Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anatarajiwa kuanza kambi nzito
jijini Arusha kuanzia keshokutwa (Jumatano) kwa nia ya kuhakikisha kuwa
mgombea ubunge wa chama chake katika katika Jimbo la Arusha Mjini,
Godbless Lema anatetea kiti chake kwa ushindi wa kishindo.
Taarifa ambazo Nipashe ilithibitishiwa jana na watu wa karibu wa
Lowassa zilieleza kuwa (Lowassa) ataungana na timu ya kampeni ya Chadema
kujichimbia jijini Arusha kwa siku zote zilizobaki za kampeni kabla ya
kufanyika kwa uchaguzi huo Jumapili ijayo.
Uchaguzi wa kumpata Mbunge wa Arusha Mjini haukufanyika Oktoba 25,
2015 kama ilivyokuwa kwa majimbo mengine nchini kufuatia kifo cha
mgombea wa ACT-Wazalendo, Estomiah Mallah.
“Ni kweli, Lowassa atapiga kambi Arusha kuanzia Jumatano
(keshokutwa) kwa ajili ya kuungana na kina Lema ili kuhakikisha kuwa
jimbo hilo linarejea mikononi mwa Chadema kwa ushindi wa kishindo, “
chanzo kiliiambia Nipashe jana.
Kadhalika, ilielezwa kuwa hatua hiyo ya Lowassa ni muendelezo wa
ushiriki wake katika kuiimarisha Chadema kwa nia ya kuleta ukombozi wa
kweli kwa Watanzania. Hivi karibuni alikuwa Mwanza na Geita kwa siku
kadhaa katika kushughulikia mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema
mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ambaye aliuawa kinyama na watu
wasiojulikana.
LEMA MATUMAINI 100%
Katika hatua nyingine, Lema anayegombea kutetea jimbo hilo,
alisema ushindi kwake na chama chake uko wazi kwani wananchi wameamka na wengi wamepania kumrejesha madarakani.
Alisema kampeni zake za nyumba kwa nyumba ndizo zinazomuongezea
uhakika wa kushinda kwani hupokewa vizuri na wote humuahidi kujitokeza
kwa wingi Jumapili ili kumchagua.
“Kwa kweli sijaona nitashindwaje kurudisha ubunge wangu, wananchi wangu wananipa moyo sana,” alisema.
Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni jana, Lema alisema
atakapochaguliwa, kazi kubwa atakayoifanya ni kuhakikisha kuwa mapato ya
Halmashauri ya Jiji yanaongezeka ili kufanikisha dhamira ya kuboresha
huduma za jamii kwa wananchi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment