Social Icons

Pages

Thursday, June 04, 2015

TEMBO 10,000 RUAHA-RUNGWA WAPOTEA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Zaidi ya tembo 10,000 katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa wamepotea ama hawajulikani walipo.
Akitangaza matokeo ya sensa ya tembo ya mwaka 2014 mjini hapa jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema wataalam wa hifadhi wameshindwa kubaini waliko au nini kimewatokea tembo hao na kulinganisha kupotea huko sawa na ilivyotokea kwa ndege ya Malasia Machi mwaka huu ambayo haijaonekana hadi leo.
Sensa hiyo ilifanywa na Shirika la Taifa la Utafiti Wanyamapori (Tawiri), Frankfurt Zoological Society na Vulcan Inc katika eneo la kilomita za mraba 268,692 ambazo ni sawa na asilimia 28.3 ya eneo lote la nchi, kuanzia Mei hadi Novemba 2014.
Maeneo ilikofanyika sensa hiyo ni Serengeti, Tarangire-Manyara, Katavi-Rukwa, Burigi-Biharamulo, Malagarasi-Muyovosi, Soulus-Mikumi na Ruaha-Ruangwa, Mkomazi na Saadani. “Wizara yangu inajipanga kikamilifu kujua sababu za kupotea kwa tembo hao…je?, waliuawa au waliondoka katika eneo la hifadhi?. Kwa kawaida kama kuna idadi kubwa ya vifo vya wanyama kama hiyo kunakuwa na mabaki ya mizoga au mifupa kitu ambacho hakijaonekana tangu kupotea tembo hao,” alisema.
Idadi ya tembo katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa imepungua kutoka 20,000 mwaka 2013 hadi kufikia 8,272 mwaka 2014. “Tembo 10,000 katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa hawajulikani walipo na wala mizoga yao haijaonekana, wamepotea kama ile ndege ya Malasia. Hali hii inatufanya kuendesha sensa nyingine majira ya kiangazi kuanzia Agosti hadi Novemba, wataalam wanajiuliza kila siku tembo hao wamepotelea wapi, hizi ni habari zinazosumbua,” alisema.
Aidha, alisema matokeo ya sensa hiyo pia yamebaini kuwapo kwa upungufu mkubwa katika mfumo wa ekolojia ya Ruaha-Rungwa. Akitangaza matokeo ya ujumla ya sensa hiyo, Nyalandu alisema imeonyesha kupungua kwa tembo kutoka 110,000 mwaka 2009 hadi 43,330 mwaka 2014.
“Kwa mfano katika Pori la Akiba la Selous lenye ukubwa wa kilomita za mraba 55,000 katika ikolojia yake kulikuwa na upungufu mkubwa wa tembo kwa mwaka 2013,” alisema. Hata hivyo, waziri huyo  alisema idadi ya tembo imeongezeka kutoka 13,000 mwaka 2013 hadi 15,217 mwaka jana, ongezeko ambalo ni zaidi ya tembo 2,000.
Alisema katika ikolojia ya Serengeti kuna ongezeko la asilimia 98 la tembo kutoka 3,068 mwaka 2009 hadi 6,087 mwaka jana. Kwa upande wa ikolojia ya Tarangire-Manyara kuna ongezeko la asilimia 64 kutoka tembo 2,561 mwaka 2009 hadi 4,202 mwaka jana.
Alisema Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Kibondo ilikuwa na tembo 49 mwaka 2009, lakini hadi mwaka jana ilikuwa na tembo 102, wakati Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilikuwa na ongezeko la tembo kwa asilimia 100 yaani kutoka 100 mwaka 2009 hadi 200 mwaka 2014.
Nyalandu aliongeza kuwa katika ikolojia ya Katavi-Rukwa idadi ya tembo imeendelea kubaki ile ile ya 6,396, Malagarasi-Muyovosi ilikuwa na asilimia 81 lakini imeshuka kutoka tembo 15,198 mwaka 2009 hadi 2,953 mwaka jana, wakati Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro kulikua na tembo 450 mwaka 2009 na wameongezeka hadi kufikia tembo 100 mwaka 2014.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: