Social Icons

Pages

Wednesday, June 03, 2015

HATIHATI YA MAALIM SEIF KUSHINDA URAI ZANZIBAR

Tayari Maalim Seif Sharifu Hamadi, ameshachukua fomu ili kuomba ridhaa ya chama chake kimkubalie tena kukiwakilisha kwa mara ya tano mfululizo kugombea kiti cha urais wa Zanzibar.
Tafakuri ya Abuu Iddi leo itajikita kwenye uwezekano wa kushinda au kushindwa kwa Maalim Seif katika Uchaguzi Mkuu. Kabla ya kutafakari mazingira yaliyosababisha  Maalim Seif  kushindwa au ‘kunyimwa’ ushindi katika chaguzi zilizopita, kwanza tutafakari kwa pamoja ugumu wake wa kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kwanza, tukumbuke kwamba kura za wapinzani katika uchaguzi zitagawanyika, hasa tukizingatia kwamba aliyekuwa miongoni mwa mihimili mikuu ya CUF, Hamad Rashid atagombea nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama chake kipya cha ADC. Ni kujidanganya kwamba eti Hamad Rashid hana wafuasi wa kutosha kumuwezesha kutoa changamoto kwa wagombea wengine.
Pili, tusisahau kwamba mazingira ya chama cha CUF kwa mwaka huu katika kuomba kura za Wazanzibar yatapata uzito mkubwa kwa sababu CUF ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.
Kamwe CUF haitoweza kujinasua na ‘upungufu’ uliojitokeza katika uendeshaji wa serikali hiyo hasa ikizingatiwa kwamba baadhi ya wizara nyeti zipo chini ya mawaziri kutoka chama hicho.
Tatu, Maalim Seif atakaposimama hadharani kuomba kura za Wazanzibar kwa mara ya tano, atalazimika kuwaeleza atawafanyia nini akiwa Rais wa Zanzibar, na yeye kama Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar amewafanyia nini na ameshindwa kuwatekelezea nini akiwa kama sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Maalim Seif atakumbana na maswali magumu,  kwa sababu haiwezekani kuipongeza au kuilaumu Serikali ya Zanzibar halafu yeye pamoja na mawaziri wake kadhaa kutoka CUF wasiwemo. 
Lakini tayari pia baadhi ya Wazanzibar wameshapata wasiwasi hasa baada ya kuona mambo yakiendeshwa kinyume cha matarajio yao katika baadhi ya zile wizara zilizomo katika mikono ya mawaziri wa CUF. Maalim Seif asisahau kwamba changamoto hii itampunguzia kura zake.
Maalim Seif asisahau kwamba; unapomuahidi mtu kuwa ukipata mkate mzima yeye utamgawia nusu yake, halafu ikatokea umepata nusu yake na huyu uliyemuahidi anajua vyema hilo, matarajio yake ni kwamba atapata robo ya mkate huo, kwani kama ungepata mzima ungelimpa nusu.
Ikiwa umepata nusu na yeye hukumpa hata hiyo robo halafu hali ikawa ni ya kawaida tu, tarajia kwamba ukimya wake unabeba jambo zito moyoni mwake.
Vilevile Maalim Seif asiisahau changamoto mpya ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu iliyozalishwa na tatizo la baadhi ya wasiofahamu nguvu za mihimili mitatu ya nchi, kwamba kila mmoja mipaka yake inakomea wapi.
Wapo baadi ya Wazanzibar wanaoamini kwamba watuhumiwa walioko mahubusu katika magereza wanaweza kutolewa mara moja tu kwa amri ya viongozi wa serikali.
Wenye mtazamo huo, walitarajia wamuone Maalim Seif akilisimamia hilo hasa kwa kuzingatia kwamba baadhi ya madai ya watuhumiwa wale ni kuidai Zanzibar yenye mamlaka kamili.
Kitendo cha Maalim Seif kukaa kimya na kuendelea kubakia katika serikali ambayo ni “dhalimu” (kwa mtazamo wao) kinawapa hasira ya kumsubiri kwenye sanduku la kura wamuwajibishe.   
Changamoto nyingine itakayopunguza sana kura za Maalim Seif ni kitendo cha “kula matapishi yake”. Tayari yeye aliitambua Serikali halali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na ndio maana akakubali kukaa nayo, wakaendesha vikao vyenye mafanikio makubwa hadi kufikia mwafaka  uliozaa matunda haya ya kihistoria.
Ni vipi leo baada ya mafanikio hayo anakumbushia tena yale ‘majeraha’ yaliyopita na kutamka hadharani kwamba safari hii hatokubali tena kuporwa ushindi wake, akimaanisha kwamba hata uchaguzi uliomfanya yeye kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais aliporwa ushindi.
Aliwezaje kukaa kikao pamoja na Serikali ‘isiyo halali’ kisha akakubali yaliyoafikiwa katika kikao hicho kwa sababu tu ‘maslahi yake’ yamechungwa?
Changamoto nyingine itakayomfanya Maalim Seif ashindwe ni ukosefu wa hoja zinazokinaisha juu ya vipi atashinda, kwani yeye mwenyewe amewahakikishia Wazanzibar kwamba anashinda isipokuwa anaporwa ushindi.
Wazanzibar wanasubiri awape mchanganuo na maelezo yanayotosheleza kwamba amejipanga vipi kuzuia huo uporaji kama ni kweli huwa anaporwa, kwa sababu mfumo wa upigaji kura ni ule ule na mfumo wa ulinzi wa kura ni ule ule.
Kutokana na haya, ndiyo maana nikaonelea leo tusaidiane katika tafakuri kwamba: Je, Maalim Seif atashinda?
Kwa upande wangu, tafakuri inanipa natija kuwa hawezi kushinda, kwa sababu yeye mwenyewe anashindwa kubainisha hizo nguvu zitakazomfanya ashinde. Nihitimishe kwa kumpa nasaha hizi: Akumbuke kwamba kura ni siri tena siri kubwa.
Kwa hiyo anapojenga hoja kwamba amekuwa akishinda na atashinda tu, aseme na kubakisha, kamwe asimalize maneno, kwani umati unaojaa kwenye mikutano ya kampeni sio kielelezo halisi cha upigaji wa kura.
Amkumbuke Augustino Mrema na mikutano yake alipokuwa NCCR – Mageuzi, na pia mikutano ya kampeni ya CCM kule Pemba ilivyokuwa ikijaza watu wengi mno, lakini matokeo ya kura baadaye ni tofauti.
Namkumbusha pia juu ya ‘tabia mpya’ ya wapigakura wa Tanzania pale wanapoamua kumpa kura za kutosha mgombea wa ubunge wa chama fulani, lakini katika nafasi ya urais wakaamua kumpa kura za kutosha mgombea wa chama tofauti.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: