Rais Kikwete akipata mapokezi Rasmi kwa mwenyeji wake Rais wa Finland Mhe Sauli Niinisto.Rais wa Finland, Sauli Niinisto, amesema uhusiano
baina ya Tanzania na Finland ni wa kudumu na utaimarishwa na kutafutiwa
namna ya kuukuza zaidi ya hapa ulipo sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, Rais huyo aliyasema
hayo juzi Ikulu jijini Helsinki wakati wa mazungumzo baina yake na Rais
Jakaya Kikwete.
"Uhusiano wetu ni wa muda mrefu, umedumu kwa miaka 50, tumekuwa na
uhusiano ambao umeleta maendeleo ya kiuchumi kwa Tanzania," alisema na
kuongeza: "Hii inatupa nafasi ya kutafuta mbinu mpya za kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano huu zaidi,"
Rais Kikwete aliwasili Helsinki Juni Mosi, mwaka huu, kwa ziara ya
kikazi ya siku tatu, ambaye pamoja na mambo mengine alimshukuru rais
Niinisto kwa mwaliko wake na kumueleza hali ya kisiasa, kiuchumi na
kijamii nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, Rais pia amemueleza mwenyeji wake kuhusu uchaguzi mkuu ujao nchini Tanzania. "Nimekuja kukushukuru pamoja na wananchi wa Finland kwa ujumla kwa
mchango na misaada yenu ya maendeleo kwa Tanzania tangu nchi yetu ipate
uhuru hadi leo na bado uhusiano wetu upo imara,” alifafanua.
Aidha, aliiomba Finland kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuletea watu wake maendeleo. Pia aliwaaga na kuwashukuru viongozi na washirika wa Tanzania
katika maendeleo, ambao wametoa mchango mkubwa na msaada kwa serikali na
wananchi wa Tanzania katika kipindi chake cha uongozi.
Rais Kikwete pia alifanya mazungumzo na wabunge wa Finland ambao ni
viongozi wa vyama vya siasa nchini humo, wakiongozwa na Spika wao Maria
Lohela, na kwamba ndiye kiongozi wa kwanza kutembelea na kufanya
mazungumzo na wabunge hao walioshika nyadhifa hizo Aprili, mwaka huu.
Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, ametembelea chuo Kikuu cha
Aalto jijini Helsinki ambacho ni chuo cha tatu kwa ukubwa nchini
Finland, pia chuo hicho kina utaratibu wa kubadilishana wanafunzi na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment