Jaji Damian Lubuva
Tanzania tuliamua kuandikisha upya wapigakura
katika Daftari la Kudumu baada ya kujiridhisha kuwa tulilonalo halifai.
Kutokana na ukweli huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Jaji Damian Lubuva aliweka bayana kuwa hataendesha uchaguzi wowote kabla
ya uandikishaji kumalizika.
Awali, ilitarajiwa kwamba uandikishaji huo
ungekamilika kabla ya Aprili 30, siku iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya
upigaji wa Kura ya Maoni lakini mashine za uandikishaji za BVR
zilichelewa na kusababisha mchakato huo kusuasua.
Hivi sasa Tume iko katika maandalizi ya Uchaguzi
Mkuu na tayari imeshasema utafanyika Oktoba 25. Kama ilivyo kwa Kura ya
Maoni, Uchaguzi Mkuu nao utategemea kukamilika kwa uandikishaji huo.
Makadirio yanasema kuwa wanaotarajiwa kuandikishwa
ni watu 24 milioni. Kwa siku 96 kuanzia Februari 24 hadi Mei 31,
wameandikishwa watu milioni sita tu na kwa mujibu wa ratiba ya Tume
uandikishaji unapaswa kukamilika Julai 18, hivyo ndiyo kusema kuwa
zimesalia siku 44 tu kuandikisha watu zaidi ya milioni 18.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu la Taifa (NBS),
inakadiriwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una wapigakura wapatao milioni
2.9. Hao wanatarajiwa kuandikishwa katika Daftari kwa siku 12 tu kuanzia
Julai 4 hadi 16. Sababu inayotolewa na NEC ni kuwa eti mashine zote
8,000 za BVR kwa wakati huo zitakuwa Dar es Salaam jambo ambalo halina
uhalisia kwani wakati huo ndipo mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga
itakuwa inaendelea na uandikishaji.
Takwimu za NBS zinakadiria kuwa Morogoro ina watu
wanaostahili kupiga kura wapatao 1.28 milioni wakati Tanga ina
wapigakura wapatao 1.12 milioni. Hao wote kwa ujumla wao ni sawa na watu
milioni 2.4 idadi ambayo ni ndogo kuliko ya wapigakura wa Mkoa wa Dar
es Salaam, lakini huko wamepewa mwezi mzima wa uandikishaji.
Kwa mtiririko huo wa mambo, hatuoni jinsi ambavyo
NEC itakamilisha uandikishaji kabla ya Uchaguzi Mkuu. Hofu hiyo wanayo
Watanzania wengi, lakini kama kawaida Tume imekuwa bingwa wa kuweka nta
masikioni.
Tunaitaka iongeze kasi ya uandikishaji ili kuwapa
matumaini Watanzania hasa kwa sababu uzoefu unatuonyesha kuwa katika
maeneo ambayo tayari uandikishaji umekamilika ilibidi ziongezwe siku kwa
sababu wapigakura waliojitokeza ni zaidi ya makadirio.
Hivyo, kwa makadirio yasiyo rasmi yawezekana
wapigakura wakawa zaidi ya milioni 27. Kama hivyo ndivyo, NEC inabidi
ijipange upya na iweke nguvu zaidi kukabiliana na changamoto hiyo,
kinyume chake kuandikisha watu zaidi ya milioni 20 kwa siku 44
zilizosalia ni ndoto. Hata kama ikibadili ratiba na kusema itaandikisha
mpaka Oktoba 24 bado siku hizo hazitoshi kutokana na mwenendo wenyewe wa
uandikishaji unavyoendelea.
Hadi sasa bado malalamiko ya misururu mirefu
katika vituo vya uandikishaji yanaendelea sambamba na waandikishaji
kuchukua zaidi ya nusu saa kuandikisha mtu mmoja, hali hiyo
inadhihirisha kuwa tumefanya makosa kufanya jambo kubwa kama hili la
uandikishaji upya wapigakura mwaka wa uchaguzi.
Mambo yamekuwa mengi, tumejizonga na kuzongeka na
sasa joto la wasiwasi linazidi kupanda. Ndiyo maana tunasema tunapaswa
kutafuta mpango B mapema kabla hatujaenda mrama.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment