Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, jana alipata ajali ya gari jijini Dar
es Salaam na kukimbiziwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako amelazwa.
Awali, taharuki kubwa iliibuka miongoni mwa watu mbalimbali
kutokana na taarifa kusambaa kuwa mkurugenzi huyo anayefahamika na wengi
kutokana na harakati mbalimbali za kupigania haki za binadamu kupata
ajali mbaya, kisha kuonyeshwa picha za gari lililopinduka na kuharibika
vibaya, zikielezewa kuwa ndilo alilokuwamo na kupinduka nalo.
Taarifa za awali zilidai kuwa Dk. Bisimba alipata ajali wakati
akienda kanisani, chanzo kikitajwa kuwa ni gari lake kugongana na gari
jingine.
Hofu kuhusiana na ajali ya Bisimba iliongezwa na baadhi ya watu
waliokuwa wakichangia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa kumpa
pole huku wakikumbushia mkasa mwingine wa kukamatwa kwa wafanyakazi wa
kituo chake waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
25, mwaka kwa ridhaa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondya, alithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo na kusema ilitokea jana asubuhi katika makutano
ya barabara za Bibi Titi Mohamed na Jolly Club. “Kwa sasa nipo katika Hospitali ya Aga Khan. Ni kweli amepata ajali
(Kijo Bisimba) na tutatoa taarifa zaidi kuhusu majeruhi wa ajali hiyo,”
alisema Kamanda Mkondya.
Mkurugenzi wa Utetezi wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu(LHRC), Harold Sungusia, aiiambia Nipashe kuwa ajali hiyo
ilitokea saa 5:00 asubuhi. “Nimepata taarifa saa saba mchana na nikaamua kuja moja kwa moja
hospitali ya Aga Khan, ili kuzungumza na Mkurugenzi mwenyewe na kufahamu
nini kilitokea, kwa sasa naelekea hosptali,” alisema Sungusia.
HOSPITALINI AGA KHAN
Nipashe ilifika katika hospitali ya Aga Khan alikolazwa Dk. Bisimba
na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa LHRC, Ezekiel Masanja, alisema
taarifa za awali zinaonyesha kuwa Dk. Bisimba amevunjika mguu, ingawa
hali yake ilikuwa inaendelea kuimarika.
“Dereva wa Bisimba alikuwa anapatiwa matibabu. Naye amejeruhiwa,
lakini taarifa ya awali ya daktari ni kuwa Mkurugenzi (Dk. Bisimba)
amevunjika mguu, ingawa uchunguzi zaidi unaendelea,” alisema Masanja.
Alisema taarifa walizo nazo ni kwamba ajali hiyo ilitokea wakati
bosi wao akielekea kanisani, baada ya gari lake kugongwa ubavuni na gari
jingine lililokuwa likiendeshwa na kijana mdogo ambaye hakutajwa jina.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment