Social Icons

Pages

Thursday, June 04, 2015

SITTA: MAMBO MATANO KWA TAIFA

Mtemi Msagata Fundikira akiwa amemshika Margareth Sitta ambaye ni mke wa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (kushoto)  kwa ajili ya kuwapa  baraka ya na kuwapandisha cheo kuwa Mjukuu wa Mkubwa wa Unyanyembe, kabla  ya Waziri huyo kutangaza nia ya kugombea Urais, kwenye viwanja ya Ikulu ya Itetemya Tabora jana.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akieleza kuwa anataka kulifanyia Taifa mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kusimamia Muungano, kukamilisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya, kuweka mfumo wenye motisha kwa wote ili kuchochea uchumi endelevu na wa viwanda, vita dhidi ya rushwa na kukiimarisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kiuchumi.
Sitta alitangaza nia hiyo jana kwenye Ikulu ya Wanyanyembe iliyopo Itetemia, takriban kilomita saba kutoka mjini Tabora. “Ili kukomesha tatizo hilo (la rushwa), hatuna budi kutunga sheria itakayotenganisha biashara na uongozi,” Sitta alisema akiungana na Rais Jakaya Kikwete ambaye pia aliwahi kuahidi kutenganisha siasa na biashara lakini hadi sasa bado hajatunga sheria hiyo.
“Mtu achague moja, biashara au uongozi wa siasa. Ikiwa mfanyabiashara atataka kuingia katika uongozi wa siasa itabidi akabidhi mali na biashara zake kwa mdhamini atakayeziendesha wakati mhusika anatumikia umma,” alisema Spika huyo wa Bunge la Tisa.
Alisema mikataba mibovu ya huduma na mauzo, ununuzi hewa, ununuzi uliojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni kwa rushwa na hasa rushwa katika ajira, imelisababisha Taifa hasara kubwa.
Alisema hatua ya pili ya kupambana na rushwa ni kutunga sheria mpya zilizo kali na ambazo zitakuwa na matokeo ya kumzuia mtu asitamani kusaka rushwa. “Katika hilo tutahakikisha mali za viongozi zinatajwa kwa uwazi. Mali isiyolingana na kipato na kukosa maelezo ya kutosheleza itaifishwe, kesi za rushwa ziwe na utaratibu wenye uwazi,” alisema mbunge huyo wa Urambo Mashariki.
“Tume inayoshughulikia maadili ya viongozi ipewe nguvu kubwa za uchunguzi na ufuatiliaji wa mali za viongozi bila kuzuiliwa na mamlaka yoyote. Pia Tume ifanye kazi zake kwa kuyaweka mambo wazi kuhusu watuhumiwa, tuhuma zao, majibu yao na hatua zinazofuatia. Vikao vya tume vya kusikiliza mashauri ya maadili viwe vya wazi kwa wananchi.”
Alisema adhabu ya utoaji na wapokeaji rushwa itakuwa kali na iambatane na mali zitakazothibitika kupatikana kwa rushwa, zitataifishwa.
“Ikumbukwe kwamba, kiongozi tutakayemuamini kupambana na rushwa hana budi awe na historia ya uadilifu wa muda mrefu kama nilivyo,” alisema Sitta.
Sambamba na kupiga vita rushwa, alisema watachukua hatua kali dhidi ya hujuma za uporaji wa maliasili za nchi na rasilimali zake. “Madini, misitu, vyanzo vya maji, bahari, maziwa na mito ni rasilimali ambazo zisipotunzwa zitatishia uendelevu wa uchumi kwa vizazi vijavyo. Kwa hivyo uhalifu dhidi ya maliasili na rasilimali za nchi itabidi uwekewe sheria na taratibu kali,” alisisitiza Sitta.
Alisema mazingira ya rushwa pia yataangaliwa pamoja na kuimarisha utawala bora. Tabia za watendaji serikalini kusimamia taratibu zenye usumbufu kwa wananchi inazifanya huduma za jamii zipatikane kwa tabu kubwa. “Tabia za njoo kesho na wananchi kuzungushwa zungushwa wanapofuatilia haki zao itabidi zikomeshwe, zikemewe na ziwe kigezo cha kuwapima watumishi,”alisema.
Akizungumzia uamuzi wake wa kutangaza kugombea urais, Sitta alisema: “Kugombea nafasi ya urais wa nchi yetu si jambo jepesi. Linahitaji fikra ya kina ukizingatia kuwa nafasi hiyo ya uongozi inabeba matumaini ya Watanzania milioni 47. “Naamini kuwa kipindi cha uongozi cha 2015-2020 ni kipindi chenye changamoto nzito za kitaifa ambazo zinahitaji aina ya uongozi wenye uimara, uadilifu, uzalendo na maarifa thabiti ili kuivusha nchi kwa usalama. alisema.
Sitta, ambaye anajulikana kama ‘Mzee wa Viwango’ kutokana na kaulimbiu aliyoitumia wakati akiongoza Bunge la Tisa ya “Kasi na Viwango”, alisema mgombea yeyote makini wa nafasi ya urais, hana budi kuyapima mazingira ya Taifa katika miaka mitano ijayo na kuzielewa changamoto zitakazokuwapo katika kipindi cha uongozi anachokusudia kuongoza.
“Kipindi cha miaka mitano ijayo kina mwelekeo wa mifarakano katika masuala ya Muungano wetu, kutetereka kwa mshikamano wetu kunakotokana na chokochoko za siasa za ushindani, udini na kupanuka kwa tofauti ya kipato, ongezeko la kundi kubwa hususan la vijana mijini lisilo na uhakika wa ajira na haya yote yanaashiria ongezeko la uhalifu,” alisema.
Sitta, ambaye alianza kuteuliwa kuwa waziri miaka ya sabini, alisema anaamini ana mchanganyiko wa uzoefu wa uongozi unaomuwezesha kukusanya nguvu chanya za Watanzania ili kuyatatua matatizo hayo. Ninaweza kufanya hayo yote kwa kuwa nimeitumikia Serikali katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa zaidi ya miaka 30. “Kwa kifupi ninao uelewa na uzoefu unaolingana na changamoto za kipindi kigumu cha miaka mitano ijayo yenye mwelekeo wa kutikisa misingi ya utawala wa nchi yetu… kwa uimara wangu wa uongozi, nitajumuisha nguvu na maarifa ya wananchi ili tuvuke salama na pia tutekeleze kazi za maendeleo kwa ufanisi na tija zaidi,” alisema Sitta.

Mambo anayosimamia
Sitta alisema katika vipaumbele vyake atakavyosimamia akipitishwa na CCM na baadaye kushinda kwenye Uchaguzi Mkuu, atahakikisha Muungano unaimarishwa licha ya kuwa na viashiria vya kutaka uvunjwe.
“Pande zote mbili za Muungano zinatoa kauli na vitendo ambavyo vinaashiria kutaka nchi zetu mbili zilizoungana zitengane. Zanzibar, tunashuhudia wanasiasa wanaodai kuwa nchi hiyo itanufaika zaidi ikirejea kuwa na uhuru kamili bila kuwa sehemu ya Muungano,” alisema na kuongeza:
“Baadhi ya watu wa Tanzania Bara wanawaona ndugu zao wa Zanzibar kuwa ni wakorofi na wasioridhika na chochote kitakachofanywa na Muungano, wanahisi kuwa mfumo wa huu unapendelea upande mmoja.”
Alisema hakuna shaka kwamba pande mbili za Muungano zikitengana kutazuka uhasama na matokeo yake ni kuvunjika kwa amani.
Alisema ushiriki wake katika Serikali tangu awamu ya kwanza ya uongozi, unamuweka katika nafasi nzuri ya kuongoza mchakato utakaowezesha kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano.

Aufagilia mchakato wa Katiba
Sitta, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema pamoja na kuwa muafaka kamili kuhusu Katiba Mpya haujapatikana, Katiba Inayopendekezwa ina maeneo mengi ya msingi ambayo yanaweza kuwaleta karibu Watanzania.
“Hakuna mshindi wala mshindwa katika kufikia muafaka wa kukubalika kwa Katiba ya Taifa letu. Katiba yoyote ni waraka unaobadilika kulingana na mahitaji ya wakati husika,” alisema na kubainisha kuwa hakuna Katiba duniani ya kumridhisha kila mmoja lakini kadri muda unavyokwenda, inaweza kuboreshwa kwa kuzingatia maoni ya wengi.

Uchumi endelevu
Sitta, ambaye pia amewahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji kwa miaka tisa, alisema ili kukuza uchumi wa nchi, lazima jitihada za makusudi zifanyike kuubadili mfumo wa uendeshaji nchi, ili uwe na motisha kwa wazalishaji.
Alisema mfumo huo utasaidia kujenga uwezo mkubwa zaidi wa bajeti ya Serikali, utakaotosheleza katika utoaji wa huduma bora kwa jamii kama vile afya, elimu na maji.
“Mifumo ya nchi zilizopiga hatua kubwa za maendeleo duniani ni ile iliyoweka mazingira chanya ya kuaminiana baina ya Serikali na sekta binafsi. Hali hii haijatimia hapa kwetu,” alisema Sitta.
Aliishukuru Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete akieleza kuwa imefanya kazi kubwa ya kutandaza miundombinu, hususan barabara, mawasiliano na nishati.
“Sasa wakati umefika wa ushirikiano na kuaminiana baina ya sekta binafsi na Serikali ili kuzifungua rasilimali za nchi zirutubishe uchumi kwa faida ya wote,” alisema.
“Mazingira ya Serikali na sekta binafsi kufanya kazi kama timu moja yatafungua fursa nyingi za uchumi na hivyo kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.”

Kuimarisha CCM kiuchumi
Sitta ambaye amewahi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM 2005-2010, alisema: “Chama tawala madhubuti ni nyenzo muhimu sana katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata kwa ufanisi, huduma zote zilizoahidiwa kwenye ilani.
“Katika hili, ni wajibu wa mwenyekiti wa chama kuhakikisha kwamba vitengo na vitegauchumi vya chama vinakuwa na tija inayokiwezesha kuendesha shughuli zake kwa kujitegemea.
“Chama tawala kilicho imara kiuchumi kitakuwa na watendaji wanaofanya kazi zao kwa kujiamini na hivyo kuisimamia Serikali yake itimize wajibu wake kwa wananchi.
“Chama imara kiuchumi kitakuwa na ufanisi zaidi katika kuendesha shughuli zake bila kujidhalilisha kwa kuomba misaada kutoka kwa matajiri. Mfumo mzima wa chama unaozingatia nyenzo kamili na masilahi endelevu kwa watumishi wake ni msingi bora wa kuendesha masuala ya nchi kwa uadilifu.
“Nikibahatika kuchaguliwa katika nafasi ya rais na kukiongoza chama, nitatumia uzoefu wangu wa miaka tisa na nusu katika kukiongoza Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuziunganisha shughuli za uchumi za chama na wawekezaji makini ili kupunguza utegemezi wa chama kwa ruzuku ya Serikali na pia utegemezi hatari zaidi kwa matajiri wachache,” alisema.

Kwa nini alitangazia Ikulu ya Wanyanyembe?
Sitta alisema Ikulu ya Wanyanyembe ndiyo sehemu iliyokuwa makao makuu ya mashujaa wa Unyanyembe kama Isike na Kiyungi walioendesha harakati dhidi ya dhuluma na unyanyasaji wa wakoloni.
Alieleza asili ya neno Ikulu kuwa ni la Kinyamwezi lenye maana ya Itetemia ambalo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1961 alilitumia kumaanisha ‘State House’. “Neno hili maana yake ni makazi ya mkuu wa nchi ambayo hapa Tanzania yako jijini Dar es Salaam na mimi nimeamua kuanza safari yangu ya kuelekea Ikulu hapa.”
Alisema kitendo chake cha kutangazia nia ya kugombea urais akiwa Ikulu ya Wanyanyembe kinaamnisha kuienzi sehemu hiyo ambayo ina historia yenye kutukuka ya Itetemia.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: