Social Icons

Pages

Wednesday, June 03, 2015

MBUNGE UKONGA AFARIKI DUNIA

Wifi wa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga marehemu, Eugen Mwaiposa , Sauda Mwaiposa, akilia baada ya kupata taarifa za msiba nyumbani Ukonga, Dar es Salaam jana.
Mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa amefariki dunia usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake eneo la Chadulu mjini Dodoma saa chache baada ya kutoka katika kikao cha 19 cha mkutano wa 20 wa Bunge la 10.
Mbunge huyo alikuwa bungeni juzi wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na alimweleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama kuwa ataiwekea ‘ngumu’ bajeti hiyo kama asingepatiwa majibu ya kuridhisha.
Kifo cha mbunge huyo kinafanya idadi ya wabunge waliofariki dunia tangu Januari mwaka hu kufikia wawili baada ya kifo cha Kapteni John Komba aliyekuwa mbunge wa Mbinga Magharibi.
Taarifa za kifo cha Mwaiposa zilitangazwa jana saa 6:58 mchana na Naibu Spika, Job Ndugai na kusababisha wabunge kuanza kuangua vilio, huku wakieleza jinsi walivyozungumza na marehemu juzi jioni.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Sofia Simba alisema mpaka wanaachana na marehemu alikuwa akisisitiza zaidi suala la maendeleo ya wananchi wa jimbo lake na hakuonekana anaumwa.
Kikao cha jana kilikuwa kikiongozwa mwenyekiti wake Lediana Mng’ong’o na ilipofika saa 6:55 mchana alimpisha Ndugai ambaye alitangaza taarifa za kifo hicho na kusitisha shughuli za Bunge hadi kesho.
Akitangaza kifo hicho Ndugai alisema Mwaiposa alifariki dunia akiwa usingizini usiku wa kuamkia jana.
“Marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu. Hakika Bunge limepata msiba mzito. Mwili wa marehemu umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,” alisema.
“Taarifa zaidi tutazisambaza kupitia simu za mkononi mara baada ya familia ya marehemu kufika. Kamati ya Uongozi tukutane mara moja ili kujadili suala hili. Msiba uko nyumbani kwake Chadulu,” alisema Ndugai.
Alisema shughuli za kuaga mwili wa marehemu zitafanyika leo nyumbani kwake Chadulu.

Nyumbani kwake Dar
Nyumbani kwa marehemu Kipunguni jijini Dar es Salaam jamaa, majirani na watoto walikuwa kwenye hali ya majonzi, huku ndugu wakishindwa hata kuzungumza. Katibu wa Siasa na Uenezi (CCM), Wilaya ya Ilala, Said Sidde aliyekuwa nyumbani hapo, alisema juzi usiku walikuwa wakiwasiliana na alihisi kuwa anaumwa lakini alipomuuliza mbunge huyo alijibu hana tatizo lolote.

Wabunge wamlilia
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenesta Mhagama alisema, “Jana (juzi) Mwaiposa alinifuata na kuniambia kuwa muda wa kupitisha vifungu vya bajeti ya wizara ya elimu atashikilia shilingi kwa ajili ya kujijenga jimboni kwake. Mhagama alisema kilichomuuma zaidi ni tukio la Mwaiposa kumpungia mkono wakati akiondoka bungeni juzi jioni, kitendo alichotafsiri kuwa alikuwa akimuaga.
Simba alisema, “Jana (juzi) nilizungumza naye kuhusu jimbo lake la Ukonga. Tulizungumza masuala ya kugawanywa kwa majimbo na nilimpa moyo kuwa kama jimbo hilo likigawanywa atakuwa na nafasi nzuri ya kushinda. “Aliniambia hana wasiwasi katika suala hilo kwa sababu wananchi wa Ukonga wanampenda. Alinihakikishia hali yake ya kisiasa katika jimbo hilo ni nzuri,” alisema Simba.
Aliongeza, “Hakuniambia anauwa ila kuna baadhi ya watu aliwaeleza kuwa alikuwa anaumwa, aliwaambia kuwa alikuwa akiumwa akiumwa na mishipa ya shingo.”
Kwa upande wa Mbatia alisema, “Nakumbuka jana (juzi) nilipomaliza kuchangia bajeti ya elimu nilizungumza naye, aliniuliza kuhusu jinsi ya kutatua foleni za Dar es Salaam.”

Taarifa zaidi
Taarifa zilizolifia gazeti hili zinaeleza kuwa dereva wa mbunge huyo alikwenda nyumbani kwa bosi wake jana asubuhi kumchukua kwenda bungeni, alipofika eneo analoishi aligonga mlango lakini hakujibiwa.
Baada ya kuona hali hiyo alimpigia simu mume wa marehemu ambaye aliwasiliana na mbunge mmoja ambaye aliondoka bungeni akiambatana na polisi kwenda nyumbani kwake ambako walivunja mlango na kukuta amekwishafariki.

Wasifu wa marehemu
Mwaiposa alizaliwa Novemba 23, 1960 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro ambapo mpaka anakutwa na mauti alikuwa na umri wa miaka 55. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Nkweseto mwaka 1967 hadi 1974 na kujiunga na shule ya sekondari Masama mwaka 1976 hadi 1980 ambapo baadaye alipata elimu ya juu ya sekondari katika shule ya biashara ya Shinyanga (Shycom) mwaka 1981 hadi 1983, baadaye alipata shahada mbili za uzamili, moja akiipatika katika Chuo Kikuu cha Strathclyde kilichoko Glasgow, Scotland.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: