Social Icons

Pages

Thursday, April 23, 2015

TAKUKURU: CCM IKITAKA TUTAIONDOLEA RUSHWA

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dar es Salaam, Daniel Mtuka  
Wakati viongozi wa CCM wanaendelea kupiga kelele bila ya kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya rushwa wanavyodai vinafanywa na makada wanaotaka uongozi wa nchi, Takukuru iko tayari kukisaidia chama hicho kikongwe kupambana na uhalifu huo kama kitakuwa tayari kutoa ushirikiano.
Karibu viongozi wote wa CCM wameshanukuliwa wakilalamikia kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya chama hicho, hasa nyakati za uchaguzi, lakini wamekuwa wakieleza tu kwamba wahusika watawajibishwa na vyombo vya maadili vya chama hicho, licha ya vitendo hivyo kuwa vya uhalifu.
Juzi, akiwa kwenye vikao vya ndani na viongozi wa chama hicho wa Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangulla alisema fedha zinazotumiwa na makada kununua wanachama “kama maandazi”, zitakuwa kitanzi chao kwenye uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa wanachama hao watang’olewa.
Lakini wakati wasomi waliohojiwa na Mwananchi wanahoji sababu za chama hicho kutowashitaki makada hao kwenye chombo kinachojishughulisha na kupambana na rushwa, ofisa huyo wa Takukuru amesema inawawia vigumu wao kuwashughulikia wahalifu hao bila ya viongozi kutoa ushirikiano.
“Taasisi iko tayari hata kama viongozi au wanachama watatuletea malalamiko hayo leo (jana). Bila ushirikiano wa viongozi inakuwa vigumu kufuatilia,” alisema kamanda wa Takukuru wa Dar es Salaam, Daniel Mtuka.
“(Iwapo watatoa ushirikiano) Itakuwa rahisi kuona tunaanzia wapi, pia (kwa kuangalia) mfumo wa chama, taratibu zake, katiba na ilani yake wanafanyaje kazi,” alisema.
“Kwa kesi ya rushwa kwa wagombea hao, ni vigumu kwani tuliwahi kukutana na changamoto ya kushindwa kufanya kazi yetu miaka iliyopita tulipomnasa mgombea fulani wa ubunge CCM ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama. Sisi tulidhani ni tatizo, lakini hali hiyo ikaonekana kuwa siyo tatizo, akasema ni sahihi na ataingia kutekeleza ilani ya chama.”
Alisema kutokana na mazingira hayo ni muhimu zaidi kupata ushirikiano wa chama ili kurahisisha kazi yao hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi ambacho kinatazamiwa kuwa na matukio mengi ya rushwa kuanzia ndani ya vyama vya siasa.
“Lakini kwa sasa tumeshaanza kufanya uangalizi wa ndani ya vyama ili kuhakikisha rushwa haichukui nafasi katika uchaguzi huu.”
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema Takukuru hawahitaji kupata mwaliko wa CCM ili kufanya uchunguzi wa kukamata wagombea wanaotumia rushwa ndani ya chama hicho. Alisema rushwa inayoendelea kwa sasa iko wazi na kwamba sheria ya gharama za uchaguzi 2010 inawapatia mamlaka ya kufanya kazi bila vikwazo.
“Sheria hiyo inawapa mamlaka ya kuchunguza mazingira haya. Hakuna asiyeona wazi mazingira ya rushwa kwa wagombea kwani kama mtu anataka kugombea kisha anawachukua makada kwa ajili ya kula nao chakula nyumbani kwake, unadhani kuna nini kinaendelea hapo? Hilo mpaka waambiwe, nadhani huko ni kukwepa majukumu yao,” alisema Nape.
Mbali na Mangula, wengine waliowahi kulalamikia rushwa ndani ya chama hicho ni Mwenyekiti Jakaya Kikwete ambaye alitahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kukiuangusha chama. Kadhalika, Nape amekuwa akilalamika dhidi ya makada wanaotaka urais kuwa wanahonga wanachama.
Aidha, Bernard Membe na Fredrick Sumaye ambao wanatajwa kuwa na nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, wameshawahi kulalamika kuwa rushwa imezidi ndani ya CCM hasa kipindi cha uchaguzi na kuonya kuwa ikiendelea chama hicho kinaweza kuanguka.
Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo.
Baadhi ya wasomi na wanachama wa CCM waliozungumza na gazeti hili, walisema kama uongozi CCM una hakika na matukio ya rushwa ni vyema ukachukua hatua.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema tatizo la viongozi wa CCM kutochukua hatua dhidi ya rushwa, linachangiwa na kukosekana kwa ushahidi wa watuhumiwa. Alitoa mfano wa mkakati wa CCM ulioitwa Kujivua Gamba, ulivyoshindwa kuwaondoa viongozi wasio waadilifu kwa kukosa ushahidi. “Kama wanatambua kuna rushwa kwa nini wamekuwa wakilalamika wakati kuna vyombo vya kuchunguza? Walitakiwa kufanya uamuzi huo muda mrefu, lakini matokeo yake rushwa imeendelea kusambaa ndani ya chama mpaka serikalini, kwa wagombea wanaoamua kufidia rushwa zao walizotoa ndani ya vyama,” alisema Mbunda.
Profesa Abdul Sheriff, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, alisema kama rushwa imekithiri ndani ya Serikali, CCM haitakuwa na uwezo wa kuiondoa ndani ya makada wake.
“Viongozi kuzungumza pekee kwenye vyombo vya habari haisaidii kabisa na kama wangekuwa na uwezo, basi wangekuwa wameshachukua hatua ila kwa sababu ya nguvu za wanasiasa wa Serikali sidhani kama wataweza,” alisema Profesa Sheriff.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema: “Chama hakiongozwi kwa makaripio, mkakati wa kujivua gamba na matamko katika vyombo vya habari. Kinaongozwa kwa mifumo imara, fikra sahihi, dira na historia yake nzuri. “Ndiyo maana wanachama wa CCM wamekuwa wakitenda mambo kinyume na katiba ya chama chao na hakuna wa kuwachukulia hatua. (Katibu mkuu wa zamani, Horace) Kolimba aliwahi kusema kuwa CCM haina dira wala mwelekeo. Hilo linaonekana sasa, imeshindwa kukemea rushwa.
“Mchawi yupo ndani ya CCM yenyewe. Jimbo la Bukoba Vijijini limegawanyika kwa sababu ya rushwa inayotolewa na wanaotaka ubunge, hayo yote CCM hawayaoni na kukimbilia yanayotokea Zanzibar,” alisema Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana.
Alisema: “CCM ni chama ambacho kinajibu mapigo ila hakitoi mapigo. Kinachotokea sasa ni dalili mbaya kwake kwani kimekuwa dhaifu katika kuwashughulikia wanachama wake wasio waadilifu.”
Mwishoni mwa mwaka jana, Mangula alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa suala la rushwa linafuatiliwa kwa karibu na dawa yake itapatikana baada ya vikao vya kamati ya maadili.
Mangula alitoa kauli yake huku kukiwa na madai kuwa baadhi ya wanachama wanagawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya nchi.
Mangula pia aliwahi kukaririwa na gazeti la CCM mwishoni mwa mwaka jana, akisema: “Hakuna mwanachama aliye juu ya katiba, kanuni na miongozo ya chama na hivyo hakitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kutumia fedha.”
Oktoba 25, mwaka juzi, Rais Kikwete alisema endapo rushwa haitakomeshwa ndani ya CCM, chama hicho kitaanguka vibaya katika Uchaguzi Mkuu 2015 na iwapo kitanusurika hakitapita mwaka 2020.
Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Sumaye aliyewahi kuliambia gazeti hili kuwa iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya CCM itaendelea kulalia kwenye rushwa, hataendelea kuwa sehemu yake na kuonya kuwa tatizo hilo limefikia pabaya na litakiangusha chama hicho.
Mwaka 2011, Rais Kikwete alitangaza mkakati wa ‘kujivua gamba’ akiwataka makada wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari na kujiondoa ndani ya siku 90, lakini hata baada ya muda huo kumalizika, mkakati huo uliyeyuka na viongozi wakaanza kubadili maudhui yake.
Akizungumzia suala la rushwa ndani ya CCM, mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki alisema kwenye akaunti yake ya twitter: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya kwa wajumbe husika wa CCM ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa nafasi na si uwezo wa uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Kagasheki alisema: “Hii ni line yangu ninaitumia kutoa mawazo siku zote, lakini nimeshangaa leo watu wameshikia kidedea maoni hayo mpaka wengine wanatumia lugha kali... Sijamtaja mtu kwa sababu najua wapo watu wengi wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki.
aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.


CHANZO: MWANANCHI

No comments: