Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli akionyesha begi lenye fomu za 
kuomba kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama cha 
CCM baada ya kukabidhiwa makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana. 
Kushoto ni Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Dk Mahammed Seif Khatibu.
Tofauti na makada wengine wa CCM ambao walianza 
kwa kutangaza nia kisha baada ya kuchukua fomu kuzungumza na waandishi 
wa habari, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, jana alichukua fomu 
kimyakimya bila kutaka kuzungumza lolote.
                
              
Badala yake akasema atatafuta muda muafaka wa kuzungumza na vyombo vya habari baada ya kusoma fomu alizopewa na chama chake.
Hata hivyo, kwa kifupi kabisa alisema endapo 
atapata ridhaa ya kuiongoza nchi atatekeleza Ilani ya CCM na kuwaomba 
Watanzania wamuombee.
Dk Magufuli ambaye alikuwa amevalia suruali nyeusi
 na shati la kijani, hakuwa na mbwembwe za wapambe wengi kama ilivyokuwa
 kwa wagombea wengine.
Alisindikizwa na watu watatu akiwamo, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama na wapambe wawili walioshuka katika gari lake.
Kada huyo alichukua fomu yake saa 11.30 jioni na kisha kuondoka zake katika eneo hilo kimyakimya.
John Magufuli ni nani?
Alizaliwa Oktoba 29, 1959 huko wilayani Chato, Kagera (hivi sasa Chato ni wilaya ya Mkoa wa Geita).
Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Chato 
mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya 
Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma kidato cha kwanza na cha pili
 mwaka 1975 – 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako 
alisoma kidato cha tatu na nne mwaka 1977 – 1978.
Alisoma kidato cha tano na sita mkoani Iringa 
katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Halafu 
akarudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi 
akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii ilikuwa mwaka 
1981 – 1982.
Alipopata stashahada yake, moja kwa moja alikwenda
 kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha 
masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na 
1983.
Kisha alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 
kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983),
 kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na 
akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea 
Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati 
na alihitimu mwaka 1988.
Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha
 Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza 
masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford, 
Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma
 kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa 
maana ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa 
katika Jimbo la Chato kwa tiketi ya CCM na kushinda wakati akiwa na 
miaka 36. Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri wa Miundombinu.
Mwaka 2000 aligombea na kushinda kwa mara ya pili.
 Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Miundombinu na akakaa hapo hadi 
kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipokamilika.
Mwaka 2005 aliingia kwenye orodha ya wabunge 
waliopita bila kupingwa na Rais Jakaya Kikwete alimteua kuongoza Wizara 
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa 
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 ikiwa mara ya nne aligombea na 
alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast na 
alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea 
huyo wa Chadema. Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako
 yuko hadi hivi sasa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment