
Chama Cha Mapinduzi (CCM)
     
Makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 
wamechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chao kuwania urais huku 
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akiweka msimamo kwamba anaingia 
kwenye mbio hizo akiwa na matumaini ya kushinda na siyo kushindwa.Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na mmoja wa waandishi wa 
habari kama CCM haitampitisha je, atakuwa tayari kumuunga 
atakayeteuliwa? “Sina mpango wa kushindwa,” alisema bila kufafanua katika hadhira 
iliyokuwa imejaa waandishi na wafuasi wa CCM kwenye Makao Makuu ya chama
 hicho mjini Dodoma jana.
Mbali na Lowassa wengine waliochukua fomu jana ni Waziri Mkuu 
mstaafu, Frederick Sumaye, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, 
Balozi Ali Karume, Mfanyakazi wa CCM Idara ya Uhusiano na Siasa, Amos 
Siyatemi na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.
Orodha hiyo imefikisha makada wa CCM wanaowania urais kuwa 13. Walikwisha kuchukua fomu ni 10 hadi jana. Lowassa ambaye alikuwa mwanachama wa tano kuchukua fomu kati ya 
watangaza nia sita kwa siku ya jana, hali ilikuwa tofauti na wagombea 
wengine kutokana na umati mkubwa wa wananchi kujitokeza wakiwamo 
wanafunzi wa vyuo vya mjini Dodoma na akina mama wafugaji wa Kimasai.
Lowassa aliwasili katika viwanja vya CCM makao makuu Dodoma saa 
10:09 jioni akiwa na msafara wa magari zaidi ya manane akisindikizwa na 
baadhi ya wabunge na wenyeviti wa CCM wa mikoa. Wabunge walioonekana kumsindikiza ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, 
Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, Mbunge wa 
Kilindi, Beatrice Shelukindo, Naibu Waziri wa Kazi na Vijana, Makongoro 
Mahanga, Anna Abdallah (Viti Maalum), Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof. 
Juma Kapuya na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye.
Wenyeviti wa CCM mikoa walijitokeza kumsindikiza Lowassa ni, Mgana 
Msindai (Singida), Khamis Mgeja (Shinyanga), Onesmo Nangole (Arusha), 
Mohamed Sinaye (Mtwara). Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Lowassa alisema katika mbio za kusaka urais mwaka huu hakusudii kushindwa bali kushinda.
RUSHWA NA UFISADI
Akijibu swali kwa nini baadhi ya makada wenzake wanamhusisha na 
vitendo vya wizi na ufisafi, alisema kama kuna anayejiamini amtaje kwa 
hoja. Alisema amechoka utaratibu wa siasa za tuhuma na matusi ambazo 
haziwezi kusaidia nchi katika maendeleo na wala hazitaweza kupima 
viongozi kwa rekodi zao.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli alisema vyombo vya habari 
visaidie kuwaelimisha wananchi, maana hawezi kujibu kila mtu mambo 
ambayo hayana maana. "Nimechoka kujibu tuhuma na matusi ya nguoni na kimsingi hizi ni 
siasa za maji taka, wabaneni watu kwa rekodi zao wewe umefanya nini toka
 umekuwa kiongozi, tuulizane bila aibu anafanya nini kumtoa Mtanzania na
 kwa mipango gani na je, kuwa rekodi yake anaaminika au ni bulabula," 
alisema.
Alisema hakuna sababu ya kuchonganishwa kwani hali hiyo haiwezi 
ikasaidia kupata viongozi waliobora. Alisisitiza kinachotakiwa ni kuwa 
na mijadala itakayoleta viongozi wanaokubalika na watu.
UTEUZI WA BARAZA LA MAWAZIRI
Alipoulizwa iwapo atachaguliwa kuwa rais atawateua watu waliokaribu
 naye katika Baraza la Mawaziri, alisema hilo litajulikana atakapovuka 
daraja. Awali alieleza kuwa kama atachaguliwa, ataanza kushughulikia 
matatizo ya wafanyakazi wa CCM makao makuu ambao wanakimbiliwa na 
matatizo mengi. "Makao makuu ya CCM ndio roho ya chama, naelewa matatizo 
yanayowakabili watumishi wa chama kuhusu malipo ya mishahara midogo, 
hawakopesheki na hawalipwi  fedha za likizo.
Alisema Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi nzuri sana kukiimarisha 
chama na kwamba kinachotakiwa sasa ni kukiimarisha kiuchumi ili kisiwe 
ombaomba. "Kama chama kitanipa ridhaa ya kuwa rais nitashughulikia matatizo 
ya watumishi kwani bila CCM madhubuti na bila viongozi wazuri CCM 
itayumba," alisema.
MATESO KWA WANANACHI
Akizungumzia kuhusu mateso wanayofanyiwa wananchi na wanahabari, 
alitoa pole kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kinanda, na 
kwamba vitendo wanavyofanyiwa wananchi siyo demokrasia. "Nalaani vitendo hivyo na serikali yangu haitakuwa tayari kuingilia uhuru wa mtu," alisema .
MAGUFULI AINGIA MITINI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI
Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli alifunga dimba kwa kuchukua fomu, 
lakini aliingia mitini kuzungumza na waandishi waliokuwa wakimsubiri 
katika ukumbi wa CCM makao makuu. Wakati waandishi wakimsubiri ukumbini kwa zaidi ya nusu saa ghafla 
ofisa habari wa CCM makao makuu, alifika na kuwaeleza kuwa Dk Magufuli 
ameshachukua fomu na kuondoka zake.
AMOS SIYANTEMI; NITAFILISI WALA RUSHWA
Naye Amos Siyantemi wa CCM ambaye ni mtumishi wa chama amechukua 
fomu na kusema kuwa amefikia uamuzi wa kugombea nafsi hiyo ili kurudisha
 imani ya chama kwa wananchi na kwamba akichaguliwa atahakikisha 
anawafilisi wala rushwa. "Vitendo vya rushwa katika chaguzi mbalimbali kunaweza kukiangamiza
 chama, hivyo atahakikisha kuwa wote watakaotuhumiwa na rushwa 
watafilisiwa mali zao," alisema Siyantemi.
Alisema atahakikisha anarejesha misingi ya azimio la Arusha la ujamaa na kujitegemea. Kada huyo alisema suala la huduma za jamii ikiwamo afya atalipa 
kipaumbele kikubwa ikiwamo kuhakikisha kuwa badala ya kuwapeleka 
wagonjwa nje ya nchi kutibiwa atawaleta wataalam hao hapa nchini ili 
kupunguza gharama za serikali.
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye alisema atahakikisha 
anakomesha suala la wafanyakazi wa umma kuwa wafanyabiashara na kuahidi 
kuunda vyombo viwili vya kupambana na rushwa. Alivitaja vyombo hivyo kuwa ni chombo cha uchunguzi na mahakama maalum kwa watuhumiwa wote wa rushwa. "Kila kiongozi au mfanyakazi wa umma lazima achague kati ya biashara au kufanyakazi,” alisema.
Sumaye alisema hataki kuwa na vipaumbele vingi bali atakuwa navyo vichache ikiwamo vya kupambana na rushwa. "Ikiwa nitapata ridhaa ya chama changu sitakuwa na mchezo katika 
kupambana na rushwa kwani matatizo mengi ambayo yapo dawa ni uchumi tu, 
hakuna mtambo wa uzalishaji wa kuboresha elimu, huduma za afya na 
mengineyo, lakini mtambo wa yote hayo ni kuwa na uchumi imara," alisema 
Sumaye
DK.BILAL
Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, amesema nia na madhumuni 
ya kujitokeza kuchukua fomu ya kuwania urais ni kusaidia kuiletea nchi 
mabadiliko zaidi. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Dk.
 Bilal alisema hatua hiyo ameitumia kama ni haki yake kidemokrasia kama 
mwanachama na Mtanzania ambaye anaamini ana uwezo wa kulisaidia Taifa 
kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
"Nia na madhumuni ni kukipa uimara zaidi chama chetu maana bila ya 
kuitikia wito kwa kila mwenye nia na uwezo wa kujitokeza basi 
nisingekuwa nimekitendea haki chama chetu," alisema Dk.Bilal
VIPAUMBELE KATIKA AWAMU YA TANO
Dk. Bilal alisema endapo atapata ridhaa ataendeleza pale walipomalizia wenzake bila kupoteza mwelekeo. "Hivyo ili Taifa letu lizidi kuendelea kutumia fursa ambazo 
kiongozi wetu Dk. Kikwete ameanzisha kwa kushirikiana nasi naomba 
niungwe mkono ili niweze kupeperusha bendera ya chama, kupitia sera, 
malengo na ilani ya CCM na vipaumbele vikuu," alisema Bilal.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kulinda misingi ya utaifa na 
kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa imara, lenye upendo na mshikamano. Alisema atahakikisha anaimarisha umoja, utaifa, uhuru, ulinzi na usalama wa Taifa ili kunusuru Muungano.
"Muungano siyo kama ulivyo kuwa zamani, sasa unakabiliwa na 
changamoto nyingi zaidi, kwa hivyo ni jukumu langu kuhakikisha 
nitashirikisha wadau mbalimbali ili kutatua changamoto hizi na 
tutaimarisha muungano wetu," alisema.
Kuhusu uchumi, Dk. Bilal alisema atahakikisha anashirikisha 
wananchi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kukuza sekta ya viwanda, 
ujasiriamali na teknolojia, sekta binafsi ambayo ni shirikishi, kilimo, 
ushirika na ugatuzi wa madaraka kwa wananchi.
Alisema madaraka yatagatuliwa katika ngazi za vijiji na vitongoji, 
na pia kuendeleza kuzalisha ajira mbalimbali ili kuhakikisha wanaboresha
 maisha ya Watanzania wote na iwe Tanzania shindani katika kanda, Afrika
 na Dunia kwa ujumla. Aidha alisema katika matumizi ya rasilimali za Taifa atahakikisha 
anasimamia vyanzo vya mapato na kuhakikisha yanatumika ipasavyo kuleta 
maendeleo kwa Watanzania.
MIIKO NA MAADILI YA VIONGOZI
Dk. Bilal alisema atahakikisha anarejesha na kusimamia maadili na 
miiko ya uongozi pamoja na utumishi wa umma kutokana na nchi kupoteza 
maadili, hivyo atasimamia taasisi za umma na uwajibikaji wa mtu mmoja.
Alisema atalinda haki za binadamu ikiwa ni pamoja na utawala bora na kuhakikisha nchi inasimamiwa kwa misingi ya sheria. "Awamu ya tano inaendelea kusimamia na kuimarisha utawala wa 
sheria, haki za binadamu, haki za kina mama na watoto na walemavu hasa 
wa ngozi, haki ya kuunda asasi za kiraia pamoja na uhuru wa kupata 
habari," alisema Dk. Bilal
BALOZI KARUME
Alisema mtu ambaye siyo mwadilifu asikabidhiwe nchi kwani itakuwa ni hatari kwa nchi.
MUHONGO, SITTA, KAMANI ZAMU YAO LEO
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya 
Mifugo, Dk Titus Kamani na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais Prof. Sospeter 
Muhongo watachukua fomu leo.
     CHANZO:
     NIPASHE
    

No comments:
Post a Comment