Miaka 20 iliyopita ilikuwa ni nadra kukutana na
mwanamke anaendesha gari na wachache waliomudu kuwa na chombo hicho
walionekana kuwa na uwezo wa hali ya juu.
Huenda hali hiyo kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na
dhana ya mfumo dume uliojengeka katika katika jamii kuwa wanaume ndiyo
wanaopaswa kumiliki na kuendesha magari. Dhana hiyo ilianza kuondoka kuanzia miaka ya 2000
baada ya wanawake wachache kuamua kuvunja ‘mwiko’ kwa kununua na kuingia
barabarani wakiwa na magari yao.
Baada ya mfumo wa uendeshaji gari kubadilishwa
kutoka ‘manual’ hadi ‘automatic’, ndivyo idadi ya wanawake waliotaka
kuendesha magari ilivyoongezeka. Anael Kimario ambaye anajihusisha na biashara ya
uagizaji wa magari kutoka nje ya nchi anasema hivi karibuni idadi ya
wanawake wanaoendesha vyombo hivyo imeongezeka maradufu.
Anasema pamoja na kuendesha wanawake pia wamekuwa
na uthubutu wa kumiliki magari tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo
chombo hicho kilikuwa kinaonekana cha anasa. “Mambo yamebadilika wanawake wamekuwa na uthubutu
wa hali ya juu kutaka kumiliki na kuendesha magari na ndiyo maana
ukipita barabarani haiwezekani ipite dakika mbili bila kumuona mwanamke
kwenye usukani.”
Kimario anaeleza kuwa ujasiri huo wanawake
umechangiwa kwa kiasi kikubwa wa utengenezaji wa kisasa unaofanya zoezi
zima la uendeshaji gari kuwa rahisi.
“Unajua magari mengi kwa sasa yamerahisishwa
teknolojia yake yanakuwa automatic hivyo kwa kiasi kikubwa linajiendesha
lenyewe kwa msaada mdogo wa dereva ndiyo maana wanawake wengi wanaweza
kuendesha bila wasiwasi wowote”
Magari gani yananunuliwa zaidi na wanawake kwa sasa?
Kimario anaeleza kuwa licha ya wanawake wengi
kumiliki magari lakini idadi kubwa ya magari hayo huwa ni yale
yanayouzwa na kuendeshwa kwa gharama nafuu. Anataja Toyota IST kuwa ni mojawapo ya aina ya
gari ambayo inanunuliwa zaidi na wanawake kwa sasa tangu kuanza
kuingizwa nchini miaka mitatu iliyopita.
Gari hili ambalo bei yake ni kati ya Sh9 milioni na Sh12 milioni
limekuwa kivutio kikubwa kwa wanawake kutokana na muundo wake wa nje.
Udogo wa ‘engine’ ya gari hilo umechangia
kuwavutia wanawake wengi kwani inatumia kiwango kidogo cha mafuta hali
inayowawezesha wengi kumudu gharama za uendeshaji.
Kimario analitaja gari lingine linalonunuliwa
zaidi na wanawake ni kuwa ni Toyota Spacio modeli mpya ambalo umbile
lake ni kubwa kidogo ikilinganishwa na IST.
“Spacio bei yake inaanzia kwenye milioni 10 mpaka
15, gari hili linawavutia wengi kutokana na muundo wake wa nje upo kama
yai halafu ni imara endapo mtumiaji atakuwa muangalifu,” anasema
Kimario.
Kwa upande wake Hubert Muganyizi ambaye pia
hujihusisha na biashara hiyo anasema magari madogo aina ya Toyota Vitz,
Raum na Passo yamekuwa yakinunuliwa kwa wingi na wanawake ikilinganishwa
na aina nyingine.
Muganyizi anaeleza kuwa sababu ya magari hayo kuwa
na soko kubwa kwa wanawake inatokana na unafuu katika bei ya ununuzi na
gharama za uendeshaji. “Kwanza magari haya yanauzwa bei nafuu mfano Passo
na Vitz inacheza kwenye milioni saba mpaka tisa na ukiagiza kutoka
Japan inakuwa nafuu halafu kitu kingine ni miundo yake inaendana kabisa
na wanawake,” anasema Muganyizi.
Anasema, “Sina kumbukumbu vizuri lakini mzigo wa
magari nilioagiza mwishoni mwa mwaka jana nililazimika kuongeza idadi ya
Passo, Vitz na IST kwani zimekuwa zikihitajika zaidi na wateja wa
jinsia zote.”
Pamoja na unafuu wa bei, Muganyizi anasema
upatikanaji wa vipuli vya magari hayo kwa urahisi ni sababu nyingine
inayochangia kupendwa siyo na wanawake pekee bali watu wengi wa hali ya
kawaida kiuchumi.
Anaeleza kuwa magari aina ya Toyota RAV 4 na Nadia
nayo yamekuwa yakipendelewa zaidi na wanawake lakini idadi yake siyo
kubwa ikilinganishwa na magari madogo.
Vitu gani wanaangalia wanawake wanapochagua gari?
Brenda Maganga anasema kabla ya kufanya uamuzi wa
kununua gari analomiliki kwa sasa ambalo ni Toyota Spacio alizingatia
mambo kadhaa lakini kubwa lilikuwa rangi na unafuu katika gharama. “Chaguo langu la kwanza lilikuwa aina ya gari pili ilikuwa rangi
masuala ya kiufundi siyafahamu kwa sana ingawa kwa akili ya kawaida
naweza kubaini kuwa hari haliko sawa,” anasema Brenda.
Kwa upande wake Lilian Kisamo jambo kubwa analozingatia kwenye uchaguzi wa gari ni ukubwa wa mashine na ulaji wake wa mafuta. “Kwa hali ya maisha ya Watanzania wengi
tunaangalia gharama binafsi lazima nichague gari zuri ambalo litakuwa na
bei nafuu halafu hata uendeshaji wake nitaumudu hivyo napendelea gari
linalotumia mafuta kidogo”
Takwimu hizo haimaanishi kuwa ni aina hizo za
magari pekee ndiyo hununuliwa na wanawake Kimario analeza wapo
wanaonunua magari yenye gharama na muundo mkubwa kama ilivyo kwa
wanaume. Anayataja Toyota Allex, Runx, Harrier ni aina nyingine za
magari ambazo zimekuwa zikipendwa na kununuliwa na wanawake. “Wapo wanawake wanaonunua magari ya kifahari kama
Range, Prado, VX, Kluger, Alteza, Mark X, Verossa, Voxy, Lexus lakini
hawa siyo wengi kama ilivyo kwenye magari madogo niliyokueleza,” anasema
Kimario.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment