Waziri Mkuu Mizengo
Pinda atakipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bunda,
baada ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kutishia kuwa hawatakipigia
kura kutokana na kiongozi huyo kutoa ahadi hewa ya upatikanaji wa maji
safi na salama.
Wakazi hao wameapa kuwa labda ahadi hiyo
iliyotolewa na Waziri Pinda Machi mwaka jana, itekelezwe kabla ya
Uchaguzi Mkuu, kinyume cha hivyo hawataipigia kura CCM ili kuonyesha
kuwa hawaridhiki na namna wanavyodanganywa.
Wakazi hao walitoa tishio hilo juzi katika mkutano
wa hadhara uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo, Katibu
wa CCM mkoa wa Mara Adam Ngalawa na Naibu Katibu wa Umoja wa Vijana wa
CCM (UVCCM) Mfaume Kizigo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano
huo, walisema, wameazimia kutoipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba kwa kuwa viongozi wa CCM na Serikali yake wanatoa ahadi za uongo
na zisizotekelezeka.
Michael Kweka alitaja ahadi iliyotolewa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda Machi mwaka jana kwamba tatizo la maji lingekoma
Juni, kuwa ni moja ya ahadi hewa za viongozi wa Serikali ya CCM
zinazowachefua wananchi. “Hatutawapigia kura za urais, ubunge wala udiwani
wagombea wote watakaoletwa na CCM mwaka huu kwa kuwa wanakuwa
wakitudanganya kwa ahadi hewa,” alisema Kweka.
Kweka alisema akiwa ziarani wilayani Bunda Machi
mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa ahadi kwamba tatizo la maji
lingekwisha ifikapo Juni mwaka huu, lakini hadi sasa hakuna dalili
zozote za kumaliza kero hiyo.
Alisema hali hiyo inawafanya wakazi wa mji huo
ambao wamekuwa wakidamka nyakati za usiku kutafuta huduma ya maji safi
na salama kuichukia Serikali ya CCM, wakiamini kuwa haiwajali. “Mimi
kero yangu ni maji. Hiki kimekuwa kilio chetu kwa muda mrefu.
Lakini kinachotuumiza ni ahadi hewa za viongozi wa
Serikali ya chama chetu cha Mapinduzi kuhusu mradi unaotekelezwa hapa.
Mnaonaje tukiwanyima kura sababu mmezidi ubabaishaji,” alisema mkazi
mwingine wa eneo hilo akiwahoji viongozi wa CCM waliokuwapo meza kuu.
Nyerere Lucas aliilalamikia Serikali ya CCM kwa
kile alichoeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi zake za kuboresha
miundombinu ya barabara wilayani humo kama ilivyoahidi katika Uchaguzi
Mkuu uliopita na kuwafanya wakazi wa maeneo hayo kusafiri kwa tabu
kutafuta maji mbali na maeneo yao. Kero nyingine walizolalamikia wakazi
wa wilaya hiyo ni mikopo kwa vijana na akinamama.
Walisema mikopo kwa makundi hayo imekuwa ikitolewa
kwa watu maaalum hasa vikundi vinavyomilikiwa na watumishi wa serikali,
jambo ambalo limeonekana kwamba kuna nia ya dhati ya kuwasahau
wananchi.
Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoa wa Mara, Adam
Ngalawa katika majibu yake ameshindwa kueleza lini mradi huo wa maji
utakamilika badala yake akasema umepangwa kutekelezwa katika bajeti ya
mwaka 20015/16.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mfaume Kizigo aliwataka
viongozi wa chama hicho ngazi zote kutokaa ofisini badala yake waende
kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitafutia majawabu.
viongozi hao wa CCM walikuwa katika ziara ya kukijenga chama katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment