Social Icons

Pages

Monday, November 09, 2015

WATOTO 68,000 HUFARIKI DUNIA KWA KUKOSA HUDUMA BORA YA UZAZI

 
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Act-Wazalendo, Anna Mghwira. Jumla ya watoto wachanga 68,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa huduma bora ya uzazi kwa mama.
Aidha, jumla ya watoto zaidi ya asilimia 48 hufariki dunia mara baada ya kuzaliwa kuanzia siku moja hadi tano. Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Neema Rusibamayila, wakati akizungumza na wananchi wa jijini Dar es Salaam waliojitokeza kuchangia fedha kwa ajili ya kununua mashine za kuhifadhia watoto waliozaliwa kabla ya miezi tisa (njiti).
Mpango wa uchangiaji hiari wa mashine za kulelea watoto huo, unaendeshwa na Taasisi ya Doreen Mollel, kwa lengo la kupata mashine 80 zitakazogawanywa katika kanda nane nchini ikiwa ni sehemu ya kupunguza vifo hivyo.
“Kwa Tanzania, asilimia 80 ya watoto wanaozaliwa hupoteza maisha kwa matatizo ya kuzaliwa njiti, matatizo ya uzazi na maambukizi ya magonjwa mbalimbali kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” alisema Dk. Maile.
Aliwataka Watanzania kujitokeza kuchangia huduma hizo kwani kila mmoja anajukumu hilo ili kumaliza vifo vinavyozuilika kwa kuhakikisha hospitali zinakuwa na vifaa na huduma bora.
Naye Mkurugenzi wa Doreen Mollel Foundation, Miss Mollel, alisema lengo la kuanzisha mfuko huo ni kuhakikisha watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wanapata huduma bora ili waishi.
“Lengo letu ni kuhakikisha siku ya kuadhimisha mtoto njiti, Novemba 17, tuwe na mashine 10 katika kila kanda nchini ili watoto wanaozaliwa wakiwa na hali hiyo wapate huduma,” alisema Mollel.
Pia alisema katika mchakato huo, wameweza kupata mashine nane hivyo bado wanauhitaji wa mashine nyingine 72 ili zitimie 80. Alibainisha kuwa kila mashine moja inauzwa kiasi cha Sh. milioni 3.5, hivyo ili kupata mashine zote 80, zinahitajika Sh. milioni 280.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambaye alikuwa mgeni rasmi, Paul Makonda (pichani), aliahidi kushirikisha viongozi mbalimbali wa serikali akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ili achangie na kusaidia watoto hao wenye uhitaji.
Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Act-Wazalendo, Anna Mghwira, aliitaka jamii na serikali kushiriki kikamilifu kusaidia watu wenye uhitaji kama watoto hao.
Alisema sekta ya Afya inapaswa kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya kutoa huduma bora hasa ya uzazi ambao ndiyo wenye changamoto kubwa ya vifo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: