika maeneo mengine ya maendeleo. Hili lilishindikana katika serikali 
ya awamu ya nne iliyokuwa na mawaziri 55.
5.GHARAMA SIKU YA UKIMWI, UHURU
Miongoni mwa maeneo yanayoligharimu taifa fedha nyingi ni sherehe, maadhimisho na pia sikukuu mbalimbali za mwaka. Serikali ya Magufuli imeepuka gharama hizi baada ya kufutilia mbali
 gharama za zaidi ya Sh. milioni 200 zilizokuwa zitumike katika 
maadhimisho ya Siku ya Ukimwi mkoani Singida, zaidi ya Sh. bilioni 
zikaokolewa kutoka katika madhimisho ya Siku ya Uhuru na kuelekezwa 
katika kujenga barabara ya lami kutoka Mwenge hadi Morocco jijini Dar es
 Salaam, fedha nyingine Sh. milioni 215 zikaokolewa kutoka katika 
tafrija ya wabunge kujipongeza baada ya kuapishwa na kupelekwa kununulia
 vitanda 300 vya wagonjwa Hospitali ya Muhimbili na pia mamilioni 
mengine ya fedha yameokolewa na Rais Magufuli baada ya kufuta kadi za 
krismasi na mwaka mpya za mwaka huu kwa fedha za umma. Hatua zote hizi 
hazikuwahi kufanyika katika miaka mitano ya mawaziri 55 wa serikali 
iliyomaliza muda wake Novemba 5.
6. SAFARI ZA NDANI
Mbali na kudhibiti safari za nje, Rais Magufuli na serikali yake 
pia amedhibiti safari za ndani baada ya kuagiza kuwa vikao vyote vya 
kikazi baina ya viongozi wa mikoa vifanywe kupitia teknolojia ya video 
(video conference) na siyo kusafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine au 
kukodi kumbi za mikutano. Hili halikuonekana katika serikali iliyomaliza
 muda wake.
7. MICHANGO SHULENI MARUFUKU
Hii ni moja ya ahadi za Rais Magufuli. Katika siku zake 32 akiwa 
madarakani, tayari ameshaagiza utekelezaji wa jambo hili na sasa 
wanafunzi wa darasa la kwanza watakaoanza mwezi ujao hawatakumbana na 
rundo la michango na pia wa sekondari pia watasalimika dhidi ya ada na 
michango. Kero hii ya michango kama ya ulinzi, jembe, madawati, kwanja, 
uji, na mingineyo ilikuwa sugu katika serikali ya mawaziri 55 
iliyomaliza muda wake.
WASOMI WANENA 
Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mtakatifu 
Stefano Moshi (SMMUCo), Dk. Gasper Mpehongwa, anasema katika utawala wa 
Rais Kikwete, ripoti zilikuwa zinatolewa kwa watendaji wa serikali 
lakini haamini kwamba walikuwa wakizitendea haki.
Anasema utawala uliopita ulikuwa na baadhi ya viongozi ambao 
walikuwa hawachukui maamuzi ya haraka na hilo lilikuwa na athari kubwa 
katika utendaji.
“Mimi naamini Rais alikuwa akipewa summary (muhtasari) wa utendaji 
kazi katika kila wizara, ila watendaji wake walikuwa wanamuangusha. Hata
 hili suala la Kamishna wa TRA lingetokea enzi za utawala uliopita 
lingechukua muda mrefu kuchukuliwa maamuzi. Hii ndiyo tofauti iliyopo,” 
alisema Dk. Mpehongwa, akisisitiza kuwa aina ya utendaji kazi wa Rais 
Magufuli na Kikwete ni tofauti na kueleza kuwa katika nchi kama 
Tanzania, anachofanya Magufuli kwa kuchukua uamuzi wa haraka ndiyo 
inayohitajika.
Alisema hata Rais Kikwete alipokuwa madarakani alikuwa anasema ana 
majina ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya lakini hadi 
anaondoka madarakani hakuwahi kuwataja wala kutangaza kuwa amewachukulia
 hatua.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Essau Ntabindi, 
alisema kuna mambo mawili ambayo ana amini yanaweza kuwa yalitokea 
katika utawala wa mawaziri 55 wa Rais Kikwete. Anasema jambo la kwanza uwezekano kuwa mambo ambayo Rais Magufuli 
anayafanya sasa, utawala uliopita wa Rais Kikwete ulikuwa hauyaoni  ama 
ulikuwa unayaona lakini ulishindwa kuchukua hatua za haraka.
Anasema Rais Magufuli ameweza kufanya kazi kubwa kwa kipindi kifupi
 lakini ni lazima awe na Baraza la Mawaziri makini kwani hawezi kufanya 
mambo yote peke yake. “Kwa mfano Rais hawezi kujua wizi wa chaki shuleni unavyofanyika 
au madudu katika halmashauri, lazima atahitaji wasaidizi,” alisema 
Ntabindi.
Mkurugenzi Mkuu wa Sikika, Irenei Kiria, alisema mambo anayofanya 
Rais Magufuli kwa sasa hayajawahi kutokea wala kufanywa hapo kabla.
Anasema Rais Magufuli amefanya kazi iliyowashinda mawaziri 
waliokuwapo katika utawala wa Rais Kikwete na kwamba, hayo yanayofanyika
 sasa ndiyo waliyokuwa wakiyataka wananchi. “Kwakweli anayoyafanya sasa Rais Magufuli yameshitua hadi baadhi ya
 watu wa chama chake kwa sababu sidhani kama walitarajia angeyafanya 
haya,” alisema Kiria.
Anasema maouvu anayoyafichua Rais Magufuli kwa sasa yalikuwapo kwa 
muda mrefu na viongozi walikuwa wanayaona lakini walikuwa hawayachukulii
 hatua, mfano ni ufisadi na ukwepaji kodi bandarini ambao haukuwa jambo 
la siri.
Mwenyekiti wa Wafanyabishara, Johnson Minja, alikuwa anawaeleza 
wakuu wa TRA, Bandari na hata mawaziri wa serikali ya Rais Kikwete juu 
ya namna wafanyabishara wakubwa wanavyokwepa kodi bandarini, lakini mara
 zote alikuwa akipuuzwa.
     CHANZO:
     NIPASHE
    
 

No comments:
Post a Comment