Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi.
Umoja wa wafanyabiashara Soko la Machinga Complex,
jijini Dar es Salaam, umeeleza kusikitishwa na tetesi za kuuzwa kwa
jengo hilo kwa mwekezaji kutoka China hivyo kumwomba Rais Kikwete,
kuingilia kati kabla hajaondoka madarakani.Tetesi hizo zilibainishwa jana na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo,
Gerald Mpangama, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maendeleo ya soko hilo na kupinga taarifa aliyodai kutolewa na Meya wa
jiji hilo, Dk. Didas Masaburi, kwamba hatambui upangaji wa shule ya
Lamoon kwenye jengo hilo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, suala la uuzwaji wa jengo hilo
lililojengwa kwa mkopo na Shirika la Hifadhi la Jamii (NSSF), kwa
Sh.bilioni 12, lilijadiliwa katika kikao chake cha bodi hivi karibuni. Alisema wafanyabiashara hawako tayari kuona jengo hilo, ambalo
lilijengwa na serikali kwa ajili ya kupunguza changamoto ya maeneo ya
kufanyia biashara kwa wafanyabiashara ndogondogo ‘machinga’, likiuzwa.
“Sisi wafanyabiashara wa Machinga Complex, tunasema msimamo wetu
utakuwa palepale kwamba jengo hili lilijengwa na serikali kwa ajili ya
kutatua au kupunguza suala zima la maeneo ya kufanyia biashara kwa
wafanyabiashara wadogowadogo nchini,” alisema na kuongeza:
“Tunaomba serikali kupitia Rais wetu, ambaye kwa nia na dhamira
yake nzuri kwetu sisi na wafanyabiashara wadogo wa Machinga Complex,
tunamuomba alizungumzie suala hili la uuzwaji wa jengo letu la Machinga
Complex na kulitolea ufafanuzi katika moja ya hotuba zake za mwezi kabla
hajaondoka kwenye kiti chake cha urais.”
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, hawajashirikishwa wala hawajui mauzo
yake yataanza lini japokuwa tayari wameshabaini mwekezaji kutoka China
akija kupiga picha jengo hilo kwa madai ya mauzo ya takribani Sh.
bilioni 38.
Kuhusu kupangishwa kwa shule hiyo katika jengo hilo, Mpangama
alisema anayehusika kutia sahihi ya mkataba huo ni halmashauri ya jiji,
ambao ndio wenye jengo na wala hakuna mahali popote katika nyaraka zake
panapomruhusu meya wa jiji kuweka sahihi.
Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa jiji hilo, Wilson Kabwe,
alisema hana taarifa yoyote ya kuuzwa kwa jengo hilo, lakini wapo katika
mazungumzo na NSSF kuhusu urejeshwaji wa deni hilo ambalo kwa sasa
limefikia Sh. bilioni 34 kutoka Sh. bilioni 12.
Kwa upande wake, Masaburi alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, simu
yake haikuwa hewani na alipotumiwa ujumbe wa maandishi haukujibiwa.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment