Social Icons

Pages

Thursday, June 04, 2015

SITTA: NITATENGANISHA SIASA, BIASHARA


Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, amekuwa kada wa tisa kutangaza nia ya kuomba Chama Cha Mapinduzi, kumpa ridhaa ya kupeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, Oktoba, mwaka huu.
Sitta alitangaza nia jana katika kijiji cha Itetemia mkoani Tabora, makao makuu ya  mashujaa wa Unyanyembe, walikotawala watemi Isike na Kiyungi  walioendesha harakati  dhidi ya dhuluma na unyanyasaji wa wakoloni.
Alisema iwapo atapewa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho, atahakikisha anatenganisha masuala ya siasa na biashara kwa sababu ‘ishu’ hizo mbili ni chanzo kikubwa cha kuwapo rushwa kubwa na kusainiwa mikataba mibovu. “Nina ari, uwezo na utayari wa kuimarisha nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema. 

RUSHWA
Waziri Sitta aliainisha baadhi ya vipaumbele atakavyosimamia kuwa ni pamoja na kupambana kwa nguvu zote na rushwa kwa kutenganishe siasa na biashara. Alisema rushwa kubwa zimekuwa na athari mbaya kwa uchumi wa nchi na kusababisha kuwapo na mikataba mibovu ya huduma na mauzo, manunuzi hewa, manunuzi yaliyojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni kwa rushwa na rushwa katika ajira ambavyo vimesababisha hasara ya trilioni za fedha kwa taifa.
"Uchumi unakosa afya kutokana na kubanwa na rushwa ambayo sasa imeenea mijini na vijijini...hatua ya kwanza hatuna budi kutenganisha biashara na uongozi, hivyo mtu achague kushiriki kwenye biashara ama siasa,” alibainisha Sitta.
Aliongeza kuwa kwa sasa baadhi ya wanasiasa na watumishi waandamizi serikalini wanatumia nafasi zao kujitajirisha kwa kujipendelea, jambo ambalo ni hatari wanasababisha kuchochea rushwa na usumbufu kwa wananchi, kupunguza ari ya wafanyabiashara wa dhati na kudumaza uwekezaji.
Alitaja hatua nyingine katika kukabiliana na rushwa ni kutunga sheria mpya zilizo kali na zitakazokuwa na matokeo ya kumzuia mtu asitamani kusaka rushwa, mali za viongozi zitamkwe kwa uwazi, mali isiyolingana na kipato na kukosa maelezo ya kutosheleza kutaifishwa, kesi za rushwa ziwe na utaratibu wenye uwazi na tume inayoshughulikia maadili ya viongozi ipewe nguvu kubwa za uchunguzi na ufatiliaji wa mali za viongozi bila kuzuiwa na mamlaka yoyote.
"Sambamba na kupiga vita rushwa, hatuna budi kuchukua hatua kali dhidi ya hujuma za uporaji wa maliasili za nchi na rasilimali zake…madini, misitu, vyanzo vya maji, bahari, maziwa na mito ni rasilimali zisipotunzwa zitatishia uendelevu wa uchumi kwa vizazi vijavyo, hivyo uhalifu dhidi ya maliasili na rasilimali za nchi itabidi iwekwe sheria na taratibu kali," alisema. 
 
MUUNGANO
Sitta ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, alisema atahakikisha anaimairisha Mungano kutokana na kuonekana kuna mwelekeo wa mifarakano, mshikamano hafifu kuwapo na chokochoko za siasa za ushindani, udini na kupanuka kwa tofauti ya kipato na vijana wengi wasio na ajira.
Kutokana na hali hiyo, Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la tisa, alisema atatumia mchanganyiko wa uzoefu wa uongozi kutanzua changamoto hizo zikiwamo za Muungano. Alisema kwa sasa zinajitokeza kauli na vitendo ambavyo vinaashiria kutaka nchi mbili zilizoungana zitengane, wapo wanaodai Zanzibar itanufaika iwapo itabaki huru bila muungano, na Bara nao wanawatazama Wazanzibar ni wakorofi wasioridhika na chochote kinachofanywa na serikali ya Muungano.
Alisema ili kuziweka nchi hizo mbili ni kudumisha Muungano na kuuokoa hivyo kiongozi anayeweza kuzileta pamoja kambi hizi na kuuokoa muungano pekee. “Ushiriki wangu katika serikali yetu tangu awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu, unaniweka katika nafasi nzuri ya kuongoza mchakato utakaowezesha kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano,” alisema. 
 
KATIBA
Kingine ni Katiba na kwamba licha ya muafaka kamili kuhusu Katiba mpya kutofikiwa, lakini ile iliyopendekezwa ina maeneo mengi ya msingi ambayo yanaweza kuleta ukaribu ikiwa ni hatua ya awali inayowezesha kusonga mbele kwa amani.
"Naamini pande zinazosigana kuhusu Katiba zina wazalendo ambao wanaweza kukubaliana kuwa na kipindi cha mpito cha utulivu na maelewano kitakachotuwezesha kama taifa kusonga mbele, viongozi wa kisiasa na wa jamii washawishike kukubali hoja mbili, hakuna mshindi wala mshindwa katika kufikia kukubalika kwa Katiba ya taifa letu na katiba yoyote ni waraka unaoenda unabadilika kulingana na mahitaji ya wakati husika,” alisema. 
 
UCHUMI
Sitta alisema jambo jingine ambalo atalipa kipaumbele ni kujenga mfumo wenye motisha kwa wote, ili kuchochea uchumi endelevu na wa viwanda ili kukuza uchumi wa nchi kwa kasi inayopunguza umaskini kwa haraka.
"Tukijenga uwezo mkubwa zaidi wa bajeti ya serikali kutosheleza ubora wa  huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji, hatuna budi kufanya jitihada za makusudi za kuubadili mfumo wa uendeshaji nchi uwe ni wa motisha kwa wazalishamali, mifumo ya nchi zilizopiga hatua kubwa za maendeleo duniani ni ile iliyoweka mazingira chanya ya kuaminiana baina ya serikali na sekta binafsi lakini kwetu haijatimia,” alisema.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara wakubwa wa ndani hawawekezi vya kutosha ndani ya nchi ili kuleta maendeleo ya haraka ya huduma, viwanda, kilimo na biashara na baadhi yao baada ya kuchuma pesa wanazihamishia nje ya nchi huku watendaji serikalini wakiwatazama wafanyabiashara ambao hawana uzalendo na wakwepa kodi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: