
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
Serikali ya Marekani imesema itaendeleza mahusiano
baina yake na Tanzania katika sekta ya nishati ili kukuza uchumi na
kujenga miundombinu endelevu katika sekta hiyo.
Katibu Msaidizi wa Nishati na Mafuta wa Marekani kutoka Idara ya
Nishati, Christopher Smith, aliyasema hayo jana mara baada ya kutembelea
mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi unaodhaminiwa na Marekani kupitia
mradi wa MCC.
Alisema serikali za Marekani na Tanzania zitaendelea kushirikiana
katika masuala ya nishati ili kufikia malengo waliyopanga ya kuhakikisha
tatizo la ukosefu wa umeme kwa wananchi linamalizika. Alisema mradi wa ujenzi wa vinu vya kusambaza umeme wa Kinyerezi
vitatumia gesi utakapomalizika kutasaidia kwa asilimia kubwa kusambaza
umeme kwa wananchi.
Naye Meneja Miradi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Simon
Jilima, alisema ujenzi wa mradi huo wa uzalishaji umeme kwa sasa
umefikia asilimia 88. Alisema hatua inayoendelea kwa sasa ni kuunganisha nyaya katika
gridi ya taifa na nguzo zimeshawekwa ili majaribio yatakapoanza ya
kuwasha mtambo huo umeme uweze kuingia moja kwa moja.
Alisema majaribio ya kuwasha mtambo huo yataanza Julai, mwaka huu,
lakini kutakuwapo na majaribio ya awali yatakayoanza mwishoni mwa mwezi
huu. “Umeme utaanza kuingizwa katika gridi ya taifa mwezi ujao, lakini
ni lazima kuwa na majaribio na siyo kuwasha moja kwa moja hivyo
majaribio yataanza mwishoni mwa mwezi huu,” alisema Jilima.
Alisema majaribio hayo yatafanyika katika mitambo na katika njia za
kupitishia umeme na yanaweza kudumu kwa kipindi cha mwezi mmoja na kwa
wakati wa kufanya majaribio hayo uzalishaji utakuwa unaendelea. Alisema mtambo huo utakapokamilika utakuwa na uwezo kwa kuzalisha megawati 150 za umeme.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment