
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe, ameanza ziara ya siku sita kwenye mikoa ya
Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kagera.
Ziara hiyo inalenga mwendelezo wa uzinduzi wa programu ya FTP
maalum kwa ajili ya mafunzo ya uzalendo kwa vijana, shughuli ambayo
amekuwa akiifanya tangu Januari mwaka huu. Taarifa kwa vyombo vya habari jana iliyotolewa na Afisa Habari wa
Chadema, Tumaini Makene, ilisema ziara hiyo aliianza jana katika Wilaya
ya Nzega, mkoani Tabora.
Alisema ziara hizo zitaambatana na mikutano ya hadhara wilayani
Bariadi, Shinyanga kabla ya kwenda wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza. Maeneo mengine atakayozindua programu hiyo ni Bukoba Mjini kisha
Kyerwa na kwamba katika maeneo yote wamelialika Jeshi la Polisi kutoa
elimu ya ulinzi shirikishi na polisi jamii.
Makene alisema pia, wameialika Taasisi ya Kupambana na kuzia Rushwa
(Takukuru) ili kutoa elimu ya kupambana na kuzuia rushwa hasa wakati wa
uchaguzi. Aidha, alisema viongozi wengine wajuu wa chama hicho wataendelea na
programu ya uzinduzi wa mafunzo ya kukiandaa chama kushinda dola na
kuiongoza serikali, kwenye mikoa ya Tanga, Shinyanga na Mbeya.
Alifafanua kuwa Makamu Mwenyekiti Taifa Bara, Prof. Abdallah
Safari, atakuwa Korogwe Mjini na kuzindua mafunzo hayo kwa viongozi wa
Korogwe mjini na vijijini kisha kufanya mkutano wa hadhara Korogwe
mjini.
Alisema, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, atazindua mafunzo
wilayani Bariadi na pia atakuwa na mkutano wa hadhara Bariadi na Maswa. Kadhalika, alisema Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu,
atazindua mafunzo hayo wilayani Mbalizi na kufanya mkutano wa hadhara
Njombe mjini.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment