Social Icons

Pages

Monday, March 30, 2015

UJENZI RELI YA KATI KUANZA JUNI 2015 KWA TRILIONI 14/-

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Serikali imetangaza ujenzi wa mradi mkubwa wa reli mpya ya kati utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 7.6 (Sh. trilioni 14), ambao jiwe lake la msingi linatarajiwa kuwekwa na Rais Jakaya Kikwete Juni 30, mwaka huu, kwa ajili ya kuanza rasmi kazi hiyo, itakayochukua miaka mitano.
Pia imetangaza mpango wake wa kuweka mawe ya msingi katika reli ya Kusini (Mtwara-Songea-Mbambabay na Mchuchuma-Liganga) na reli ya Kaskazini (Tanga-Arusha-Musoma na viunganishi vya Engaruka Soda Ash Mines, Minjingu Phosphete), zitakazogharimu dola za Marekani bilioni 6.6.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (pichani), alisema  jana jijini Dar es Salaam kuwa reli mpya ya kati itakayokuwa na kiwango cha upana wa mita moja zaidi tofauti na wa reli iliyopo, itakuwa na urefu wa kilomita 2,561, uwezo mkubwa wa kimataifa na itaanzia Dar es Salaam mpaka Kigoma kupitia Tabora, Mwanza, Isaka hadi Rusumo; Kaliua-Mpanda-Karema na Uvinza-Musongati nchini Burundi.
Sitta alisema Kampuni ya Rasilimali za Reli (Rahco) wamekamilisha utaratibu wa kumpata mshauri wa mradi, ambaye ni kampuni ya Rothschild ya nchini China itakayowezesha kupata fedha za ujenzi wa reli hiyo kwa kiwango hicho. Alisema mradi huo ndiyo mkubwa kutekelezwa na serikali tangu uhuru na kwamba serikali haitatoa hata dola moja kutoka Hazina, badala yake utagharimiwa na mabenki takriban 100, ambayo ndiyo yatakayotoa fedha.
Waziri Sitta alisema mkopo huo utarejeshwa kwa kipindi cha miaka watakayokubaliana kutokana na gharama za tozo ya mizigo itakayopitishwa kwenye reli hiyo. “Tunatarajia mkopo huo utalipwa ndani ya muda wa miaka 20,” alisema Waziri Sitta.
Alisema pamoja na masuala mengine, reli hiyo itasaidia kukidhi mahitaji makubwa ya ubebaji mizigo kwenda nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Burundi na Rwanda na pia itasaidia usafirishaji wa wananchi kwenda mikoani kwa wingi na kwa kasi zaidi.
Alisema serikali imeamua kujenga kutokana na ile iliyopo sasa, ambayo ni kiwango cha meter gauge uwezo wake wa kubeba mizigo hata baada ya ukarabati kwa mwaka ni tani milioni tano, ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo ya kanda hiyo, ambayo yatafikia tani milioni 30 ifikapo mwaka 2025.
“Hivyo basi, tunahitaji kukabiliana na uongezekaji wa mizigo kwa kujenga uwezo wa kuihudumia kwa kuwa na reli, ambayo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba mizigo hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi na kwa starehe, lakini pia kwa kasi ya spidi ya wastani wa kilomita 100 kwa saa, hivyo kuwezesha abiria kufika haraka zaidi sehemu wanazokwenda,” alisema Sitta.
Alisema mradi huo utaajiri Watanzania takriban 300,000 watakaohusika na ujenzi wa reli hiyo. Kwa mujibu wa Waziri Sitta, reli hiyo itafanya upelekaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam mpaka DRC kuchukua muda wa takriban saa 12. “Tumejipanga ili uzinduzi wa ujenzi wa reli hii ya kihistoria ufanywe na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuweka jiwe la msingi ifikapo Juni 30, 2015 kule Mpiji kituo cha stesheni mkoa wa Pwani, ambako ndiko reli hii itaanzia,” alisema Sitta.
Alisema uamuzi wa reli hiyo mpya kuanzia Mpiji, ambako Rahco imechukua eneo la hekta 1,000, unatokana na reli hiyo kutotaka milima sana, ambayo kutoka Mpiji kwenda Pugu mpaka Dar es Salaam ni  vigumu  kuipenya  milima  iliyopo. Alisema kama kampuni nyingine zitaamua kuanzia Mwanza na nyingine Kigoma, suala hilo litafuatia baadaye kwa kuwa linahitaji utaalamu.
Pia alisema ujenzi wa reli ya Kusini na Kaskazini utawatengenezea zaidi ya Watanzania 500,000 ajira mpya. “Kwa jumla reli zote tatu zitagharimu jumla ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 14.2, ambazo ni sawana Sh. trilioni 26 zitaajiri zaidi ya Watanzania milioni moja kwa miaka yote zitakapokuwa zinajengwa kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2021,” alisema Waziri Sitta.
Awali, Waziri Sitta alisema Machi 26, mwaka huu, walipokutana wawekezaji, Tanzania ilitiliana saini makubaliano ya awali kati yake na DRC na Burundi kukubaliana kupitisha mizigo ya nchi hizo yenye uzito wa tani milioni 12 kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Alisema hadi sasa bandari hiyo inahudumia tani milioni 14 na kwamba, tani hizo za mizigo ya nchi hizo zitakuwa za ziada.

CHANZO: NIPASHE

No comments: