Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitoa heshima za mwisho wakati wa kuaga
mwili wa marehemu Eugene Mwaiposa, kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma
jana.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT),
Dodoma, Samuel Mshana, amewataka viongozi wakiwamo wabunge katika
kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, kuondoa `presha' na msongo wa
mawazo kwa kumtanguliza Mungu mbele.
Akizungumza katika Ibada Maalum ya kuaga mwili wa Mbunge wa Ukonga, marehemu Eugen Mwaiposa (55), katika viwanja vya Bunge jana, Mshana alisema kipindi hiki cha
kuelekea Uchaguzi Mkuu kuna misongamano ya presha kutoka kwa watu wengi
wanaotaka kuwania nafasi za uongozi na kuwataka wasichepuke kwenda kwa
`sangoma' (waganga wa kienyeji).
Mwaiposa anayetarajiwa kuzikwa Jumamosi, jijini Dar es Salaam,
alifariki dunia usiku wa kumkia juzi kutokana na tatizo la shinikizo la
damu akiwa amelala nyumbani kwake, mjini hapa. “Naomba mshushe presha, sisi tunawaombea, msipoteze matumaini kwa
kuchepuka na kwenda kutafuta mambo mengine kwa sangoma,” alisema.
Alisema kipindi hiki ni cha watu kujichunguza mienendo yao na
kwamba mpaka mtu anafikia hatua ya kutangaza nia ajue kuwa amemsimamia
Mungu badala ya kutegemea michepuko. “Chunguza njia zao na kuzijaribu, kama hamkutuhudumia vizuri huu ni
muda wa sisi kuwachapa, kama humkutoa huduma sawasawa huu si muda wa
wewe kukimbilia kwa sangoma,” alisema.
Mchungaji Mshana alisema kuna watu wamepoteza matumaini na kuhoji
kwa nini wanapoteza matumaini haraka hivyo na kuwataka kurudi kwenye
imani.
Katika Ibada hiyo, Naibu Spika, Job Ndugai, Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa,
Kaimu Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu na Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ni kati ya viongozi walioongoza kuaga
mwili wa marehemu. Katika viwanja vya Bunge, familia ya marehemu
ikiongozwa na mume wake, Ally Mwaiposa, iliingia saa 6:01 mchana na
mwili wa marehemu uliingia viwanjani hapo saa 6:14 mchana ukitokea
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ulikokuwa umehifadhiwa.
BUNGE LAMLILIA
Katika salamu za rambirambi, Naibu Spika Ndugai, alisema Bunge limepoteza msemaji na mtu wa vitendo.
Alisema Mwaiposa alikuwa mmoja wa wanawake aliyethubutu kuingiia ubunge kwa ngazi ya jimbo na alipambana na kushinda. Alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliyekuwa safarini Geneva,
amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa hizo na kwamba atashiriki katika
maziko yatakayofanyika Jumamosi.
Mwakilishi wa familia ya Mwaiposa, aliomba Bunge limuenzi Mwaiposa
kwa kujadili mchango wake aliotaka kuchangia katika Wizara ya Elimu
Jumatatu, lakini kutokana na kujisikia vibaya na kurudi nyumbani
kupumzika, aliwaomba wabunge wenzake wamsaidie kutoa mchango wake
uliohusu jimbo lake.
LUKUVI: CCM IMEPATA PIGO
Kwa upande wa serikali, Waziri wa Nchini, Waziri Mkuu (Sera na
Uratibu), Jenister Mhagama, alisema CCM imepata pigo kwenye jimbo lake
la Ukonga na hasa kwa wananchi aliokuwa akiwawakilisha. “Alikuwa hodari na mwaminifu kwa wapiga kura wake alikuwa tegemeo
kubwa na jembe imara kwa CCM, amekufa akifikiria wananchi wake,”
alisema.
Alisema ndani ya bunge alikuwa ni rafiki wa kila mtu bila kujali huyu anatoka chama cha upinzani au chama chake.
KAMBI YA UPINZANI: ALIKUWA MBUNGE WA PEKEE
Kaimu Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema Mwaiposa alikuwa mbunge wa kipekee. Alisema Jimbo la Ukonga lina watu wengi na lipo katika mkoa wa Dar
es Salaam ambao ni wa kisiasa, lakini alifanikiwa kushinda ubunge na
kwamba alikuwa mfano si kwa wanawake tu bali kwa wabunge wote.
WABUNGE WANAWAKE: NI PIGO KWETU
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wabunge Bungeni, Anna Abdallah,
alisema kifo hicho ni pigo kwa akina mama kwa kuwa alikuwa mtendaji,
shupavu, jasiri na mpigania haki za wanawake wenzake ndani na nje. Alisema kutokana na ucheshi na urafiki kwa wabunge wenzake walizoea
kumuita “Dear”. “Kwa heri Dear wetu, umetangulia na sisi tuko nyuma
yako.”
KAMATI YA TAMISEMI: ALIKUWA MAKINI
Mwenyekiti wa Kamati ya Tamiseni, Dk. Khamis Kigwangwala, alisema
Mwaiposa alihamishiwa katika kamati yake akitokea Kamati ya Mambo ya Nje
kutokana na umakini na weledi wake wa kutosha kwenye mahesabu.
JK AMLILIA
Rais Jakaya Kikwete, ametuma salamu za pole kwa Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia na ndugu na kueleza kuwa
amepokea kwa mshutuko na masikitiko taarifa za kifocha Mbunge Mwaiposya.
“Kwa hakika, taifa letu limepoteza kiongozi muhimu kutokana na
kifo hiki. Mbunge Mwaiposya alikuwa mwakilishi hodari na mtetezi wa
kuaminika wa wananchi wa Jimbo la Ukonga. Napenda kukutumia wewe
Mheshimiwa Spika salamu zangu za rambirambi kwa kupoteza Mbunge mahiri
sana. Aidha, kupitia kwako, nawatumia Wabunge wote salamu zangu za
rambirambi kwa kuondokewa na mwenzao," ilisema taarifa ya Ikulu jana.
Rais Kikwete aliongeza: “Kupitia kwako, Mheshimiwa Spika, napenda
pia kutuma salamu zangu kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga ambao wamepoteza
mwakilishi wao. Vile vile, napenda kutoa pole nyingi kwa familia, ndugu
na jamaa wa Mbunge Mwaiposya kwa kuondokewa na mama na mchangiaji
mkubwa katika maisha yao.”
Rais Kikwete alisema yupo pamoja na waliokubwa na msiba huo kwa
kuwa anaelewa uchungu wao katika kipindi hiki na nawaombea subira ili
waweze kuvuka kipindi hiki, ikiwa ni pamoja na kuungana na waombolezaji
kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Mheshimiwa Eugenia
Mwaiposya. Amina.
MEYA SILAA AIFARIJI FAMILIA
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, ameifariji familia ya Mbunge Mwaiposo, katika eneo la Kipunguni B, Dar es Salaam.
Akizungumza na NIPASHE, Meya huyo alisema amepokea kifo hicho kwa
kwa masikito makubwa kwa kuwa alikuwa kiongozi makini aliyewatumikia
wananchi wake vyema huku akisisitiza yale yote waliyojadili katika vikao
kabla ya umauti wake yatekelezwe kama njia ya kumuenzi. “Nimesikitishwa sana na kifo chake kimekuja ghafla bila kutegemea
tutakuwa bega yale yaliyopangwa kutekelezwa na marehemu yatatekelezwa
kama njia ya kumuenzi,” alisema.
Kwa upande wa Diwani Kata ya Kipawa (CCM), Bona Kaliwa, alisema
msiba kifo hicho kimemshtua kwa kuwa marehemu alikuwa msaada kisiasa na
kifamilia.
Msemaji wa familia, Winston Simbo, alisema mwili wa marehemu
umewasili jana saa 8 mchana, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere (JNIA), kutoka Dodoma na kupelekwa moja kwa moja kuhifadhiwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema mwili utazikwa jumamosi nyumbani kwake baada ya watoto wake
kurejea kutoka nje ya nchi. Aidha, alisema watoto marehemu
wanaosubiriwa ni Mecktilida Mwaiposa anayetokea Cananda na Samira
Mwaiposa kutoka nchini Malaysia. Marehemu ameacha watoto wawili na mume.
Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,Amen
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment