Askari wa Bunge wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Mbunge wa
Ukonga, Marehemu Eugune Mwaiposa ulipowasili katika Viwanja vya Bunge
kwa ajili ya wabunge kutoa heshima za mwisho, Dodoma jana.
Wanasiasa
wanaojiandaa kuingia katika Uchaguzi Mkuu, wametakiwa kumuomba Mungu ili
awape nafasi hizo kwa njia sahihi kuliko kutumia ‘sangoma’. Wito huo ulitolewa jana na Mchungaji Samuel Mshana
kwa niaba ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Dayosisi ya Dodoma katika ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Eugen
Mwaiposa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga (CCM).
Mwaiposa alifariki dunia juzi akiwa usingizini kwa
kile kilichoelezwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la
damu, mwili wake ulisafirishwa jana kwa ndege ya kukodi kupelekwa Dar
es Salaam ambako utazikwa keshokutwa nyumbani kwake Kipunguni, Dar es
Salaam.
Ilikuwa ni siku ya huzuni jana, wakati wa ibada
iliyofanyika kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma, iliyohudhuriwa na
umati wa waobelezaji wakiwamo wabunge, wafanyakazi, viongozi wa mkoa na
Taifa akiwamo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Katika Bunge la kumi, huyu ni mbunge wa saba kufariki dunia. Akihutubia kwenye ibada hiyo, Mchungaji Mshana
alisema ni wakati wa kuangalia namna watu wanavyopaswa kutafuta madaraka
kupitia njia zisizofaa.
Serikali katika ibada hiyo iliwakilishwa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Jenister Mhagama, ambaye
alisema hadi Mwaiposa kabla ya kukutwa na umauti alionekana mwenye afya
njema na aliomba kuchangia katika hotuba ya Wizara ya Afya. Mhagama
alisema, Serikali na Chama cha Mapinduzi vimepoteza mtu mahiri ambaye
pengo lake halitazibika na kutoa rambirambi ya Sh5 milioni.
Akiwakilisha Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu
alisema kuwa mbunge huyo alikuwa kipenzi cha kila mmoja na wakati wote
walipenda kumuita ‘Dear’ kuonyesha kuwa alikuwa anapendwa.
Mwili wa marehemu uliwasili Dar es Salaam jana saa
9:32 alasiri, huku ndugu, jamaa na viongozi wa kada mbalimbali
wakijumuika nyumbani kwake Kipunguni. Majonzi na vilio vilitanda nyumbani kwa marehemu
Mwaiposa, huku baadhi ya viongozi akiwamo Meya wa Ilala, Jerry Silaa
akielezea kusikitishwa kwake na kifo hicho. Mwili huo ulienda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo huku taratibu za mazishi zikiendelea.
Wakati huohuo Rais Jakaya Kikwete ameelezea masikitiko yake kutokana na kifo cha Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Eugen Mwaiposa.
CHANZO: MWANANCHI
Katika salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, Rais Kikwete alisema: “Nimepokea kwa
mshtuko na masikitiko taarifa za kifo cha Mbunge Mwaiposa ambaye
nimejulishwa ameaga dunia mjini Dodoma ambako alikuwa anaendelea
kuhudhuria vikao vya Bunge.”
Pia, Rais Kikwete ambaye kwa sasa yuko nchini Finland, alitoa pole kwa familia kwa kuondokewa na mama na mchangiaji mkubwa katika maisha yao.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment