Social Icons

Pages

Thursday, April 23, 2015

MAGHOROFA JANGA JINGINE


Licha ya ujenzi maghorofa marefu kutajwa kuwa kielelezo cha maendeleo katika miji mikubwa, jijini Dar es Salaam hali ni tofauti kutokana na hofu iliyopo kuhusu ubora wa majengo hayo, mfumo wa majitaka, mipango miji na ukosefu wa maeneo ya maegesho.
Miaka 20 iliyopita, ilikuwa vigumu kuzungumzia maghorofa marefu jijini Dar es Salaam bila ya kutaja majina kama Kitega Uchumi (NIC House), kumaanisha jengo la Shirika la Bima la Taifa lenye ghorofa 16 na urefu wa mita 57.40, IPS lenye ghorofa 12 na urefu wa 43.05, au Extelecom House, kumaanisha jengo la Shirika la Posta lenye ghorofa 14 na urefu wa mita 50.23.
Lakini anga la Dar es Salaam sasa limepambwa na minara ya maghorofa marefu, yakiongozwa na jengo jipya la PSPF Towers ambalo urefu wake ni mara tatu ya kimo cha maghorofa yaliyokuwa yakisifika miaka 20 iliyopita. Jengo hilo lililo mbioni kukamilika lina urefu wa mita 152.85 likiwa na ghorofa 35.
Maghorofa mengine yaliyochomoza miaka michache iliyopita ni Uhuru, lenye ghorofa 27, jengo la Kakakuona lenye ghorofa 37, Benjamin Mkapa lenye ghorofa  37.
Mengine ni PSPF Golden Jubilee Towers lenye ghorofa 24 na urefu wa mita 103.2, jengo la uhuru Heights lenye ghorofa 27 na urefu wa mita 102.6, Umoja wa Vijana  lenye ghorofa 26, Viva Tower lililoko Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ambalo lina ghorofa 21 na urefu wa mita 75.34, BOT Towers lenye ghorofa 20 na urefu wa mita 100 na PPF Tower lenye ghorofa 16 na urefu wa mita 57.40.
Majengo marefu, ambayo kwa kawaida hupatikana kwenye miji mikubwa ambako hujengwa kutokana na ukosefu wa ardhi kubwa, yanatumika kwa ajili ya shughuli za kiofisi, makazi na kibiashara, hasa hoteli na klabu za usiku.
Lakini majengo hayo yameongezeka kwenye sehemu ndogo ya katikati ya jiji yakitegemea miundombinu iliyowekwa miaka 150 iliyopita, isipokuwa majengo machache kama Mawasiliano House, Millenium Towers na Ubungo Plaza yaliyo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mahitaji ya umeme sasa ni makubwa kuliko wakati mwingine wowote, hali kadhalika majisafi wakati kuingia katikati ya jiji nyakati za asubuhi na kutoka jioni ni shughuli kubwa kutokana na misululu mirefu inayosababishwa na idadi kubwa ya magari yanayobeba wafanyakazi wanaoenda kwenye ofisi zinazoendelea kuongezeka.
“Master plan (ramani kuu) ya Dar es Salaam iliisha muda wake miaka 36 iliyopita,” alisema meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Jerry Silaa hivi karibuni.
Alisema kukosekana kwa mpango huo, majengo marefu yanajengwa kiholela katikati ya jiji na kusababisha matatizo mbalimbali yakiwamo ya mafuriko na foleni kutokana na maji kujaa barabarani wakati wa mvua.
Silaa alisema baadhi ya sehemu ya zilizokuwa kwa ajili ya mashamba na makazi holela ya watu, hivi sasa zimegeuzwa viwanja vya kujenga majengo marefu.
Hata hivyo, alisema kutokana na ongezeko la watu katikati ya jiji, baadhi ya ofisi zimeanza kuhamishiwa sehemu za kando ili kukwepa foleni.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alikiri kuwa miundombinu iliyopo hailingani na mahitaji ya ongezeko la maghorofa. “Ni kweli kuwa miundombinu yetu ina walakini wakati maghorofa nayo yakichipuka kila siku,” alisema mkuu wa Sadiki alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kushamiri kwa majengo marefu. “Hata hivyo, ni dalili ya maendeleo ya kiuchumi kwa upande mwingine,” alisema.
Sadik alishauri maghorofa haya kujengwa katika miji mipya au ‘satelite cities’ ili kuepusha msongamano katikati ya Jiji.
Majengo hayo mengi yanamilikiwa na taasisi za fedha, kampuni za ujenzi na mifuko ya hifadhi ya jamii, matajiri wakubwa na mashirika mengine. Imeelezwa kuwa kiasi cha Sh800 bilioni zimewekezwa kwenye miradi mikubwa mitano, ukiwamo wa PSPF Towers.
Maghorofa ni lazima
Mkurugenzi wa kampuni ya maendeleo ya makazi ya Watumishi Housing, Dk Fred Msemwa alisema ongezeko la maghorofa jijini halizuiliki kutokana na mahitaji makubwa ya maeneo ya kufanyia biashara na ofisi. “Kasi ya kuongezeka kwa maghorofa ilitokana na kuwepo tofauti kubwa kati ya huduma za makazi na mahitaji, hivyo kampuni nyingi ziliwekeza eneo hilo ili kutoa huduma inayokosekana. Mpaka sasa bado kuna tofauti ndiyo maana majengo yanaendelea kujengwa na yanajaa haraka,” alisema.
Ripoti ya Kituo cha Makazi ya Gharama Nafuu (CAHF) ya 2014 inaeleza kuwapo kwa miradi mingi mikubwa ya ujenzi ambayo itaongeza wingi ya maghorofa hayo kwa kiwango kikubwa.
Ripoti hiyo inasema Shirika la Nyumba (NHC) pekee lina miradi lukuki ya ujenzi wa maghorofa  na inaeleza kuwa shirika hilo lina miradi minne na wabia kutoka China ya ujenzi wa majengo pacha yenye ghorofa 26 yatakayojengwa kwa Sh70 bilioni.
Inaongeza kuwa yapo majengo matatu yenye ghorofa 16 yatakayojengwa kwa gharama ya Sh30.3 bilioni kila moja na Group Six International na mengine mawili ya ghorofa 16 yanayojengwa na Estim Construction.
Pia ipo miradi mingine inayoendelea kama jengo la Kakakuona lenye ghorofa 36 litakalokamilika 2017 na Mzizima Tower litakalokuwa na ghorofa 33.
Hata hivyo, bado wasiwasi mkubwa ni kasi ya ujenzi huo kutolingana na kasi ya uboreshaji huduma hizo kwa jamii kama miundombini mibovu ya majitaka ambayo hufurika muda mfupi tu baada ya mvua kubwa kunyesha yakiacha takatakla zikizagaa barabarani, wakati ufinyu na uchache wa barabara hufanya kuwe na misululu mirefu ya magari wakati wakazi wakiwahi kwenye ofisi zinazoongezeka katikati ya jiji kutokana na ujenzi wa majengo hayo.

Athari zake
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa baadhi ya majengo yanajengwa chini ya kiwango kutokana na ujuzi mdogo, uzembe na rushwa na watu kadhaa wameshapoteza maisha kutokana na majengo hayo kuporomoka.
Machi 2013, jengo lililozidishwa urefu kinyume cha taratibu Mtaa wa Indira Gandhi liliporomoka na kuua watu zaidi ya 30. Maofisa wa Manispaa ya Ilala, mmiliki na mkandarasi walishtakiwa.
Ukiacha miradi mikubwa, majengo mengi yamejengwa sehemu zisizo na nafasi ya kutosha na hivyo kutoruhusu kirahisi magari ya uokoaji.
Mfano mwaka 2013 moto uliposhika ghorofa ya 17 ya jengo la PPF Tower, ilichukua saa kadhaa kwa Kikosi cha Zimamoto kukabiliana nao.
Matumizi ya umeme
Hadi kufikia Februari, 2014 Tanesco ilikadiria kuwa majengo manne tu ya PSPF Twin Tower, Uhuru Height, Viva Tower na Benjamin Mkapa Tower kwa pamoja yatatumia megawati 12 za umeme, ambazo ni zaidi ya megawati nane zinazotumika na mkoa mzima wa Mtwara.
Kiasi hicho cha umeme ni sawa na umeme unaotumiwa na mkoa huo na Lindi.
Afisa habari wa Tanesco, Adrian Severin alisema kuwa idadi ya maghorofa haijawa kubwa kiasi cha kuzidi kiwango cha mwisho cha ugavi, lakini akaongeza “tuna hofu tutazidiwa siyo muda refu ndiyo maana tunakamilisha ujenzi wa substation ya zaidi ya megawati 100 kuongeza nguvu kwa iliyokuwepo Barabara ya Sokoine”.
Ofisa Uhusiano wa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), Everlasting Lyaro alisema baadhi ya majengo katikati ya jiji yalijengwa kwa ajili ya makazi ya watu nane, lakini yamebadilishwa kuwa ya biashara hivyo kutumiwa na zaidi ya watu 500 huku mfumo wa maji taka ukibaki kuwa ule ule wa zamani.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: