Kasi ya Rais John Magufuli katika kubana matumizi
yasiyo ya lazima ya serikali ili fedha zinazookolewa zielekezwe katika
kuimarisha huduma za jamii imeendelea kuvutia wengi katika nchi jirani
za Afrika Mashariki baada ya jina lake kuanza kutumiwa na wagombea urais
nchini Uganda.
Kati ya wagombea wote, aliyejipambanua kwa uwazi kuwa atafuata
nyayo za Magufuli katika kuhakikisha kuwa serikali inaendesha mambo yake
kwa nia ya kubana matumizi yasiyo ya lazima, kukomesha ufisadia na
mwishowe kuwanufaisha watu wa tabaka la chini kupitia uboreshaji wa
huduma za jamii ni mgombea wa upinzani anayemtikisa Rais Yoweri Museveni
katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Kizza Besigye wa chama cha Forum for
Democratic Change (FDC).
Katika kampeni zake mwishoni mwa wiki, Besigye amesema wazi kuwa
pindi atakapochaguliwa na wananchi na kuingia madarakani, atafuata nyayo
za Magufuli kwa kuanza kuipiga bei ndege inayotumiwa na Museveni kwa
maelezo kuwa inalibebesha taifa lao gharama kubwa ambazo zinaweza
kutumiwa katika kuboresha huduma za jamii.
Uchaguzi Mkuu nchini Uganda unatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Februari, 2016.
Akiwa amefuatana na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Profesa Ogenga
Latigo, kwenye mkutano wa kampeni wilayani Agago nchini humo, Besigye
ambaye pia ni Kanali wa Kijeshi, alisema ataiuza ndege hiyo aina ya
Gulfstream V Jet, iliyoligharimu taifa hilo shilingi za Uganda bilioni
88.2 (Sh. bilioni 55.6 za Tanzania).
Besigye alisema ndege hiyo haiongezi faida yoyote kwa walipa kodi
wa Uganda, licha ya Rais Museveni kudai kuwa anaitumia tu wakati akitaka
kusafiri nje ya nchi, hoja ambayo Besigye anaipinga kwa kuwa hata kama
haitumii kwa safari za ndani, bado inatakiwa mashine zake zitunzwe na
wafanyakazi wake pia wahudumiwe.
Besigye alisema yeye anaunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais
mpya wa Tanzania, Magufuli, ambaye anaishi kulingana na jina lake la
utani la ‘tingatinga’ kutokana na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya
ufisadi, kuongeza ufanisi wa kazi katika ofisi za umma na pia kuongeza
nidhamu ya matumizi kwa manufaa ya taifa na siyo watu wachache.
Magufuli amekuwa akiwavutia Watanzania wengi wa kawaida huku
akijielekeza katika kuhakikisha kuwa anashughulikia kero za wananchi
ambazo zimekuwa zikisababishwa na tabaka la watawala na wafanyabiashara
ambao wamekuwa wakijitajirisha wenyewe. Besigye anaonekana kumuiga
Magufuli kwa kuelekeza kampeni zake katika kushughulikia kero za
wananchi wa kawaida.
Aidha, katika kufuata zaidi nyayo za Magufuli, Besigye amekuwa
akizungumzia masuala yanayohusu hatma ya kila siku ya maisha ya watu wa
kawaida, hasa kina mama wasioweza kupata fedha zinazotozwa kwao wakati
wa kujifungua. Kadhalika, Besigye amekuwa akizungumzia vijana wanaohaha
kutafuta kazi kila uchao baada ya kumaliza shule na pia wananchi wengine
ambao wengi wanakabiliwa na lindi kubwa la umaskini.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment