Kada wa CCM kutoka Wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza, akimkabidhi,
Mbunge wa Jimbo hilo, William Ngeleja (wa pili kulia) kiasi cha
Shilingi Milioni moja kwa ajili ya kuchukulia fomu ya urais.
Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja ametangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM, huku
akiahidi kupambana na mambo sita aliyoyaita maadui wakuu wa nchi ambayo
ni umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
Akitangaza nia hiyo kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) Mwanza jana, Ngeleja alisema anatambua kwamba Watanzania
wa leo wanatamani kumpata rais ambaye atapambana kwa dhati na vitendo na
maadui hao.
“Nina mikakati madhubuti ya kujibu swali la
kiutafiti linaloonyesha kwamba mamlaka, idara na taasisi za umma zenye
dhamana kubwa ya maisha ya Watanzania mfano, Polisi, Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na watendaji wakuu wa taasisi za biashara (CEO) ndiyo
wanaoongoza kwa tuhuma za kupokea rushwa,” alisema.
Ngeleja akiwa ameambatana na mkewe, Blandina na
Mwenyekiti wa Kamati yake ya Maandalizi, Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu
waliingia ukumbini saa sita mchana na kupokewa na makada wa CCM
waliohudhuria ambao walitoka maeneo mbalimbali ikiwamo vyuo vikuu,
wajumbe wa halmashauri kuu kutoka bara na visiwani, wawakilishi wa
wamachinga na wavuvi.
Alisema Watanzania wanatamani kuwa na rais ambaye
atasimamia kwa dhati umoja na mshikamano wa kitaifa, Muungano, kulinda
amani, kukemea kwa nguvu zote ubaguzi wa dini, kabila, rangi na aina
nyingine yoyote ya ubaguzi inayoweza kujitokeza nchini na kuendelea
kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi.
“Historia ya nchi yetu ni ndefu na imepita misukosuko mingi lakini kwa umoja, udugu na mshikamano wetu tumefanikiwa,” alisema.
Hata hivyo alisema hivi sasa rushwa, ufisadi, uvivu na mmomonyoko wa maadili ni maadui wengine walioongezeka kwa kasi. “Kadri Watanzania tunavyozidi kuongezeka kwa idadi
na maadui zetu hawa nao wanazidi kujitanua. Hivyo mbinu, mikakati na
silaha za kupambana na maadui hawa lazima zibadilike,” alisema.
Ngeleja alisema baada ya kushauriwa na baadhi ya
Watanzania kutoka pande zote za nchi tena wa kada mbalimbali
amejitafakari, kujitathmini na kujiridhisha kuwa anayo dhamira ya kweli
kuwatumikia Watanzania.
“Nimejitafakari, nimejitathmini na kujiridhisha
kwamba ninayo dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania kupitia nafasi
ya urais. Mbali ya dhamira ya kweli nimejipima kwamba ninao uwezo wa
kubeba matarajio ya Watanzania, kupitia utekelezaji wa kaulimbiu yangu
isemayo: “Maono Sahihi, Mikakati Thabiti, Matokeo Halisi (MMM),”
alisema.
Alisema mwaka huu siyo wa siasa za kawaida kama
ilivyozoeleka, utakuwa wa kutathmini hatma ya Taifa, kujitazama na
kujiuliza, malengo na dira na juhudi za kila Mtanzania mmojammoja na
kwamba, rais ajaye lazima atoe matokeo halisi dhidi ya umaskini, ujinga,
maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
Azungumzia kujiuzulu, escrow
Akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari, Ngeleja
alisema hakufukuzwa uwaziri kwa sababu ya kashfa, bali ni mabadiliko ya
kawaida na kwamba, ambaye ana ushahidi kuwa alifukuzwa kwa kashfa anampa
nafasi kuuwasilisha.
“Sikuondolewa kwa kashfa, CAG (Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali) hajanitaja hata kwa herufi moja. Mwenye
taarifa sahihi ajitokeze kesho na ushahidi anipinge kwamba niliondolewa
kwa kashfa,” alisema Ngeleja na kuongeza:
“Mara kadhaa imekuwa ikisemwa kumbukumbu zipo kwa
sababu mamlaka zipo, mabadiliko yaliyofanyika Novemba 4, 2012 yalikuwa
ya kawaida, sikuwa, hata sasa siwezi na haitakuwa kuondolewa kwenye
nafasi ya uwaziri kwa kashfa.”
Kuhusu kashfa ya Escrow iliyosababisha kuvuliwa
uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Ngeleja
alisema hawezi kuzungumza zaidi ya yale aliyozungumza Rais Jakaya
Kikwete Desemba 22 mwaka jana.
“Mimi bado ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
kutoka Wilaya ya Sengerema…naamini Watanzania watanipima kwa yale
niliyofanya, naamini ninafaa kuliko wenzangu kwa mazingira ya sasa,”
alisema.
Kasi ya maendeleo
Ngeleja alisema Watanzania wanatambua wazi kwamba
aina ya uongozi watakaoweka madarakani ndiyo utakaotafsiri aina na kasi
ya maendeleo wanayotaka kati ya sasa na mwaka 2025, hivyo ni fursa
nyingine ya kumchagua rais mzalendo na mchapakazi, anayekerwa na
umaskini wa wenzake wengi.
“Maendeleo ya kweli ya nchi yetu hayawezi kuletwa
na sekta ya umma peke yake, bali yataletwa kwa kushirikisha kikamilifu
sekta binafsi, ni muhimu rais wa awamu ya tano awe na weledi wa kutosha
kuhusu utendaji wa sekta ya umma na binafsi,” alisema.
Pia, alisema atasimamia vizuri rasilimali za Taifa
zilizopo sasa kwa manufaa ya Watanzania wote na kuzikabili changamoto
za sasa na zijazo na kwamba, matarajio ya Watanzania ni kumpata rais
mwenye hofu ya Mungu ambaye hataongoza nchi kwa jazba, mihemko wala
visasi.
Umaskini
Alisema sehemu kubwa ya Watanzania ni watoto wa
wakulima, wafugaji wa ng’ombe na wavuvi na kwamba kihistoria, wazazi wa
vijana wengi hawakubahatika kusoma, hivyo wamekulia na kuuishi umaskini.
Ngeleja alisema kutokana na ukweli huo, Watanzania
wengi wanajua madhila ya umaskini vizuri na kuongeza kuwa, dhamira ya
kupambana nao ni sehemu ya maisha yao.
Keki ya Taifa
Jeuri yake
“Hata kwa upande wangu, ujasiri wa kujitosa katika
kinyang’anyiro hiki unatokana na dhamira ya kweli ya kupambana na
umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi, uvivu na mmomonyoko wa
maadili kwa nchi yetu,” alisema Ngeleja na kuongeza:
“Shauku yangu ya kupata mafanikio ni kubwa kuliko
hofu yangu ya kushindwa. Hii inatokana na ukweli kwamba shauku yangu hii
ni dhamira ya dhati kuwakomboa wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji
wadogo, wajasiriamali ambao ndiyo kundi kubwa la Watanzania
linalokabiliwa na umaskini. Ukubwa wa kundi hili unaifanya shauku yangu
ya kufanikiwa, kuwa kubwa zaidi kuliko hofu ya kushindwa.”
Alisema atakuwa na jibu la swali la msingi kwamba
kwa nini wakati takwimu zinaonyesha uchumi unakuwa kwa wastani wa
asilimia saba takriban kwa muongo mzima mfululizo, umaskini unapungua
kwa wastani wa asilimia mbili kwa mwaka.
Keki ya Taifa
Ngeleja alisema atasimamia ugawanaji wa pato la
Taifa na kwamba mikoa mingine inachangia zaidi lakini ipo nyuma kwa
maendeleo, kwa sababu ya kutokuwapo kwa mgawanyo sawa wa keki hiyo.
Alisema licha ya uchumi kukua: “Takwimu za makazi
zinaonyesha takriban asilimia 70 ya Watanzania bado wanaishi nyumba za
tembe, wanaoishi katika nyumba bora ni asilimia 30 tu ya zaidi ya
milioni 45,” alisema.
Aliahidi kuboresha huduma za jamii, elimu, afya,
maji haraka iwezekanavyo, ndani ya muda mfupi ujao na kwamba ana
mikakati thabiti na bora ya kurekebisha kasoro zinazohusu mikopo ya
wanafunzi vyuoni na kupunguza tatizo la ajira nchini.
Jeuri yake
Ngeleja alisema akigeuka nyuma na kuangalia
alikotoka kutokana na utendaji wake kuhusu ya mambo aliyosimamia na
kuyatekeleza alipokuwa Wizara ya Nishati na Madini (Januari 2007 – Mei
2012), anamejipima na kuridhika kwamba anatosha.
“Tuliasisi mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara –
Dar es Salaam mwaka 2009, utekelezaji wake ukaanza 2011 na
utakapokamilika baadaye mwaka huu utaliwezesha Taifa kuokoa zaidi ya
Sh1.6 trilioni zinazotumika sasa kugharamia mitambo ya kufua umeme kwa
kila mwaka. Mradi huu ni mwarobaini wa kero ya mgawo wa umeme nchini,”
alisema.
Alisema walianzisha mradi kabambe wa kusambaza
umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) nchi nzima
kuanzia mwaka 2009, baada ya kutengewa Sh27 bilioni lakini kutokana na
mafanikio waliyopata, bajeti ya mwaka 2010/11 iliongezeka hadi Sh137
bilioni.
“Tulibuni na kuanza kutekeleza miradi mingi ya
kuzalisha umeme iliyopo Kinyerezi – Dar es Salaam, Somanga Fungu
(Kilwa), Mchuchuma-Liganga (MW 600), Nyakato, Mwanza (MW 60), lengo
likiwa ni kufikia uzalishaji wa umeme wa MW 3,000 ifikapo mwaka
2015/16,” alisema.
Vipaumbele vyake
Pia, alisema walibuni mradi wa kuunganisha mikoa yote kwenye
Gridi ya Taifa kupitia miradi ya North-West Grid (kutokea Shinyanga,
Geita, Kigoma, Katavi, Rukwa hadi Mbeya), Makambako- Songea na
kuimarisha huduma ya umeme kupitia North-East Grid (kutokea Dar hadi
Kilimanjaro).
Alisema walianzisha kupitia Rea, utaratibu wa
kuwaunganishia wananchi umeme kwa gharama nafuu na hivi sasa
wanaunganishwa kwa Sh27,000.
“Tulisimamia ufungaji majenereta mapya ya kufua
umeme maeneo ambayo hayakuwa yameunganishwa kwenye Gridi ya Taifa… mwaka
2008 nilisimamia utungwaji wa sheria mpya ya umeme iliyoondoa
ukiritimba wa Tanesco kuhusu shughuli za uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji nchini,” alisema.
Alisema mwaka 2008 alisimamia kutungwa kwa sheria
mpya ya mafuta iliyoweka pamoja na mambo mengine, utaratibu wa kuagiza
mafuta kwa pamoja.
Pia, alisema mwaka 2009, walitunga sera mpya ya
madini, ambayo ilisababisha kutungwa Sheria ya Madini mwaka 2010 na
baadhi ya manufaa yake ni sharti la Serikali kumiliki kwa niaba ya
wananchi, hisa za bure katika migodi.
Vipaumbele vyake
Ngeleja alisema ili afanikiwe, lazima awe na
vipaumbele vichache ambavyo aliviainisha kuwa ni uchumi imara, utawala
bora, huduma za jamii na miundombinu.
Alisema akipewa ridhaa ya kuongoza nchi kipaumbele
namba moja kitakuwa ni ujenzi wa uchumi imara akisema tangu nchi ipate
uhuru bado kuna changamoto kubwa ya kuwa tegemezi.
“Nchi yetu imeendelea kuwa soko (dampo) la bidhaa
zinazotengenezwa na nchi nyingine. Mwisho wa siku tunauza nje ajira
ambazo Watanzania wangeajiriwa. Nikiteuliwa na baadaye kuchaguliwa kuwa
rais wa awamu ijayo, kazi kubwa ya kwanza itakuwa ni kurekebisha hali
hii,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment