Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akitoa maoni yake juu ya Bajeti Kuu
iliyosomwa Bungeni mjini Dodoma juzi.
Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), umesema vita ya kurushiana maneno miongoni mwa makada
wa CCM wanaotaka kugombea urais ni faraja kwao, kwani inawasafishia njia
ya kuingia Ikulu .
Katibu Mwenza wa umoja huo, John Mnyika alisema
hayo jana alipokuwa akichambua hotuba za makada wa CCM waliotia nia kwa
nyakati tofauti ya kuwania nafasi ya Urais.
Alisema wagombea wote ndani ya CCM wanapaswa kujua
kuwa hawawezi kushinda uchaguzi ujao kwa kuwa tayari Watanzania
wamekichoka chama hicho.
“Nimesikia ahadi zao za kuomba kura, lakini wajue
serikali ijayo itakuwa ni ya Ukawa na sisi ndio tutaunda Serikali ya
Umoja ya Kitaifa kupitia Ukawa,” alisema.
Mnyika alisema kitendo cha makada hao wa CCM
kutangaza nia huku wakipigana vijembe vya chinichini, ni faraja kwa
Ukawa kwani ‘vita ya panzi ni neema ya kunguru.’ “Waendelee na migogoro yao tu na kutangaza nia
kwenye luninga, lakini wajuwe wananchi tayari wamewakataa kutokana na
kusaliti maoni yao waliyotoa juu ya Katiba,” alisema.
Mnyika alisema Chama Cha Mapinduzi hakiwezi tena
kuaminika machoni pa Watanzania, kwani ukifika wakati wa kula rushwa,
kutetea mafisadi wapo pamoja na hivyo chama hicho kimegeuka cha
mafisadi. “Wamewasaliti wananchi na kutetea wala rushwa
mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali anawataja wezi lakini
hawachukuliwi hatua” alisema.
Mnyika alisema ukawa haimuogopi mgombea yoyote wa CCM na wakati ukifika watamtangaza mgombea wao na ndiye atakuwa Rais.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment