
Kompyuta ni moja ya nyenzo nzuri za Tehama inayoweza kusaidia mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji. Kuanzia mwaka 2011 hadi 2013, nilikuwa mmoja wa
wawezeshaji wa mradi wa kuwawezesha walimu wa shule za sekondari kutumia
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika mchakato wa
ufundishaji na ujifunzaji.
Mradi huu ujulikanao kwa jina la Science, Maths
and English -ICT Project, ulikuwa unatekelewa na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi. Mradi ulilenga masomo ya sayansi, hesabu na lugha
ya Kiingereza. Kwa mujibu wa tafiti, masomo haya yalionekana kuwasumbua
wanafunzi, hivyo mradi ulikuwa ni mpango wa majaribio wa kutafuta namna
bora ya kukabiliana na changamoto hii shuleni.
Walimu walifundishwa namna ambavyo wangeweza kutumia kompyuta pamoja na vifaa vingine kama projekta kwenye ufundishaji.
Lengo kuu lilikuwa ni kutumia Tehama katika
kurahisisha ufundishaji wa dhana ngumu ambazo hata pamoja na ufafanuzi
wa mwalimu, bado zisingeweza kueleweka kwa wanafunzi. Kwa mfano, katika somo la Biolojia, mada kama za
mifumo ya mmeng’enyo wa chakula, damu na utoaji taka, mwalimu anaweza
kutumia vifaa vya Tehama kutazama video au picha zinazoonyesha ufanyaji
kazi wa mifumo hiyo.
Zana za Tehama
Katika makala haya, nalenga kumuelekeza mwalimu
namna anavyoweza kupata zana za kidijitali za kufundishia na kujifunzia
na anavyoweza kuzitumia. Zana za kidijitali za kufundishia na kujifunzia
zinaweza kuwa ni video, tovuti, picha mnato na za kucheza, sauti. Lakini
pia unaweza kutumia maandishi yaliyomo kwenye vitabu au kwenye
majarida.
Kwa wanaopendelea picha za kucheza, lazima wawe na
kompyuta zenye vitumizi kama vile Java na adobe flash player. Vitumizi
hivi vinaweza pia kupakuliwa mitandaoni. Moja ya tovuti nzuri zenye mkusanyiko wa zana za
kidijitali za kufundishia na kujifunzia ni PHET. Hadi sasa, tovuti hii
ina zaidi ya maelezo milioni 200 ya masomo ya Kemia, Fizikia, Biolojia,
Hisabati na mengineyo.
Zana hizi zilizomo kwenye tovuti hii ni za bure.
Mwalimu, mwanafunzi au mwingine yeyote hana haja ya kuzinunua, ila
unaweza kuchangia kama sehemu ya kuwezesha timu ya waandaaji kufanya
kazi yao kwa uzuri zaidi. Habari njema pia ni kuwa, maelezo haya katika tovuti ya PHET
huweza kupakuliwa kirahisi na kuweza kutumiwa bila hata ya kuwa na
intaneti. Jambo la kufanya ni kupakua “installer” yake na kisha kuziweka
kwenye kompyuta yako.
Kompyuta kama zana
Tovuti nyingine nzuri ni Absorblearning.com.
Tovuti hii ina mkusanyiko wa video, maelezo, na picha katika masomo ya
Kemia, Fizikia, Hisabati, na elimu ya elektroniki. Hata hivyo, zana za kidijitali katika tovuti hii zinahitaji kulipiwa ili uweze kupakua na kutumia bila intaneti.
Uzuri wake ni kuwa, inawezekana kutumia zana hizi ukiwa umeunganishwa na intaneti. Ukitaka kutumia tovuti hii, chagua somo
unalohitaji kwa kuingia kwenye absorb Chemistry, absorb Physics, absorb
Mathematics, absorb advanced physics au absorb Electronics na kisha
nenda kwenye kiunganishi kinachoonyesha idadi ya zana zilizopo kwenye
somo husika. Kisha tafuta zana kulingana na kile unachokisoma.
Mtandao wa YouTube pia una video nyingi na nzuri
kwa ajili ya walimu na wanafunzi. Tutorvista ni moja ya watumiaji wa
YouTube wanaopakia video za kielimu za masomo ya sayansi kwa shule za
sekondari.
Unaweza kuzipakua video hizo na kuzitumia wakati wowote bila ya kunganishwa kwenye intaneti. Ili kukwepa gharama zaidi za intaneti, ni vyema mwalimu au mwanafunzi akapakua video anazoona zinafaa kuliko kuziangalizia mtandaoni.
Unaweza kuzipakua video hizo na kuzitumia wakati wowote bila ya kunganishwa kwenye intaneti. Ili kukwepa gharama zaidi za intaneti, ni vyema mwalimu au mwanafunzi akapakua video anazoona zinafaa kuliko kuziangalizia mtandaoni.
Moja ya kitumizi kizuri cha kupakulia video ni
‘internet download Manager’ (IDM). Kama ni mara yako ya kwanza kuitumia
kwenye kompyuta yako, utaweza kuitumia kwa siku 30 na kisha utatakiwa
kuinunua. Baadhi ya tovuti nyingine ambazo unaweza kupata
zana za kidijitali za kufundishia na kujifunzia ni pamoja na Math open
reference iliyo na mkusanyiko wa maelezo ya mada ya jiometri kwa shule
za sekondari na learnerstv, yenye mkusanyiko wa zana za masomo
mbalimbali.
Kompyuta kama zana
Pamoja na kuwa kwa sasa, walimu wengi wanamiliki
kompyuta, changamoto iliyopo ni kuwa, wengi hawana mazoea ya kutumia
kompyuta na mtandao wa intaneti katika ufundishaji. Nakumbuka katika shule fulani, ilikuwa vigumu kuwashawishi
walimu kuandaa notisi, maandalio na maazimio ya kazi kwa kutumia
kompyuta.
Hali kadhalika wanafunzi wengi wanatumia kompyuta na simu kwa mambo yasiyo ya kimasomo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment