Social Icons

Pages

Thursday, April 23, 2015

UCSAT, KAMPUNI ZA SIMU KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Prof. John Nkoma.
Mfuko wa Mawasilino kwa wote (UCSAT), umeingia mkataba na makampuni manne ya simu nchini na kampuni ya satelaiti ya Avanti ya Uingereza, kwa ajili ya kusambaza mawasiliano kwenye kata 102 za vijijini, mtandao kwa shule za serikali 250 na kuunganisha vituo na mafunzo ya Tehama 25.
Mkurugenzi wa UCSAT, Peter Ulanga, alisema kata hizo ni kati ya 158 zilizotangazwa, lakini kata 112 zilikubalika na kiasi cha ruzuku ni Sh. bilioni 14.2 pamoja na kata kumi za maradi wa mawasiliano mipakani ambazo zitagharimu Sh. bilioni 2.7.
Ulanga alisema pia mfuko huo kwa kushirikiana na makampuni hayo wameunganisha hospitali saba na sasa wameunda kikosi kazi cha kuangalia uwezekano wa kuunga hospitali 150 za wilaya katika huduma ya ‘telemedicine’.
Alisema pia wako katika hatua ya mwisho ya kusaini makubaliano na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa ajili ya kugawa kompyuta mpakato kwa wanafunzi walimu ili wanaporudi kazini iwe rahisi kufundisha wanafunzi.
Akizungumza na viongozi wa makampuni hayo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa, alisema awamu ya kwanza ilihusisha kata 52, ya pili 86 na kwamba serikali inatoa zuruku nusu kwa maeneo ya vijijini na mipakani asilimia 100 ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Tehama ya mwaka 2003 inayoeleza mawasiliano ni haki ya kila mwananchi.
Alisema serikali inatambua kuwapo kwa maeneo yasiyo na mvuto kibiashara na ndiyo maana inatoa ruzuku ya asilimia 30 hadi 80 ili kuwezesha mawasiliano kufika. “Watanzania milioni 12.3 sawa na asilimia 57 ya wenye umri wa miaka 16 na zaidi wana akaunti za fedha za simu na asilimia 14 ndiyo wenye akaunti benki…mawasiliano ni kichocheo cha maendeleo ya uchumi na kijamii, yameongeza ajira kwa Watanzania 200,000 kupata ajira za moja kwa moja, milioni 1.5 zisizo za moja kwa moja kwa makampuni hayo,” alibainisha.
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Ngodo, alisema mawasiliano ni benki, hospitali, elimu, biashara kwa kuwa yanarahisisha na kuwezesha utoaji wa huduma ya kusaidia kukuza uchumi kwa kasi kubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Prof. John Nkoma, alisema jamii inapaswa kutumia vizuri mawasiliano na mtandao kwani kwa siku za hivi karibuni licha ya kuwapo kwa kasi ya mawasiliano pia kuna kasi ya matumizi mabaya ya mtandao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: