Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Ardhini na Majini (SUMATRA)
Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam, utafungwa
kuanzia Jumatano wiki hii ili kupisha ujenzi wa mfumo wa mabasi yaendayo
haraka.
Taarifa kutoka wakala unaosimamia mradi huo, Dart ilisema ujenzi wa
sehemu hiyo utaanza Aprili Mosi, mwaka huu na mkandarasi mkuu,
Strabag Internation.
Kipande hicho kinachoanzia eneo la ‘Fire’, kina umbali wa kilomita
moja lakini ni moja ya maeneo muhimu kwa mfumo huo wa usafiri wa mabasi
yaendayo haraka. Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa mwishoni mwa
wiki jijini Dar es Salaam, njia nyingi zinazokutana na mtaa wa Msimbazi
zitafungwa moja kwa moja isipokuwa mitaa ya Lindi, Uhuru, Mafia na
Swahili ambapo taa za kuongozea magari zitawekwa katika makutano ili
kurahisisha upitaji wa magari.
Kutokana na ujenzi huo Wakala wa Dart kwa kukubaliana na Mamlaka ya
Usimamizi wa Usafiri wa Ardhini na Majini (Sumatra) na wamiliki wa
mabasi ya daladala, wamekubaliana kuwa mabasi ya abiria kutoka barabara
ya Morogoro yatavuka kona ya mtaa wa Msimbazi na kukata kulia
yatakapofika mtaa wa Lumumba.
Patakuwa na kituo kipya cha daladala katika mtaa wa Lumumba kabla
ya makutano na mtaa ya Uhuru. Daladala zitakata kushoto katika mtaa wa
Uhuru na kushoto tena barabara ya Bibi Titi na hatimaye kushoto tena
Barabara ya Morogoro.
Pia daladala kutoka barabara ya Kilwa zitakata kulia kuelekea
barabara ya Nyerere, kisha kushoto kuelekea mtaa wa Uhuru na kisha
kushoto tena kuelekea Lumumba. Baada ya hapo mabasi hayo yatatakiwa
kukata tena kulia barabara ya Nyerere na hatimaye kushoto barabara ya
Gerezani.
Mabasi ya abiria kutoka Chang’ombe na Buguruni yatatokea barabara
ya Uhuru na kukata kushoto mtaa wa Shaurimoyo ambapo yatakata kulia
kuelekea mtaa wa Lindi na kugeuzia katika eneo la muda lililojengwa
karibu na kituo cha baadaye cha mabasi yaendayo haraka cha Kariakoo. “Wakala wa Dart unaomba radhi kwa usumbufu utakaotokea kutokana na mabadiliko haya ya njia,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakala unategemea kuanza kutoa huduma
ya mabasi kwa kipindi cha mpito kutokea Mbezi Louis kuelekea Kimara hadi
Kivukoni na mabasi 76 Julai, mwaka huu. Huduma kamili inatarajiwa
kuanza mwishoni mwa mwaka 2016. Kwa ujumla kazi ya mfumo huo kwa awamu ya kwanza umeshakamilika kwa asilimia 90. Awamu hiyo inatarajiwa kukamilika Novemba, mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment