
Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba.
     
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeanzisha 
utaratibu mpya wa mafunzo kwa vitendo kwa watendaji wanaoandikisha 
wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa 
Biometric Voters Registration (BVR).
Jumla ya BVR kits 498 zitatumika kutoa mafunzo hayo, lengo likiwa 
ni kurahisisha uandikishaji, baada ya awamu ya kwanza kusuasua katika 
Mkoa wa Njombe.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa mikoa minne ya awamu ya tatu ya 
uandikishaji wapiga kura na yatakuwa endelevu ili kuharakisha 
uandikishaji utakaoanza Mei 2, mwaka huu. Mkurugenzi wa Nec, Julius 
Malaba, akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu, alisema Nec 
imeamua vifaa hivyo vitumike kwenye mafunzo ya vitendo kwa watumishi hao
 ili kuharakisha uandikishaji.
Awamu ya kwanza ya uandikishaji ilikuwa Mkoa wa Njombe, ya pili 
inayoanza kesho ni Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa na awamu ya 
tatu ni Dodoma, Mbeya, Katavi na Tabora.
“Tumeamua BVR kits zilizotumika mkoani Njombe 250 na 248 
zilizowasili mwanzoni mwa Aprili, mwaka huu, zitatumika kwa mafunzo ili 
tunapofika kwenye uandikishaji uende haraka zaidi,” alisema. Mikoa ya 
awamu ya pili ya uandikishaji kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 
mwaka 2012 kwa Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ina 
jumla ya watu wenye sifa ya kupiga kura ifikapo Oktoba, mwaka huu 
wapatao 4,306,569.
Malaba alisema BVR 1,600 zilizowasili katikati ya Aprili, mwaka 
huu, zitatumika kuandikisha katika mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara na 
Ruvuma yenye watu wenye sifa ya kupiga kura ifikapo Oktoba, mwaka huu ni
 2,599,205.
Tangu Februari 23, mwaka huu, Nec ilianza uandikishaji katika Mkoa 
wa Njombe wenye watu wenye sifa za kupiga kura 392,634, lakini hadi 
uandikishaji unafika Aprili 18, mwaka huu, walikuwa wameandikishwa watu 
300,080 ikiwa ni tofauti ya watu 92,554.
Mkurugenzi huyo alisema BVR 1,600 zitakazowasili kati ya Jumamosi 
na Jumapili wiki hii, zitatumika kwenye awamu ya pili ya uandikishaji 
wapiga kura. Alisema kwa sasa mafunzo kwa vitendo kwa idadi ya BVR zilizopo ni 
endelevu ili wakati wa uandikishaji kusiwe na ucheleweshaji kama 
ilivyotokea kwenye Mkoa wa Njombe kutokana na ugeni wa matumizi ya 
mashine hizo.
Aprili 2, mwaka huu, Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva,
 alitangaza kuahirishwa kwa Kura ya Maoni kwa Katiba inayopendekezwa 
kutokana na kushindwa kukamilika kwa daftari la kudumu la wapiga kura na
 itatangazwa tena.
Alisema tarehe ya kura hiyo itatangazwa tena baada ya Nec kushauriana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec). Nec ilisema hadi wakati huo, serikali ilikuwa imetoa Dola milioni 72 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 13). Vifaa hivyo vinanunuliwa na serikali kupitia kampuni ya Lithotech 
Export ya Afrika Kusini ambayo imeingia mkataba na Nec na inaviagiza 
China.
Taarifa zilizopatikana ndani ya tume hiyo zinaeleza kuwa, kampuni 
hiyo ndiyo inayotoa muundo wa ndani (soft ware) ya mashine hizo na 
kwamba utengenezaji wa mashine moja na kuweka vifaa vyote muhimu 
inachukua wiki sita. Hadi sasa Nec imeshapokea BVR kits 2,098 na zilizokuwa zimeagizwa kukamilisha uandikishaji nchi nzima ni 8,000.
Nec ilieleza kuwa matarajio yake ni kuwa ifikapo Julai mwaka huu, uandikishaji ukamilike nchi nzima. Pia uandikishaji utaendelea kwenye mikoa yote na Jiji la Dar es 
Salaam na Zanzibar itakuwa ya mwisho ili BVR kits zote zitumike kwa 
pamoja kwenye mikoa hiyo.
     CHANZO:
     NIPASHE
    
 

No comments:
Post a Comment