
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (kushoto) akizungumza na
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alipokwenda
kumjulia hali katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam jana.
Utata umeibuka
kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada ya kiongozi huyo
kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
Gwajima aliyetolewa kwenye chumba cha uangalizi
maalumu cha Hospitali ya TMJ jana, amelitaka Jeshi la Polisi kurudisha
bastola hiyo, akisema ni mali na aliiagiza ipelekwe hospitalini kwa
sababu ya kujilinda.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini
hapo alipolazwa baada ya kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu akiwa katika
mahojiano na polisi, Gwajima alisema anashangaa kukamatwa kwa wachungaji
wake waliokuwapo kwa ajili ya kumlinda.
Hata hivyo, katika kwa upande mwingine, Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bunduki
hiyo haina umiliki halali wa Gwajima wala wa wachungaji 15 waliokamatwa
lakini baadaye jioni baada ya maelezo ya Gwajima, alitoa taarifa akisema
bastola hiyo ni mali halali ya askofu huyo. Pia alisema kuhusu risasi
17 za bunduki aina ya Shortgun, Gwajima anamiliki bunduki ya aina hiyo
lakini akasema uchunguzi kuhusu watu hao 15 unaendelea.
Kauli ya Gwajima
Akizungumza kwa shida akiwa amejishika tumbo,
Gwajima alisema alipopata taarifa za uvumi kwenye mitandao ya kijamii
kuwa amefariki dunia, aliagiza wachungaji waende hospitalini kwa ajili
ya kumlinda, lakini wakaishia mikononi mwa polisi wakidaiwa kutaka
kumtorosha.
Alisema alihofia kuwapo kwa watu wabaya ambao
wangeweza kumdhuru halafu wakasingizia kitendo hicho kufanywa na polisi
kwa kuwa alipata tatizo akiwa mikononi mwao. “Usiku wasiwasi ulizidi, huku kila mmoja akiwa
hafahamu kwa nini ujumbe wa namna ile unasambazwa kwenye mitandao,
msambazaji ni nani, ana nia gani, nikaamua kuwaagiza waniletee silaha
yangu iliyokuwa kwenye begi ili likitokea lolote niweze kujilinda,”
alisema Gwajima.
Alisema alishangaa kukamatwa wachungaji wake na
kuchukua silaha iliyokuwa ndani ya begi na hadi jana hakuwa ameulizwa
chochote kuhusu umiliki wa silaha hiyo. “Kabla sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa
kinachodaiwa kuwa nilitaka kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka
kuzungumza na ZCO (Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi
ya ile silaha ninayo,” alisema Gwajima.
Alisema madai kuwa alitaka kutoroka ilihali polisi
alikwenda mwenyewe akitokea Arusha baada ya kusoma katika vyombo vya
habari kuwa anatafutwa.
Alifafanua kuwa hata alipofika polisi kwa ajili ya
mahojiano hakuwa na shaka hata kidogo, lakini alishangaa kuona
anaishiwa nguvu kila baada ya muda na alipoona kichwa kinamuuma,
akawaomba wampeleke hospitali ili mambo mengine yafuate baadaye, kitu
ambacho hakikufanyika kwa wakati.
Wasiwasi kwa polisi
Alisema alijaribu kuomba apelekwe hospitali mara
kadhaa, lakini hakuna aliyekubaliana naye hadi alipopoteza fahamu na
kupelekwa hospitali ya Polisi Kurasini. “Hivi hata kama ni chombo cha usalama, nimepata
matatizo nipo mikononi mwao, halafu nikubali kutibiwa katika hospitali
yao, sikulitaka hilo na hata waliposema nikatibiwe Muhimbili pia
sikutaka, ndiyo maana nilikuja hapa, sisemi moja kwa moja kama Polisi
wanahusika lakini kuna vitu vinanitia shaka,” alisema Gwajima.
Alieleza kuwa anatilia shaka Jeshi la Polisi
kutokana na kuwapo vitu vingi vinavyoashiria wana kitu kingine
wanatafuta, kwani jana tulikuwa na hofu ya kuvamiwa, waliokuja kutuvamia
ni wao, sikugombana na Pengo, nilikuwa namkemea kama kiongozi mwenzangu
wa kiroho wao, wameligeuza ni kesi. “Sijawahi kulitilia shaka Jeshi la Polisi lakini
katika hili napata wasiwasi mwingi, sina ugomvi na Kardinali Pengo,
nampenda, hajanilaumu, wala kunishtaki, nilikuwa namkemea katika masuala
yetu ya mabaraza ya dini na siyo vinginevyo,” alisema Gwajima.
Gwajima pia alionyesha wasiwasi wake kwa kile
kilichokuwa kinang’ang’aniwa na polisi kwenda kupekua nyumbani kwake
kuwa hakikuwa kitu kizuri.
Kova alipinga
Wakati Gwajima akisema hayo, Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bastola
waliyokutwa nayo wafuasi wa Gwajima haimilikiwi kihalali. “Tumegundua kuwa katika wale watu waliokuwa pale
akiwamo Gwajima mwenyewe, (bastola) haikuwa katika umiliki wao halali,
kwa hiyo hapa kuna kesi ya kupatikana na silaha bila kibali.”
Alizungumzia tuhuma kwamba polisi walimpekua mke
wa Gwajima, Kova alisema hakuna polisi waliofika nyumbani kwake kufanya
upekuzi wowote na kama wakitaka kufanya hivyo watafuata taratibu maalumu
za upekuzi. Akijibu swali kuhusu mahali Gwajima alipotakiwa
kutoroshewa, Kova alisema uchunguzi huo bado unaendelea na
utakapomalizika wahusika watafikishwa mahakamani.
Pia alipoulizwa kama Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo amemsamehe Gwajima, kwani polisi imng’ang’anie, Kova alisema;
“amesema anamsamehe lakini haingilii mambo ya sheria.”
Kuhusu sababu za Gwajima kuzimia wakati akihojiwa, Kova alisema
anayepaswa kuulizwa kwa nini alianguka wakati akihojiwa na polisi ni
Gwajima mwenyewe. “Siri za mahojiano huwa hazitolewi kabla ya
ushahidi mahakamani, sababu ya kupata shock (mshtuko) atajua mwenyewe,
kwa kuwa ukifanyiwa jambo ukafurahi au ukachukia wewe ndiyo unajua
ilikuwaje, chochote kitakachotokea ukicheka, ukinuna, ukizimia, wewe
ndiyo tukuulize ilikuwaje mpaka ukazimia kwa sababu hisia unazipata
wewe,” alisema Kova.
Wakili wa Gwajima
Wakili wa Gwajima, John Mallya alisema wakati wa
mahojiano, hawakutumia muda mrefu baina ya mteja wake na Polisi na kwa
kuwa mahojiano hayo hayajakamilika, yataendelea baada ya kutoka
hospitali. “Muda mwingi waliutumia polisi kujiandaa, walidai
kwamba walikuwa hawajajiandaa, hivyo kusema kwamba alihojiwa muda mrefu
si sahihi.”
Akizungumzia waliotaka kumtorosha alisema: “Jana
(Juzi) nilikwenda Oysterbay Polisi nikaambiwa wamehamishiwa Central
(Kituo Kikuu) lakini sijapata taarifa za kina za tukio hilo.”
Alisema silaha iliyokamatwa hajaiona wala
kuthibitisha kwamba ni ya mteja wake, hivyo ukweli wa tukio hilo
ataueleza baada ya kupata taarifa za kina. “Tuna mambo ya kujiuliza. Je, kipindi polisi
wanakagua hilo begi kulikuwa na mtu gani asiyefungamana nao? Haya ni
mambo ambayo yanahitaji ufafanuzi lakini kwa sasa nipeni muda
nifuatilie,” alisema.
Makonda amtembelea
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye
alikuwa amemwandikia Gwajima barua akimwita ofisi kwake, jana mchana
alimtembelea hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali kiongozi huyo
lakini akasisitiza kuwa nia yake bado ipo palepale. “Nilimtaka leo aripoti ofisini kwangu lakini kwa
bahati mbaya anaugua na amelazwa. Nitakwenda kumuona ili nijue hali yake
ikoje,” alisema Makonda kabla ya kufunga safari kwenda hospitali
alikolazwa.
Alisema pia atataka kiongozi huyo wa kiroho
amweleze anavyoelewa maana ya uhuru wa kuabudu unaoelezwa katika Katiba,
usajili wa taasisi yake na katiba ya taasisi hiyo. “Mimi ni mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Niliagiza polisi
wamkamate na baadaye wakimaliza kumhoji aje kwangu pia atahojiwa na jopo
la watu 20,” alisema Makonda.
Viongozi wamiminika
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba jana alikuwa kiongozi wa pili wa kisiasa kufika
hospitalini hapo kumjulia hali Gwajima, baada ya Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa aliyefika kwa mara ya kwanza Jumamosi na kurudi tena
jana.
Profesa Lipumba ambaye hivi karibuni pia aliishiwa
nguvu wakati akihojiwa na polisi, alisema kitendo kinachofanywa na
jeshi hilo cha kutumia nguvu kinatakiwa kukemewa kwa nguvu zote.
Akizungumza baada ya kumjulia hali Gwajima,
alisema yeye ni miongoni mwa waliopatwa na hali hiyo akiwa mikononi mwa
polisi kutokana na kuacha kuuliza suala husika na kutishatisha, kusumbua
sumbua, kitu kinachomfanya anayehojiwa kujisikia vibaya na hata
kupoteza fahamu. Dk Slaa alisema kinachofanywa na polisi ni
upotoshaji na hapingi wala haingilii kinachoendelea kati Gwajima na
Pengo, bali analaani kitendo cha polisi kupotosha ukweli.
Dk Slaa alisema polisi wanapotosha ukweli kwa
kuwaeleza wananchi kitu ambacho hakina ukweli kwa masilahi yao kama
ambavyo wamekuwa wakiwafanyia viongozi wa siasa, akiwamo yeye. Alisema kitendo kilichomkuta Gwajima hata yeye
kiliwahi kumkuta alikamatwa na bastola aliyoisajili na kuilipia kila
kitu, siku iliyofuata polisi wakamtuhumu kuwa ni jambazi anamilikia
silaha isivyo halali. “Mimi nasema waache wawapeleke mahakamani, ukweli utabainika,” alisema Slaa.
Maaskofu wahoji mambo manne
Wakati huohuo; maaskofu na wachungaji kutoka
makanisa mbalimbali wametoa tamko wakihoji maswali matatu kuhusu tukio
lililompata Askofu Gwajima.
Akitoa tamko hilo, Askofu wa Kanisa la Pentekoste
Agizo Kuu, Dk Mgullu Kilimba alisema wanajiuliza ilikuwaje Gwajima aende
akiwa mzima atoke akiwa mahututi? “Tumeshindwa kuelewa nini kimempata mwenzetu huyu.
Tunajiuliza je, vyombo vya usalama vimekuwa siyo sehemu salama kama
zamani?” alihoji.
Kuhusu tuhuma za kutoroshwa kwa Gwajima, maaskofu hao wamehoji:
“Kama alikuwa anaona ugumu wa kutoroka akiwa mwenye afya tele, itakuwaje
rahisi kutoroshwa akiwa mahututi na kwenye ulinzi mkali wa polisi?”
Pia walihoji kuhusu mlalamikaji wa kesi dhidi ya
Gwajima aliyetajwa kwa jina la Aboubakar, wakisema si mtu sahihi kwa
sababu hawezi kuonyesha ameumizwa kiasi gani na matamshi ya Gwajima.
Hata hivyo, Kova alisema hawamtambui mtu huyo wala hajui lolote
kuhusiana na mlalamikaji huyo aliyetajwa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment