
Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa
Kinyang’anyiro
cha kuwania urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kitafikia katika
hatua ngumu mwezi ujao kitakapochukua uamuzi mgumu dhidi ya baadhi ya
makada wake walioonyesha nia ya kuwania urais, akiwamo Edward Lowassa.
Kiongozi huyo pamoja na makada wengine sita wa
CCM, walipewa kifungo cha miezi 12 kwa madai ya kuanza kampeni za urais
mapema kinyume na taratibu za chama hicho iliyomalizika katikati ya
mwezi uliopita na sasa wanasubiri kwa hamu, tangazo la Kamati Kuu
(CC-CCM) ili wawe huru kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya
chama hicho na kuendelea na shughuli nyingine za kujiandalia mazingira
ya kupitishwa.
Mbali ya Lowassa, wengine waliofungiwa ni Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja;
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; na Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Habari kutoka ndani ya chama hicho zinasema baadhi
ya wagombea huenda wakaongezewa adhabu kutokana na kuendelea na kampeni
kabla ya wakati wake na kwenda kinyume na taratibu za chama hicho.
“Kuna wagombea wataongezewa adhabu kwa kukiuka
utaratibu wa chama kwa kuendelea kufanya kampeni za mapema,” kilisema
chanzo chetu.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo,
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hana taarifa kwa
kuwa uchunguzi dhidi ya makada hao bado haujakamilika. “Uchunguzi hata
nusu haujafika. Kuna watu wanahangaika kwa sababu hawana sifa za kutosha
na ndiyo wanaotengeneza hizo taarifa,” alisema Nape na kuongeza: “Mtu yeyote ambaye hajavunja taratibu hana sababu
ya kuwa na hofu na kama kuna watu wamevunja taratibu hawana namna ya
kukwepa mkono wa chama.”
Hivi karibuni, kumeibuka wimbi la watu wa kada
mbalimbali kujitokeza kwa makundi kwenda nyumbani kwa Lowassa Mjini
Dodoma, kumshawishi achukue fomu za kuwania nafasi hiyo ya juu ya
uongozi wa nchi hatua ambayo ilikemewa na Nape ambaye alimtaka kuacha
mara moja.
Hivi karibuni, Nape alikaririwa na vyombo vya
habari akisema vitendo vinavyofanywa na Lowassa ni kampeni za wazi za
urais kabla ya muda kufika na hivyo kukiuka kanuni za chama hicho
kitendo kinachoweza kumnyima sifa za kugombea nafasi ya urais.
“Anachokifanya Lowasa ni kuvunja kanuni na kiburi,
ni matendo ya wazi ya kampeni, bila shaka anajua adhabu yake. Matendo
hayo yanaweza kumpotezea sifa za kuwa mgombea kupitia CCM,” Nape
alikaririwa akisema. Alisema Lowassa ni miongoni mwa makada ambao
walipewa adhabu na mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha uangalizi
wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao.
Lowassa alijibu onyo hilo la Nape kwa kuyazuia
makundi hayo kuendelea kufika kwake kumshawishi lakini akihoji kuwa
kauli hiyo imetokana na uamuzi wa kikao gani ndani ya CCM. Alisema hayo
siku ambayo aliwapokea vijana waendesha pikipiki(bodaboda) zaidi ya 60
na wananchi wa kawaida waliokuwa wamefunga safari kutoka Mbarali Mkoa wa
Mbeya kwenda kumshawishi agombee urais. Lowassa alisema CCM ina utaratibu wake wa kujadili mambo kama hayo.
Mbali ya vijana hao kundi jingine lililokwenda kwa
Lowassa ni la wachungaji ambao walimweleza kwamba wameamua kumshawishi
wakiamini kuwa ndiye chaguo sahihi kwao.
Kundi la kwanza kwenda kumshawishi Lowassa
lilikuwa la Masheikh 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo, Pwani ambalo
alilieleza kwamba ameshawishika kuwania nafasi hiyo. Hata hivyo, baadhi ya watu walioshiriki katika
safari hizo za ushawishi wamejikuta katika wakati mgumu kutokana na
kuhojiwa na baadhi ya taasisi zikiwemo vyuo na za dini kujitokeza na
kusema hazihusiki na suala hilo.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba alijitokeza na kulaani kitendo hicho akisema
si cha kiungwana na kwamba kila mgombea anaweza kufanya hivyo, lakini
wanaheshimu kanuni na katiba ya CCM. January alipoulizwa jana kuhusu kuongezwa kwa
adhabu kwa baadhi ya makada, hakusema kama anazijua au hazijui taarifa
hizo lakini alieleza kuwa kati ya watu waliopewa onyo wapo waliobaki
kwenye misingi na wengine wameendelea kukusanya makundi. “Ushahidi
unakusanywa na wale ambao hawakubaki kwenye misingi watachukuliwa
hatua.”
Ofisa Habari wa Lowassa, Aboubakary Liongo alisema
jana kwamba hawajasikia lolote kuhusu kuongezwa adhabu kwa baadhi ya
wagombea waliokuwa wamefungiwa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment