Naibu Spika, Job Ndugai, amesema madai yanayotolewa kuwa amezuiliwa kuendesha shughuli za Bunge ni mambo ya kawaida.
Tangu kumalizika kwa mkutano wa Bunge wa 16 na 17 ambao ulijadili
kashfa ya uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta
Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Bunge kutoka na maazimio
nane, Ndugai hajawahi kuonekana bungeni kuongoza shughuli za Bunge.
Hakuhudhruia Mkutano wa 19 na wa 20 unaoendelea hivi sasa., hali
iliyozua madai kutoka kwa baadhi ya wabunge na watu wengine kuwa
amezuiliwa kuendesha shughuli za Bunge kutokana na msimamo wake wa
kuruhusu kujadiliwa kwa kashfa hiyo bungeni.
Baadhi ya watu ambao wamezungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti
mjini Dodoma walisema kitendo cha Ndugai kutoa uhuru zaidi wakati wa
mjadala wa sakata la Escrow inadaiwa hakikuwafurahisha wakubwa kwani
ilipelekea serikali kutikisika.
Ndugai alipoulizwa na NIPASHE jana kwa njia ya simu kuhusiana na
taarifa hizo, hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo zaidi ya kuomba
asilizungumzie. Hata hivyo, alisema kwa kifupi: “Naomba uwaambie waachane na hiyo
issue (jambo), siwezi kuzungumza lolote, mbona ni la kawaida tu.”
Alipoulizwa kuwa kwa sasa yuko wapi, alisema kuwa alikuwa safarini bila kueleza alikokuwa akielekea. Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, alipoulizwa
kama anafahamu aliko Ndugai, alisema hafahamu kwa kuwa wabunge
hawajajulishwa na ofisi ya Bunge.
Kwa upande wake Mbunge wa Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi),
alisema kiutaratibu Spika wa Bunge, Anne Makinda alitakiwa kuwafahamisha
aliko Ndugai lakini kwa bahati mbaya hajatujulisha. Taarifa za awali kutoka kwa wafanyakazi wengine Bungeni walisema Ndugai ni mgonjwa.
Wafanyakazi hao walisema mara baada ya kikao cha Bunge cha mwezi
Novemba mwaka jana Ndugai ambaye ni pia ni Mbunge wa Kongwa, alianza
kujisikia vibaya kiafya na hivyo kwenda nchini India kwa matibabu. Inadaiwa Ndugai ambaye amekaa huko kwa muda mrefu alirejea nchini
mwanzo mwa wiki iliyopita na alipitia Dar es Salaam kwa ajili ya
kupumzika.
Mwandishi wa NIPASHE alipofika ofisi ya Naibu Spika kuomba kuonana
naye, Katibu Muhtasi ambaye jina lake halikufahamika, alisema Ndugai
hayupo kwa muda mrefu na hawafahamu aliko. Chanzo kingine kilieleza kuwa muda mfupi kabla ya Mkutano wa sasa
wa Bunge kuanza, Ndugai alikuwa Dar es Salaam akijiandaa na safari ya
kwenda nje kwa matibabu.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alisema Ndugai ataongoza vikao vya Bunge kuanzia leo. Dk. Kashililah alisema Ndugai alikuwa amesafiri kikazi nchini
Ubelgiji ambako alihudhuria mkutano na alipitia India kufanyiwa
uchunguzi wa afya yake, lakini amesharejea nchini.
Katika kipindi ambacho Ndugai hakuwapo, vikao vya Bunge vilikuwa
vinaendeswa na Spika Makinda, wenyeviti wa Bunge, Mussa Zungu na Rediana
Mng'ong'o. “Leo Mheshimiwa Ndugai atakuwapo bungeni kwa sababu Spika amebaki
pekee yake baada ya Mheshimiwa Zungu kwenda Dar es Salaam kwenye
mafuriko na Mheshimiwa Mng’ong’o amekwenda nje ya nchi kuhudhuria
mkutano,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment