Makamu wa Rais, Dk Mohammed Ghalib Bilali akionyesha begi lenye 
fomu za kuomba kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia 
chama cha CCM baada ya kukabidhiwa makao makuu ya chama hicho mjini 
Dodoma jana.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu ya kuomba 
kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo, Dk Bilal alisema 
Serikali yake haitavumilia uvunjwaji wa miiko ya uongozi.
Huku akisisitiza kuwa kaulimbiu yake, ni 
mabadiliko ndani ya umoja, Dk Bilal alisema vipaumbele vyake ni 
kusimamia matumizi mazuri ya rasilimali za Taifa na kuboresha na 
kusimamia matumizi ya mapato. Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kulinda
 haki za binadamu na kuhakikisha nchi inasimamiwa kwa misingi ya sheria. “Nitahakikisha Serikali ya Awamu ya Tano 
inaendelea, kusimamia na kuimarisha utawala wa sheria, haki za binadamu,
 haki za kina mama na watoto, walemavu hasa wa ngozi, haki ya kuunda na 
pamoja na uhuru wa kupata habari.”
Dk Bilal alisema atahakikisha analinda misingi ya 
utaifa ulioasisiwa na wazee na ambayo imelifikisha Taifa katika miaka 54
 likiwa moja, imara, lenye upendo na mshikamano.
Alipotakiwa kuwatoa hofu watu wanaodhani kuwa ana 
mitazamo ya kihafidhina, Dk Bilal alisema yeye ni mwanasayansi na siku 
zote sayansi inabadilika kulingana na mazingira. “Hakuna uamuzi uliokuwa sahihi zaidi ya uamuzi wa 
kisayansi. Mimi siku zote uamuzi wangu unafuata utaratibu huo, ndivyo 
nilivyolelewa na kufunzwa na nitaendelea kuongozwa kisayansi,” alisema.
Akijibu swali lililomtaka afafanue mtazamo wa watu
 kwamba sasa ni zamu ya Zanzibar kutoa Rais, Dk Bilal alisema chama 
chake hakina vitu hivyo, bali kinachagua kiongozi au mwanachama ambaye 
ataweza kuwavusha. “Hatujali wapi ametoka, hatujali rangi yake, 
hatujali kabila lake, hatujali dini yake ilimradi ni Mtanzania. Mimi 
ninadhani ninaweza kulivusha Taifa hili,” alisema.
Alisema amejitokeza kwa sababu anayo hamu na uwezo wa kulifikisha Taifa liwe la kutiliwa mfano.
Alisema Muungano ulivyo hivi sasa si kama hapo 
zamani, sasa unakabiliwa na changamoto nyingi zaidi kwa hiyo ni jukumu 
lake kuhakikisha kuwa anashirikiana na wadau mbalimbali ili kutatua 
changamoto zilizopo.
Hali ilivyokuwa
Kabla ya kuingia ndani ya ukumbi, wakati na baada ya kuzungumzia
 na waandishi wa habari, Dk Bilal alikuwa akishangiliwa na wapambe wake 
kila mara alipojibu swali la mwandishi au kumaliza hatua moja kwenda 
nyingine. Mbali na kushangiliwa wakati anaingia baadhi ya 
wapambe walijipanga nje ya mlango wa kuingilia jengo la makao makuu kwa 
ajili ya kumlaki.
Alisindikizwa kwa nyimbo za hamasa za CCM na za 
kumpongeza. Wapambe hao na baadhi ya watumishi wa ofisi za makao makuu 
ya chama walikuwa wamevalia mavazi yenye rangi za chama.
Baadhi ya nyimbo zilizosindikizwa na makofi ni pamoja ‘Dk Bilal tutamlinda na kumtetea’.
Dk Bilal ni nani?
Alizaliwa Februari 9, 1945 na kuhitimu Shule ya 
Msingi Makunduchi mwaka 1958. Aliendelea na masomo ya sekondari katika 
Shule ya Beit-el-Ras mwaka 1962 na baadaye Lumumba zote za visiwani 
Zanzibar.
Kabla ya kuhitimu kidato cha tano, alipata 
ufadhili wa kwenda kusoma Marekani katika Chuo Kikuu cha Howard na 
kuhitimu Shahada ya Fizikia na Hesabu mwaka 1967.
Dk Bilal aliendelea na masomo ya Shahada ya 
Uzamili ya Fizikia na kuhitimu mwaka 1969, kisha alianza kufanya kazi 
akiwa mhadhiri msaidizi na baadaye kuwa mtafiti msaidizi katika Kampasi 
ya Berkely katika Chuo Kikuu cha Carlifonia.
Mwaka 1976, alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD), 
ya Fizikia chuoni hapo. Baadaye, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es 
Salaam (UDSM) akiwa mhadhiri na mwaka 1983 alipandishwa cheo hadi kuwa 
Mkuu wa Idara ya Fizikia ya Nyuklia.
Dk Bilal alishiriki katika ukuzaji wa sekta ya 
nyuklia nchini kwa kuwa mmoja wa walioanzisha taasisi ya Serikali 
inayoshughulikia masuala ya mionzi na mwaka 1988 aliteuliwa kuwa Mkuu wa
 Kitivo cha Sayansi cha UDSM.
Mwaka 1990 alipandishwa cheo na kuwa Katibu Mkuu 
katika Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Safari ya kisiasa 
ya kada huyo wa CCM ilianza mwaka 1995 alipoteuliwa kuwa Waziri Kiongozi
 katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi mwaka 2,000 aliporithiwa 
na Shamsi Vuai Nahodha.
Mwaka 2010, mwanasayansi huyo aliteuliwa na Rais 
Jakaya Kikwete kuwa Makamu wake baada ya Ali Mohammed Shein kuchaguliwa 
kuwa Rais wa SMZ.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment