Kada wa CCM, Amos Siyantemi akipongezwa na wafuasi wake baada ya
kuchukua fomu za kuomba kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano
kupitia chama hicho makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana.
Mtumishi wa CCM katika
Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Amos Siyantemi, amesema idadi
kubwa ya Watanzania wameanza kupoteza imani kwa Serikali na kuendelea
kuamini kuwa chama hicho hakijali wanyonge.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi
wa Halmashauri ya CCM mjini hapa jana baada ya kuchukua fomu ya kuomba
ridhaa ya chama chake kuwania urais, Siyantemi alisema kaulimbiu yake ni
Sura Mpya, Fikra Mpya.
Alisema endapo atateuliwa na chama chake na
kuchaguliwa na wananchi kuwa rais, miongoni mwa mambo atakayozingatia ni
kudumisha amani kwa kurejesha mfumo wa nyumba kumikumi akisema kutakuwa
na daftari la wakazi litakaloorodhesha watu wote wanaoishi katika eneo
husika na shughuli zinazofanyika.
Siyantemi ambaye alitumia nafasi hiyo kuzindua
kitabu chake cha CCM na mapambano ya uongozi, alisema hali ya usalama
nchini imeanza kulegalega kutokana na kukithiri kwa matukio ya uvamizi
wa vituo vya polisi, mauaji ya askari, wizi wa silaha, mauaji ya albino,
uhalifu wa kutumia silaha na aina nyingine. Kuhusu rushwa alisema
endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo ya juu, atahakikisha kuwa
watakaokamatwa na rushwa watafilisiwa mali zote.Mengine ambayo
atayazingatia ni umoja na mshikamano wa Taifa, kuimarisha usalama wa
nchi, kurejesha imani na matumaini ya wananchi kwa Serikali ya CCM.
“Rushwa imeendelea kuwa ugonjwa mbaya kabisa unaoiangamiza jamii. Kwa
sasa jamii yetu imegubikwa na matatizo makubwa kama vile kushamiri kwa
tabia ya kuabudu mali na fedha hali iliyokuza ubinafsi miongoni mwa watu
nchini,” alisema. Siyantemi alisema tofauti hiyo imesababisha
kupanuka kwa tabaka dogo la walionacho dhidi ya idadi kubwa ya
wasionacho wanaoishi katika lindi la umasikini, ujinga na maradhi.
Kupoteza imani na CCM
“Idadi kubwa ya Watanzania wameanza kupoteza imani
kwa Serikali na kuendelea kuamini kuwa CCM kwa sasa ni chama
kisichojali wanyonge na kwamba kimeachana na misingi yake ya ujamaa na
kujitegemea,” alisema. Alisema machoni mwa Watanzania, CCM inaonekana
kuwa chama kinachokumbatia matajiri na wafanyabiashara na si chama cha
wakulima na wafanyakazi kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Julius Nyerere.
Siyantemi alisema atahakikisha anaongeza juhudi za
pamoja za kupiga vita ujinga, umaskini, maradhi pamoja na kulipatia
ufumbuzi tatizo la ukosefu wa ajira kwa kuchochea mapinduzi katika sekta
mbalimbali ikiwamo kilimo na ufugaji. Aliahidi kufanya uwekezaji mkubwa
wa maendeleo ya sayansi na teknolojia katika maeneo yote muhimu ikiwamo
sekta ya elimu, sekta ya utoaji huduma na sekta ya uzalishaji mali,
kuendeleza juhudi za pamoja za kuyapatia makundi mbalimbali fursa sawa
kisiasa, kijamii, kiuchumi na kuutazama upya mfumo wa elimu. Alisema
baadhi ya mikakati ya kufanikisha mapinduzi hayo ni pamoja na kufufua
viwanda vya zamani, kujenga viwanda mama, viwanda vya kati, viwanda
vidogo pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa.
“Mikakati mingine ni kukuza sekta binafsi na
kupanua fursa za uwekezaji, kuhimiza ari ya kufanya kazi kwa bidii na
fikra za kimaendeleo miongoni mwa vijana, kuwahimiza Watanzania wakiwamo
vijana kujiunga katika vikundi vya ushirika wa kuweka na kukopa pamoja
na vikundi vya uzalishaji mali,” alisema.
Aliahidi kuwaboreshea maslahi ya watumishi wa CCM
endapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa rais. Kwa mujibu wa utaratibu wa
chama hicho, Rais wa nchi ndiye anayekuwa mwenyekiti wake.
Alivyochukua fomu
Siyantemi alifika kuchukua fomu akisindikizwa na watumishi wa makao makuu ya chama hicho wengi wao wakiwa wamevaa sare za CCM. Watumishi hao walionekana kushangilia karibu kipindi chote alichokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Baada ya kumaliza mazungumzo hayo, baadhi ya watumishi hao walikwenda kumkumbatia wakimpongeza.
Amos Siyantemi ni nani?
Amos Siyantemi alizaliwa Aprili 29, 1975 wilayani
Magu mkoani Mwanza. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya
Nyambitilwa (1983-89), kabla ya kujiunga na elimu ya sekondari katika
Shule ya Kinango kati ya mwaka 1994 na 1997.
Mwaka 1999 -2001 alikuwa Shule ya Sekondari
Makongo akisoma kidato cha tano na cha sita, kabla ya kujiunga na Chuo
kikuu cha Dar es Salaam alikohitimu Shahada ya Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa kati ya mwaka 2002-2005.
Mwaka 2007 hadi 2012 alikuwa katika Chuo cha
Diplomasia Dar es Salaam alipohitimu Shahada ya Uzamili katika masuala
siasa na uhusiano wa kimataifa.
Ajira yake ya kwanza ilikuwa ni katika ofisi ndogo
za makao makuu ya CCM akiwa katibu msaidizi kwenye Idara ya Itikadi na
Uenezi.
Mwaka 2006 alipata uhamisho kwenda Geita, ikiwa ni
utaratibu wa CCM wa kuwaandaa watendaji wake kuyafahamu mazingira ya
uongozi kwenye wilaya mbalimbali. Huko alihudumu cheo cha katibu
msaidizi na mhasibu wa wilaya.
Mwaka 2008 alihamishiwa Kilwa mkoani Lindi
akihudumu kwa nafasi hiyohiyo, mwaka 2009 aliteuliwa kuwa mjumbe wa
Baraza la Umoja wa vijana CCM mkoani humo.
Mwaka 2010, alirudishwa tena makao makuu na kuwa katibu msaidizi mwandamizi kwenye Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Mwa 2012, yalipofanyika mabadiliko na Dk Asha Rose
Migiro, akachukua nafasi ya January Makamba na kuwa Mkuu wa idara ya
Siasa na Uhusiano wa Kimataifa. Hapo ndipo alipopata nafasi ya
kupandishwa daraja na kuwa katibu msaidizi mkuu, anayeratibu uhusiano
kati ya CCM na vyama vya ukombozi nafasi anayoifanyia kazi hadi sasa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment